Mwanza. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na mlezi wa timu ya Pamba Jiji, Said Mtanda amesema hatamvumilia mtu yeyote atakayeingiza U-Simba na U-Yanga ndani ya timu hiyo itakapokuwa inacheza mechi zake za Ligi Kuu Bara msimu ujao.
Mtanda ametoa kauli hiyo leo Aprili 30, 2024 kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini hapa wakati akizungumza na maelfu ya mashabiki kwenye hafla ya kuipokea timu ya Pamba ambayo ilikuwa safarini kutoka jijini Arusha ilikopanda daraja baada ya kuichapa Mbuni FC mabao 3-1 mwishoni mwa wiki iliyopita.
Kiongozi huyo amesema yeye ni shabiki mkubwa wa Yanga na mtangulizi wake, Amos Makalla ni shabiki wa Simba lakini hawatakubali ushabiki huo uingie kwenye ndani ya Pamba Jiji na kuwavuruga, hivyo yeyote atakayefanya hivyo atawapisha.
“Mimi ni shabiki mkubwa wa Yanga lakini Yanga haina uhusiano na timu hii ama kiongozi yeyote. Timu ya Pamba siyo tawi la timu yeyote ni timu ya ushindani, tutaunda timu itakayotoa ushindani na burudani ikiwa popote. Yeyote atakayetuingiza kwenye siasa za Simba na Yanga tutamtoa,” amesema Mtanda na kuongeza;
“Hersi Said (Rais wa Yanga SC) ni rafiki yangu nitamuomba ushauri namna timu yake inavyofanya vizuri itusaidie kujifunza, lakini pia Murtaza Mangungu (Mwenyekiti wa Simba SC) nitamuomba ushauri kwa nini wanafanya vibaya ili nasisi tujifunze tusifanye vibaya,” amesema.
Ameongeza kwamba dhamana aliyopewa ya kuipeleka Pamba Jiji ligi kuu ameitimiza huku akimpongeza muasisi wa mafanikio hayo, Amos Makalla ambaye alifanya kazi nzuri yenye heshima na kuahidi kuendelea kuwasiliana naye kwa mawazo mazuri yenye hekima ili kuwa na timu bora yenye ushindani.
“Mimi Mkuu wa Mkoa sitafurahia majungu katika soka la Mkoa wa Mwanza nataka vitendo. Na ili tusigombane nataka mnielewe mimi sipendi majungu na fitina nataka maendeleo. Kwa hiyo watu ambao wanajiandaa baada ya timu kupanda walete majungu milango kwao imefungwa lakini wale wanaotaka kuleta ushauri mzuri milango imefunguliwa,” amesema Mtanda.
Mlezi huyo ameshauri wamiliki ambao ni Halmashauri ya Jiji la Mwanza kuunda bodi ya wataalam itakayosimamia uendeshaji wa klabu hiyo ili iendeshwe kisasa na kitaalam.
“Hatutataka kuwa watu ambao tunajihusisha moja kwa moja na uendeshaji wa timu. Timu itaendeshwa kisasa na kitaalam kwa kufuata miongozo ya soka, sisi kazi yetu ni kuja kuulizwa kuomba ushauri,” amesema Mtanda.
Ameongeza: “Tunataka timu iwe huru na menejimenti ijiendeshe. Kazi ya usimamizi na uendeshaji siyo ya Mkuu wa Mkoa, Mkurugenzi wa Jiji, Kiomoni Kibamba najua utaunda menejimenti bora ya uendeshaji na sisi tutakushauri lakini hatutakuingilia.”