Dar es Salaam. Idadi ya wanaobainika kuwa na ugonjwa wa malaria imeongezeka, chanzo kikielezwa ni mabadiliko ya tabianchi yanayochangia ongezeko la mvua zinazosababisha uwepo wa mazalia ya mbu.
Wagonjwa wa malaria wametajwa kuongezeka kwa kipindi cha mwaka 2023, huku jamii ikitakiwa kuchukua tahadhari kwa kujikinga na ugonjwa huo, ikiwamo kutumia vyandarua vyenye dawa.
Takwimu zinaonyesha Zanzibar mwaka 2022 waliripotiwa wagonjwa 4,000 wa malaria, lakini mwaka 2023 kulikuwa na ongezeko kufikia wagonjwa 19,000, huku asilimia 80 kati yao wakitokea Mkoa wa Mjini Magharibi.
Tanzania Bara takwimu zinaonyesha mwaka 2022 kulikuwa na wagonjwa 3,478,875 na mwaka 2023 walikuwa 3,534,523 sawa na ongezeko la asilimia 1.6, huku vifo vikiongezeka kutoka 1,430 mpaka 1,954 mwaka 2023.
Akizungumza leo Jumanne, Aprili 30, 2024 alipofungua kongamano la Malaria kwa mwaka 2024, Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Tumaini Nagu amesema pamoja na ongezeko la wagonjwa, vifo vitokanavyo na malaria pia vinaongezeka.
Kongamano hilo lililoandaliwa na Taasisi ya Afya Ifakara (IHI) limewakutanisha watafiti, watunga sera, serikali na vyama vya jamii kujadili njia gani bora ya kutokomeza malaria nchini.
“Tumeona kwa mwaka huu na mwaka uliopita, mvua zimeongezeka na mabadiliko ya tabianchi yanasababisha ongezeko la malaria. Wanaougua wanaongezeka, hivyo tunatafakari kwa pamoja na wanasayansi kuona ni njia gani za kufanya ili kuitokomeza malaria kama janga la kijamii,” amesema.
Profesa Nagu amesema nchi ilipiga hatua katika kutokomeza malaria tangu mwaka 2015 na kupunguza idadi ya wagonjwa na vifo vya ugonjwa huo kati ya asilimia 60 na 65 japokuwa kwa mwaka jana 2022/2023 kulionekana ongezeko na mwaka 2024.
“Kuna ongezeko la asilimia moja na zaidi, pia hivi karibuni tunaona wagonjwa na vifo vinaongezeka, si kwamba vya kutisha ukilinganisha na mwaka 2015 tulikuwa na vifo 6,900 na sasa tunarekodi vifo 1,900 katika ongezeko hili, lazima tujitafakari na kuona ni hatua gani tunachukua kukabiliana nalo,” amesema Profesa Nagu.
Amewaagiza wanasayansi kuangalia jinsi wanavyoweza kutumia teknolojia kutengeneza njia za kudhibiti malaria, akitoa mfano mabadiliko ya tabianchi ni jinsi gani wanaweza kutumia akili bandia kufikisha ujumbe kwa wananchi namna ya kujikinga na ugonjwa huo.
Profesa Nagu amesema ni lazima kutumia mbinu mbadala kwani kuna changamoto nyingi, licha ya mabadiliko ya tabianchi.
“Tuna tatizo la usugu wa dawa za malaria si kwa wingi, lakini ni jambo lenye mwendelezo kwa hiyo na sisi tunapaswa kufanya bidii kuangalia ni namna gani tunakabiliana nalo kama nchi. Lakini wanasayansi na watafiti wahakikishe wanatafuta mbinu mbadala za kukabiliana na usugu, pia kudhibiti malaria,” amesema.
Licha ya changamoto za rasilimali fedha, amewaagiza waangalie namna ambavyo wanaweza kutumia chache zilizopo.
Amesema zipo afua ambazo bado ni changamoto kuzitekeleza, ikiwamo upuliziaji dawa ambao rasilimali fedha bado ni changamoto.
“Changamoto kwamba ni jinsi gani tunatoa kipaumbele kuhakikisha tunafanikisha hili na kuweka fedha maeneo ambayo yana uhaba kushughulikia malaria,” amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Afya ya Ifakara, Dk Honorati Masanja amesema wamepokea maelekezo hayo na kama taasisi wameshaanza kutumia akili bandia katika kazi mbalimbali.
“Tunatumia teknolojia ya akili bandia kupambana na malaria, ulimwengu wa sasa ni wa teknolojia changamoto ya mabadiliko ya tabianchi lazima twende nayo sawa, eneo la ukanda wa Afrika Mashariki wakati wa mvua malaria zinaongezeka nasi tunaangalia tabia za mbu kwa kufanya utafiti ukiwemo wa chanjo,” amesema Dk Masanja.
Baadhi ya wasimamizi wa sera waliohudhuria kongamano hilo, wameeleza umuhimu wa chanjo kwa watoto katika wakati huu ambao malaria inaongezeka.
Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi, Dk Faustine Ndugulile amesema chanjo ambayo tayari imeanza kutumika duniani, imefanyiwa tathmini ya ufanisi Tanzania na kuonekana yenye manufaa na takribani nchi tano Afrika inazitumia akihoji sababu za nchi kusuasua.
“Sisi kama wabunge tumekuwa tunaihoji Serikali, nipo kamati ya afya na mjumbe wa wabunge wanaopambana na malaria tulichoambiwa bado wanaweka sawa taratibu za ndani na nadhani ifikapo mwishoni mwa mwaka huu hizi chanjo zitaanza kutolewa nchini,” amesema Dk Ndugulile.
Amesema nchi imekuwa ikifanya tafiti nyingi za mabadiliko ya dawa na afua za malaria lakini changamoto utafiti umekuwa ukinufaisha nchi zingine.
Mbunge wa Nzega Vijijini, Dk Hamisi Kigwangalla amesema chanjo ni mojawapo ya afua ambayo ikitumika vizuri itapunguza vifo kwa kundi lengwa la watoto chini ya miaka mitano.
“Tanzania inaweza ikafaidika na kuleta chanjo kwa ajili ya kukinga watoto wetu na ugonjwa huu hatari wa malaria ni jambo zuri, utafiti umefanyika hapahapa nyumbani na IHI tunaamini Serikali itaingia katika mchakato wa sheria na wataalamu ione namna ya kuingiza chanjo nchini,” amesema.
Dk Kigwangalla amesema kuna manufaa kwa nchi kutenga fedha za kutosha kushughulikia malaria kwa kuwa zaidi ya asilimia 90 ya uwekezaji wa rasilimali fedha ni wafadhili.
Mbunge wa viti maalumu, Riziki Lulida amesema mafuriko yamekuwa chanzo cha ugonjwa huo, akiitaka Serikali kuangalia namna ya kupeleka afua za kinga maeneo yanayoathirika na malaria kwa sasa ikiwemo Kibiti na Morogoro.