Dar es Salaam. Matunda ya ziara ya siku tano ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Uturuki kwenye sekta ya elimu yataanza kuonekana mwaka 2025, imeelezwa.
Kuanzia Aprili 17 hadi 21, 2024 Rais Samia na ujumbe wake wakiwemo wadau wa sekta za fedha na wafanyabiashara walifanya ziara ya siku tano nchini Uturuki kwa mwaliko wa Rais wa nchi, Recep Tayyip Erdoğan.
Rais Samia alikwenda Uturuki ikiwa ni miaka 14 imepita tangu Rais wa Tanzania alipotembelea Taifa hilo, na miaka saba tangu Rais Erdoğan alipozuru Tanzania mwaka 2017.
Katika ziara hiyo, Tanzania na Uturuki zilisaini hati sita za ushirikiano, tatu kati ya hizo zinahusu sekta ya elimu.
Hayo yameelezwa leo Jumanne Aprili 30, 2024 na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Muhamed Mussa katika mjadala wa Mwananchi X Space wenye mada ya kuchambua safari ya kihistoria ya Rais Samia suluhu Hassan nchini Uturuki. Mjadala huo umeandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kwa ushirikiano na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC).
Waziri Lela amesema makubaliano yaliyoingiwa kati ya Serikali ya Tanzania na Uturuki kwenye sekta ya elimu yana walengwa mahususi na watafikiwa moja kwa moja.
“Huu ni ufadhili kwa ajili ya wanafunzi wa shule, tulisema rasmi utaanza mwaka 2025 kwa sababu mwaka huu utaratibu wa maombi umeshakamilika. Wanafunzi wote walio kidato cha sita walioko shuleni watapewa utaratibu wa kuomba ili kuwa katika orodha ya ufadhili.”
“Wale watakaofaulu vizuri watachukuliwa moja kwa moja katika ufadhili huu. Kwa nafasi za wataalamu wa vyuo vikuu, maeneo yaliyolengwa kwa fani, kwa watu wanaohitajika kujengewa uwezo watapelekwa moja kwa moja kwenye chuo husika.”
Waziri Lela amesema lengo la makubaliano hayo ni kuondoa changamoto ya kila wakati zinapopatikana nafasi za ufadhili watu wanashindwa kuomba kwa kukosa taarifa sahihi.
Alisema hayo alipojibu swali la mchangiaji katika mjadala huo, Mussa Hassan, aliyeishauri Serikali kuhakikisha inafikisha taarifa kwa wananchi kuhusu fursa zilizopo nchini Uturuki hasa katika sekta ya elimu.
Amesema, “Mfano Uturuki wanataka mtu aliyemaliza kidato cha sita, taarifa zinapaswa kuwafikia wahusika mapema wakiwa wapo shuleni ili kuandaa nyaraka muhimu, kwa ajili ya wakati wa kuomba nafasi mchakato utakapoanza.”
Waziri Lela amesema Uturuki ni miongoni mwa mataifa yaliyopiga hatua katika vyuo vya kati, hivyo hatua ya Tanzania kuingia makubaliano katika sekta ya elimu na Taifa hilo itawezesha wanataaluma wa vyuo vya kada hiyo kuongeza taaluma yao.
Waziri Lela amesema: “Itasaidia kupata uzoefu kutoka kwa wenzetu namna walivyoweza kufanikiwa katika eneo hilo, kwa sasa wizara zetu zinaandaa mpango kazi wa kulitekeleza.”
Amesema, “Moja tulilosaini kwa upande wa Zanzibar ni maalumu kwa mwanafunzi aliyemaliza shule, atapata fursa ya kuomba ufadhili uliotangazwa kupitia taasisi husika.”
Amesema lengo la ufadhili uliosainiwa kwa upande wa Zanzibar ni kwa ajili ya wanafunzi waliofaulu vizuri katika mtihani wa kidato cha sita.
“Kwa hiyo mwanafunzi akimaliza kidato cha sita akifaulu vizuri katika masomo ya sayansi atapatra ufadhili wa asilimia 100 kusoma vyuo vikuu Uturuki katika ngazi ya Shahada. Ni maalumu kwa wanafunzi 50 watakaofaulu vizuri,” amesema.
Mwenyekiti wa Diaspora nchini Uturuki, Dk Bakari Ramadhani amesema mikataba iliyosainiwa kati ya Tanzania na Uturuki ya kutoa ufadhili wa masomo itasaidia wanafunzi wanaokwenda nchini humo kuwa na usimamizi mzuri wakati wote.
Dk Ramadhani amesema awali tatizo kubwa lilikuwa wanafunzi kupata taarifa sahihi kuhusu ufadhili unaotolewa katika Taifa hilo.
“Zamani ilikuwa rahisi kupata ufadhili kwa kuja moja kwa moja, lakini hapa katikati zilipungua na wanafunzi walikuwa wanakuja kwa kutumia fedha za wazazi wao, ndiyo maana walikuwa wanakuja kwa kutumia mawakala tofauti.
“Hatua hiyo ilisababisha kutokea kwa tatizo la kuwa na mawakala wasiokuwa waaminifu wanaowadanganya wanafunzi ambao wakifika Uturuki wanapata shida,” amesema.
Katika hatua nyingine, Dk Ramadhani ameshauri Serikali kuwatumia Watanzania wanaoishi kwenye Taifa hilo katika masuala mbalimbali, ikiwemo majadiliano yenye lengo la kuingia mikataba baina ya mataifa hayo.
“Unakuta unaalikwa kwenye majadiliano kama mtafsiri (mkalimani) lakini hujui lolote, sasa hili kwangu ni changamoto. Ingekuwa tunapewa fursa mapema kabla ya watu hawa kufika na sisi kufanya utafiti kwa faida ya nchi yetu.”
“Uturuki kuna changamoto ya lugha, lakini watu wake ni wepesi wa kufanya utafiti wa kujua kinachoendelea,” amesema Dk Ramadhani.
Pia, amezungumzia hatua ya Serikali ya Tanzania kuingia makubaliano ya kuwajengea uwezo wakufunzi, akisema ni nzuri na kuna haja ya watu kuongeza elimu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), Theobald Sabi amesema sera ya Serikali ya diplomasia ya uchumi inatekelezwa kwa vitendo hivi sasa.
Sabi ametoa mfano wa ziara za Rais Samia nje ya nchi zinavyojumuisha wanahabari na sekta binafsi, akisema ni namna mahususi ya kutekeleza sera hiyo.
Akizungumzia ziara ya Uturuki akiwa ni miongoni mwa watu walioshiriki amesema ilikuwa nzuri, hasa kwa wafanyabiashara wa Tanzania na Taifa hilo lililopiga hatua za kiuchumi.
“Uturuki ina fursa nyingi ambazo Taifa na sekta binafsi tunaweza kushirikiana kukuza uchumi na kutengeneza ajira,” amesema Sabi.
Amepongeza hatua ya Rais Samia kuiunganisha Tanzania na dunia, hasa kusaidia sekta binafsi nchini.
Amesema Tanzania ina nafasi kubwa ya kuwavutia wawekezaji kutoka Uturuki kutokana na fursa zilizopo.
Sabi amesema kuna fursa za kuwaleta wawekezaji wa Uturuki nchini kuanzisha viwanda kutokana malighafi zilizopo.
“Kupitia viwanda tutazalisha ajira na kuuza nje ya nchi bidhaa, naiona Tanzania ikiwa katika nafasi nzuri ya kupokea wawekezaji kutoka Uturuki watakaosaidia kukuza sekta binafsi.”
“Msisitizo mkubwa ni uzalishaji wa viwanda ili kuongeza thamani ya mazao, lakini ipo nafasi ya kushirikiana katika kilimo na mifugo,” amesema Sabi.
Pia amesema sekta za benki za Tanzania na Uturuki hazina tofauti, bali zinafanana katika maeneo mbalimbali.
Kutokana na hilo, amesema benki za Tanzania bado zina nafasi kubwa za kuwasaidia wafanyabiashara kuanzisha shughuli za uzalishaji nchini, lakini kutokana na ukubwa wa uchumi wa Taifa hilo, benki za Uturuki ni kubwa zaidi.
“Mabenki ya Tanzania yapo katika nafasi ya kufadhili miradi itakayowezesha biashara kati ya Tanzania na Uturuki kuendelea kukua na kufikia lengo la Dola (za Marekani) bilioni 1 ndani ya mwaka mmoja,” amesema Sabi, ambaye ni Mwenyekiti wa Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA).
Sabi amewaeleza Watanzania sekta ya kibenki inaenda vizuri na inachukua hatua za kuzisaidia taasisi zinazoanza zenye lengo la uzalishaji na kusafirisha bidhaa nje ya nchi.
“Wawekezaji waje kutoka Uturuki washirikiane na wafanyabiashara wetu kuanzisha miradi, soko lipo kubwa limezunguka, tuna kila sababu ya kufanikiwa, na Serikali imeboresha mazingira,” amesema Sabi.