HATIMAYE Pamba ya Mwanza imefanikiwa kurudi Ligi Kuu Bara tangu ishuke daraja 2001. Klabu hiyo ambayo sasa inatambulika kama Pamba Jiji, imepanda baada ya ushindi mnono wa 3-1 dhidi ya Mbuni ya Arusha kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini humo.
Pamba, klabu yenye rekodi yake barani Afrika inarudi Ligi Kuu baada ya kukaa chini kwa miaka zaidi ya 20. Pamba siyo klabu ndogo kwa hiyo kurejea kwake Ligi Kuu kunastahili simulizi za klabu hii hasa namna ilivyoshuka. Timu hiyo ilishuka 2001, mwaka ambao timu saba zilishuka; Pamba yenyewe, Lipuli ya Iringa, Reli ya Morogoro pamoja na Kagera Stars ambayo sasa ni Kagera Sugar. Halafu kulikuwa Milambo ya Tabora, Majimaji ya Songea na 44 KJ ya Mbalizi Mbeya.
Pamba ilishuka kwa kuponzwa na Kagera Stars, bila hivyo isingeshuka mwaka huo. Ligi ya mwaka 2001 ilikuwa na timu 24 zilizogawanywa katika makundi mawili A na B, na ilichezwa kwa awamu mbili; hatua ya makundi, na Sita Bora.
Timu tatu za juu kutoka kila kundi zilifuzu Sita Bora hatua iliyotumika kumtafuta bingwa wa Bara na timu za kufuzu Ligi Kuu ya Muungano. Timu tatu za chini zilishuka moja kwa moja. Kagera Stars ilikuwa ya mwisho, ikifuatiwa na Lipuli na Reli ya Morogoro.
Hizo ndizo timu zilizopaswa kushuka daraja kutoka kundi A.
Pamba ilikuwa ya nne kutoka mwisho hivyo ilistahili kubaki salama, lakini ilishuka…kwa kuponzwa na Kagera Stars.
Kagera Stars ilikuwa timu ya wananchi wa Mkoa wa Kagera. Kabla ya kuitwa Kagera Stars, timu hiyo iliitwa RTC Kagera ikimilikiwa ja kampuni ya biashara ya mkoa, RTC.
Baada ya kampuni hiyo ya serikali kufilisika, RTC Kagera ikachukuliwa na wananchi, na ndipo ikaitwa Kagera Stars.
Lakini mwaka 2001 wananchi hao wakaelemewa na mzigo wa kuiendesha timu na kuitelekeza. Kagera Stars walishindwa kuendelea na ligi baada ya mechi 13 tu, pale walipokosa kufika uwanjani kwenye mechi tatu mfululizo.
FAT ikawaondoa kwenye ligi na matokeo yao yote kufutwa. Hadi wanaondolewa walikuwa mkiani mwa msimamo wakiwa wamefungwa mechi 11 kati ya 13 walizocheza, huku wakitoka sare mbili pekee.
Kuondolewa kwao kukawafanya Pamba waliokuwa salama nafasi ya nne kutoka chini waangukie nafasi ya tatu kutoka chini, na kushuka daraja. Kama siyo Kagera Stars kutotokea kwenye mechi tatu zilizowafanya waondolewe, Pamba wangebaki salama.
Mwaka 2002 Kagera Stars ikanunuliwa na kiwanda cha sukari cha Misenyi mkoani humo, na kuitwa Kagera Sugar ambayo ipo hadi sasa.
Mwaka 2006 Kagera Sugar ikarudi Ligi Kuu na kuiacha Pamba ikihangaika. Mwaka 2019, Pamba ikiwa katika harakati za kurejea Ligi Kuu ikaangukia kwenye play off na kupangwa kukutana na Kagera Sugar. Hii ilikuwa nafasi ya Pamba kulipa kisasi lakini ikashindwa.
Mechi ya kwanza jijini Mwanza ikaisha kwa sare ya 0-0 na mechi ya marudiano mjini Bukoba, Kagera Sugar ikashinda 2-0.
Kama tulivyoona huko juu, timu saba zilishuka daraja mwaka 2001. Pamba inakuwa timu ya nne katika zile saba kufanikiwa kurudi Ligi Kuu. Zingine tatu hazikurudi kabisa na zingine zimeshafutika kwenye ulimwengu wa soka.
Majimaji FC ya Songea – kundi B
Ndiyo timu ya kwanza kurudi Ligi Kuu katika wale. Walirudi Ligi Kuu 2003, wakashuka 2005, wakarudi tena 2009 na wakashuka tena 2011 na wakarudi tena 2016 na wakashuka tena 2018 na hawajarudi tena hadi leo.
Kagera Stars ya Kagera – kundi A
Walikuwa wa pili kurudi Ligi Kuu 2006. Hawajashuka tena hadi leo.
Lipuli FC ya Iringa – kundi A
Walirudi Ligi Kuu 2017 na kushuka tena 2020. Hawarudi tena baada ya hapo.
Pamba FC ya Mwanza – Kundi A
Timu ya mwisho katika wale saba wa 2001, kurudi ligi kuu.
Milambo SC ya Tabora – Kundi B
-Hawakufanikiwa tena kurudi na hawapo tena kwa sasa. Wakati wa uhai wao walifahamika kama Taifa Jipya.
Reli ya Morogoro – Kundi A
Wakati wa uhai wao walifahamika kama kiboko ya vigogo. Hawakuwahi kufanikiwa kurudi Ligi Kuu na hawapo tena katika ulimwengu wa soka.
-Hii ilikuwa timu ya Jeshi la Wananchi kutoka Kikosi cha Jeshi (KJ) namba 44 cha Mbalizi Mbeya.
Hawakufanikiwa kurudi Ligi Kuu na hawapo tena.
Pamba imerejea Ligi Kuu siku moja baada ya fainali ya Ligi ya Muungano 2024. Hii ni ligi ambayo Pamba walishinda ubingwa wake 1990. Kwa ubingwa huo Pamba wakapata nafasi ya kushiriki Klabu Bingwa Afrika 1991 na kufika robo fainali. Lakini wakati wanashinda ubingwa wa Muungano, pia walikuwa wakishiriki mashindano ya Kombe la Washindi Afrika.
Walipata tiketi hiyo baada ya kushika nafasi ya pili kwenye Ligi ya Muungano 1989. Kombe la Washindi yalikuwa mashindano yaliyoandaliwa na CAF kuanzia 1975.
Mashindano hayo ambayo baadaye yaliitwa Kombe la Mandela yalikuwa maalumu kwa ajili ya washindi wa Kombe la FA la kila nchi ambalo kwa Tanzania liliitwa Kombe la Nyerere. Lakini katika miaka ambayo Kombe la Nyerere halikufanyika, timu ya pili kwenye Ligi ya Muungano ndiyo ilishiriki. Kwa hiyo Pamba ikapata nafasi 1990 kushiriki Kombe la Washindi, kutokana na kuwa wa pili kwenye Ligi ya Muungano 1989.
Ni kwenye mashindano hayo ndiyo Pamba FC iliweka rekodi.
Ilishinda kwa matokeo ya jumla ya 17-1 dhidi ya Anse-Aux Pins ya Shelisheli. Walishinda 5-0 ugenini na 12 – 1 nyumbani. Ushindi huo wa jumla wa mabao 17-1 unabaki kuwa rekodi ya Afrika kwa ushindi mkubwa zaidi wa jumla. Haya hivyo, Kombe la Washindi lilifutwa na CAF 2003 kwa kuunganishwa na mashindano mengine yaliyoitwa Kombe la CAF na ndipo likazaliwa Kombe la Shirikisho ambalo nalo sasa linafutwa.