Majaliwa ataka uwazi utekelezaji miradi ya umwagiliaji

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametaka uwazi na usimamizi madhubuti wa fedha katika utekelezwaji wa miradi ya umwagiliaji nchini.

Majaliwa ametoa maelekezo hayo kwa watendaji watakaohusika na usimamizi wa miradi hiyo, akisisitiza kufanya hivyo kutachagiza kukamilika haraka kwa kazi hizo.

Kauli ya mtendaji mkuu huyo wa Serikali inakuja katika kipindi ambacho, Serikali imeweka dhamira ya kutekeleza miradi lukuki ya umwagiliaji ili kuboresha sekta ya kilimo.

Katika maboresho hayo ya sekta ya kilimo, Serikali imeweka dhamira ya kuhakikisha inaongeza mchango katika pato la taifa kutoka asilimia 26 hadi 50 mwaka 2030.

Majaliwa ameyasema hayo jijini Dodoma leo Jumanne, Aprili 30, 2024 alipohutubia katika hafla ya utiaji saini wa mikataba ya ujenzi, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa miradi ya umwagiliaji.

Amesema ni muhimu watendaji watakaohusika na usimamizi wa miradi hiyo kuzingatia ufanisi na usimamizi imara wa fedha ili kazi zifanyike kwa haraka.

Pamoja na ufanisi, Majaliwa ametaka uwazi katika utekelezaji wa miradi hiyo, ili kuepuka ubadhirifu wa fedha na miradi kutekelezwa kinyume na matarajio.

“Fedha hizo ni kodi za wananchi wa Tanzania, zitumike kuwanufaisha Watanzania wote,” amesema.

Agizo lingine alilolitoa kupitia jukwaa hilo ni watendaji hao kuhakikisha ubora wa miradi unalingana na thamani halisi ya fedha iliyotolewa kwa ajili ya utekelezaji.

Lakini, ametaka kwa miradi itakayotekelezwa kwa njia ya Force Account kipaumbele cha ajira kitolewe kwa wananchi wa jirani na maeneo ya utekelezwaji.

Katika hatua nyingine, Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kusimamia kilimo cha umwagiliaji ndiyo maana imeongeza bajeti kufikia Sh361.5 bilioni mwaka 2023/2024 kutoka Sh46.5 bilioni ya mwaka 2021/2022.

“Matarajio ya Serikali ni kuona miradi inayotekelezwa itakamilika kwa wakati na kwa ufanisi mkubwa ili kuwezesha kutimia kwa azma ya Serikali ya kuongeza mchango wa sekta ya kilimo katika Pato la Taifa,” amesema.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema mikakati ya Serikali ni kuanza kutumia maji ya Ziwa Tanganyika katika miradi ya kilimo cha umwagiliaji.

Hilo, amesema litaanza na mikoa ya Katavi na Rukwa na baada ya Bunge la bajeti, upembuzi wa kina na yakinifu utafanyika ili maji hayo yasafirishwe hadi Simiyu na Tabora, maeneo ambayo aghalabu huwa na ukame.

“Baada ya Bunge la bajeti kukamilika tunatarajia kuanza kuyatumia maji ya ziwa Tanganyika katika shughuli za kilimo na uzuri mitambo tunayo naamini jambo hili litafanikiwa,” amesema.

Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), Raymond Mndolwa amesema mikataba 24 imesainiwa na kati ya hiyo, 14 ya ujenzi kwa kutumia wakandarasi yenye thamani ya Sh248.7 bilioni, sita ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa kutumia Washauri Elekezi yenye thamani ya Sh9.35 bilioni.

Miradi minne, amesema itatekelezwa kwa kutumia wataalamu wa ndani kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji yenye thamani ya Sh16.95 bilioni.

Related Posts