Bajeti ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), imepitishwa na wabunge huku fedha ya bajeti zikiongezeka.
Ongezeko hilo ni kutoka Sh9.18 trilioni iliyoidhinishwa mwaka 2023/2024 hadi kufikia Sh10.125 trilioni mwaka 2024/2025.
Ndani ya bajeti hiyo, Serikali imepanga kutumia Sh1.02 trilioni kupitia fedha zake na za washirika wa maendeleo kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli katika sekta ya elimu.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Mohamed Mchengerwa, ameelekeza fedha hizo kutumika katika vipaumbele 13 elimumsingi na sekondari.
Vipaumbele vitakavyoelekezwa kupitia fedha hizo ni ujenzi wa vyumba vya madarasa 6,357, matundu ya vyoo 1,482, umaliziaji wa mabwalo 362 kati ya mabwalo hayo 15 ni msingi na 347 ni ya sekondari na umaliziaji mabweni 36 shule za awali na msingi;
Pili, ni ujenzi wa shule mpya 184, nyumba za walimu 184 na mabweni 186 katika shule za sekondari; ununuzi wa vifaa vya Tehama shule za awali tatu , msingi 400 na shule za sekondari 500;
Kipaumbele kingine ni ununuzi wa kemikali za maabara za shule mpya 234; utoaji wa ruzuku ya elimu bila ada kwa shule za msingi 17,986 na sekondari 4,894;
Pia ununuzi na usambazaji wa vitabu 2,215,877 kwa shule za msingi na 11,880,828 kwa shule za sekondari na vitabu na vifaa vilivyoboreshwa vya kufundishia na kujifunzia elimu ya awali kwenye shule 4,500;
Eneo lingine ni ununuzi wa vifaa saidizi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika shule 130 za msingi na sekondari; 87, kutoa mafunzo ya maadili kwa wakuu wa shule 17,220, viongozi na watumishi wa TSC 460 katika ngazi ya wizara na wilaya;
Vilevile kutoa mafunzo endelevu ya walimu kazini (MEWAKA) kwenye shule za awali na msingi halmashauri 140; kutekeleza mpango wa shule salama kwa shule za awali na msingi 2,500;
Vipaumbele vya mwisho ni kuanzisha madarasa janja (smart classes) 10 kwa ajili ya ufundishaji mubashara katika halmashauri 10; Kuandaa mwongozo wa mafunzo elekezi kwa walimu wapya wanaoajiriwa katika shule za umma; na mwisho uandaaji wa kihunzi cha walimu wanaojitolea.
Mchambuzi wa masuala ya elimu, Magabilo Masambu, anasema vipaumbele vyote vilivyowekwa ni vizuri kwani vinalenga kuinua elimu.
“Lakini Serikali imekuwa ikiweka nguvu kubwa kwenye miundombinu badala kuangalia maslahi ya walimu. Kuna mwalimu anaishi kijijini ambapo tangu anaajiriwa, yeye mawazo yake anataka kuhama tu kutokana na mazingira magumu ya kazi,”anasema.
Massambu anasema ni muhimu walimu wanaofanya kazi kwenye mazingira magumu waangaliwe kwani wapo ambao hutumia Sh30,000 kufika kazini lakini mshahara wake ni sawa na anayefanya kazi mjini.
Jambo lingine anadokeza kuwapo kwa watumishi wachache wa kadan ya ualimu hasa wa masomo ya sayansi, akisisitiza idadi ya wanafunzi ni wengi ikilinganishwa na walimu.
Anaongeza kuwa hata wachache waliopo wanapostaafu hakuna ingizo jipya kuziba mapengo yaliyopo, hivyo miundombinu inaweza kuboreshwa lakini ikashindwa kutumika kutokana na uhaba wa wataalamu.
“Lipo jambo lingine la wataalamu wa maabara, watalamu hawa hawajaajiriwa kwenye shule badala yake wanaofanya kazi hizo ni walimu wa masomo ya sayansi ambao nao walijifunza wakati wa mitihani tu,”anasema.
Massambu anasema vifaa vya maabara vinavyonunuliwa na Serikali matumizi yake ni hafifu, kwa sababu hakuna hao wataalamu wa maabara kwenye shule zinakopelekwa vifaa hivyo.
Kwa upande wa upanuzi wa madarasa, anasema ni hoja anayoiunga mkono kwani shule nyingi zina mrundikano wa wanafunzi darasani licha ya juhudi zinazofanyika.
“Japo ujenzi huu upo kila mwaka, tunapaswa kuuangalia upya, ni vizuri tuje na mfumo wa wanafunzi kuingia darasani kwa awamu asubuhi na mchana tusiwe tunajenga madarasa bila kikomo,”anaeleza.
Hoja nyingine inaibuliwa na mchambuzi wa masuala ya kijamii, Dk Faraja Kristomus, anayesema changamoto kubwa wanayopata Tamisemi ni upatikanaji wa fedha inayotengwa kwa ajili ya bajeti.
“Kama fedha zote zitapatikana ndani ya mwaka wa fedha, matumaini makubwa ya kurekebisha miundombinu shuleni yataimarika sana,”anaeleza.
Anaeleza shida nyingine iliyopo sekta ya elimu ni walimu kukimbia vijijini kutokana na mazingira magumu ya kazi.
Mazingira anayotaja ni idadi kubwa ya wanafunzi wanaofundishwa na mwalimu mmoja na ukosefu wa madarasa na nyumba za kuishi kunawafanya walimu kukosa morali ya kufundisha.
Anachoshauri ili kuwe na ufanisi wa utekelezaji wa vipaumbele hivyo, ujenzi wa shule mpya ungepewa kisogo kwanza badala yake kero zikatatuliwe kwenye shule ambazo zilijengwa na hazijakamilika na hazina walimu.
Hofu aliyonayo ni ongezeko la shule zenye changamoto wakati zipo ambazo hazijatatuliwa mpaka sasa.
“Baadhi ya miradi imeelezwa kuwa itaelekezwa katika halmashauri 140 sasa hapa nchini tuna halmashauri 184. Hatujajua hizi zingine kama zimejitosheleza, kwa ujumla utoaji wa fedha kutekeleza miradi inayoahidiwa bado ni changamoto,”anaeleza.
Maoni hayo si tofauti na ya mdau wa elimu, Alistidia Kamugisha,anayesema vipaumbele vilivyowekwa ni vya msingi katika kuboresha elimu ya Tanzania.
“Yapo matundu ya vyoo nimeyaona kwenye hivi vipaumbele, tunapopanga mafunzo kwa walimu mara nyingi shule za Serikali ndio zinalengwa hakuna muongozo wa kuwalazimisha wamiliki wa shule binafsi ili walimu wao wapewe mafunzo na kwenye shule hizo tuna watoto wetu wengi,”anasema.
Alistidia anasisitiza kuwa Tamisemi iangalie namna ya kuhakikisha hata shule binafsi inasimamia mafunzo kwa walimu.
Jambo lingine kuhusu mazingira anasema hakuna juhudi inayofanyika kuwapa wanafunzi elimu namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, jambo ambalo Serikali inapaswa kuhakikisha suala la elimu hiyo linaanzia chini.
Kuhusu shule salama, anasema kila shule nchini inapaswa kuwa na shule salama na hilo linapaswa kuwa kipaumbele kwa Taifa.
“Kama ni mpango wa shule salama uangalie wote na hii iwe katika kuzijengea uwezo kamati za shule, watoto na hii yote inapaswa kuwa kwenye bajeti. Tusitegemee shule chache tu kwa sababu ya mfadhili katoa fedha kidogo bali tuwekeze kupitia fedha zetu,”anasema.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu kivuli wa chama cha ACT- Wazalendo Hamidu Bobali, anasema mipango hiyo ni mizuri ikiwekwa kwenye utekelezaji.
Wasiwasi wa Bobali, kwa miaka saba utekelezaji wa bajeti anasema umekuwa wa kiwango kidogo, akitolea mfano bajeti ya mwaka jana ambayo hadi kufikia Machi mwaka huu, ilitekelezwa kwa asilimia 64 hadi 68.
“Kuna tatizo la utoaji wa fedha na inakopelekwa, kwa bahati mbaya miradi ya elimu fedha zake zinapelekwa kwa kiwango kidogo. Kwa mwaka jana, mpango wa ujenzi wa madarasa ya Tehama na maeneo mengine kwa kiwango kikubwa fedha zake hazikupelekwa,” anasema.
Bobali anayasema hayo wakati ambapo, ripoti kuu ya ukaguzi wa serikali za mitaa kwa mwaka wa fedha 2022/23 ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), imebaini upungufu wa ruzuku ya elimu bila malipo.
Kwenye ripoti hiyo ilibainika upungufu wa ruzuku ya elimu bila malipo iliyotolewa kwa mamlaka za serikali za mitaa 15 kwa ajili ya shule za msingi na sekondari, ikiwa jumla ya Sh 1.25 bilioni kati ya Sh11.83 bilioni zilizokuwa zimepangwa katika bajeti ya kipindi hicho.
Kwa mujibu wa CAG, fedha hizo zilikuwa muhimu kwa shule kupata rasilimali muhimu kama vile vifaa vya kufundishia na kujifunzia na kuwezesha ukarabati wa miundombinu na hatimaye kuchangia katika uboreshaji wa elimu.
Hoja nyingine Bobali anasema, msingi wa elimu ya Tanzania unatengenezwa kupitia mfumo wa elimu unaozingata mitalaa, akisema elimu lazima itangamanishwe na uchumi.
Anasema wakati wa utawala wa Mwalimu Julius Nyerere, siasa ya ujamaa na elimu ya kujitegemea vilifundishwa shuleni lakini sasa tupo katika uchumi wa kibebari na elimu iliyopo haiwaandai wanafunzi kuwa wataalamu na wagunduzi.
“Leo tunaandaa Dira ya Taifa ya 2025 hadi 2050 ni lazima dira ya Taifa na mfumo wa elimu, viendane hatuwezi kupata maendeleo kama hujajengea msingi kwenye elimu. Elimu yetu isiandae wapiga debe, wachuuzi na saidia fundi, badala yake iandae wataalamu,”anaeleza.