MSIMU wa Ligi Kuu 2023/2024 unakaribia ukingoni na timu pamoja na wachezaji wanakaribia kuvuna kile walichokipanda ambacho ni ama kumaliza vizuri au kumaliza vibaya pindi mizunguko 30 ya ligi itakapokamilika.
Timu mbili ambazo zitamaliza zikiwa mkiani mwa msimamo wa ligi zitashuka daraja moja kwa moja na mbili zitakazomaliza nafasi ya 13 na 14 zitacheza mechi za mchujo ili kuwania kubaki ligi kuu.
Wakati zikibaki raundi chache kabla ya msimu kumalizika, wapo wachezaji ambao wameonyesha juhudi na uwezo wa kufumania nyavu katika timu zao japo zinaonekana hazipo katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi na itakayoshindwa kuchanga vyema karata itashuka daraja.
Mtibwa Sugar iko mkiani mwa msimamo wa ligi na kabla ya mechi dhidi ya JKT Tanzania jana ilikuwa imekusanya pointi 17 katika michezo 22 iliyocheza.
Pamoja na kufanya vibaya kwa Mtibwa Sugar kwenye Ligi Kuu msimu huu, mshambuliaji wake, Seif Karihe ameamua kutokuwa mnyonge kwa kufunga mabao ambayo pengine yatampa ulaji hapo baadaye na kabla ya kuivaa JKT Tanzania, alikuwa ameshapachika mabao manne.
Erick Okutu-Tabora United
Tabora United ni miongoni mwa timu zilizofunga idadi ndogo ya mabao kwenye Ligi Kuu msimu huu na hadi sasa imefumania nyavu mara 18.
Jambo la kushangaza ni theluthi moja ya mabao hayo yamefungwa na mchezaji mmoja tu ambaye ni Erick Okutu aliyepasia nyavu mara sita.
Mchezaji anayefuatia kwa ufungaji katika kikosi hicho cha Tabora United ni Nakibinge Ben ambaye amefumania nyavu mara nne.
Mashujaa FC imefunga mabao 19 tu kwenye Ligi Kuu na asilimia 36.8 ya mabao hayo yamefungwa na mshambuliaji wake Adam Adam.
Adam ambaye amewahi kuzichezea Polisi Tanzania na JKT Tanzania, hadi sasa amefumania nyavu mara saba kwenye ligi na anayemfuatia ndani ya kikosi cha timu hiyo ni Emmanuel Mtumbuka aliyefunga mabao mawili.
Najim Magulu-JKT Tanzania
Kabla ya mchezo wa jana baina ya timu yake na Mtibwa Sugar, Najim Magulu wa JKT Tanzania alikuwa ameshaifungia timu yake mabao matatu kwenye ligi sawa na Edward Songo na Dan Lyanga ambao kila mmoja amezitikisa nyavu za timu pinzani mara tatu.
Ikumbukwe idadi kubwa ya mabao ya JKT Tanzania msimu huu yamewekwa kimiani na viungo ambao wamefumania nyavu mara tisa.
Valentino Mashaka-Geita Gold
Msimu unaonekana kumwendea vizuri mshambuliaji wa Geita Gold, Valentino Mashaka licha ya timu yake kutokuwa na mwenendo mzuri kwenye ligi.
Mashaka hadi sasa amefunga mabao matano kati ya 19 ambayo yamepachikwa na timu hiyo na mwingine ambaye amejaribu angalau kuonyesha tatizo sio yeye bali timu, Tariq Kilakala, amefunga mabao manne.
Haonekani kama anaweza kusalia Ihefu SC msimu ujao kutokana na usajili wa mastaa wengi wa nje na ndani ya nchi ambao timu hiyo imepanga kuwasajili dirisha kubwa la usajili mara baada ya msimu huu kumalizika.
Hata hivyo Mgunda ni fundi ambaye hawezi kulala na njaa kwani mabao matatu ambayo ameifungia msimu huu, yanaweza kumfanya asikose timu ambayo itamnasa.