Samasoti baharini inayolipa vijana mkwanja wa maana

MAKACHU ni mchezo unaochezwa sana maeneo ya Forodhani, Zanzibar katika Bahari ya Hindi, kwa wachezaji kujirusha umbali mrefu kutoka nchi kavu hadi majini.

Lakini, nyuma ya mchezo huo kuna makanja wa maana tu ambao wanaingiza vijana wanaocheza makachu, kwani kwa wastani kila siku huingiza takriban Sh50,000 ambapo kwa mwezi ni zaidi ya Sh1.5 milioni.

Kwa usawa huo, ajira hiyo inayofanywa na vijana wachache visiwani humo inawawezesha kuishi kibosi, wakiwa na uhakika wa kukusanya pesa za maana tu.

Vijana wanaojihusisha na mchezo huo huingiza fedha hizo kwa kuzawadiwa na watalii pamoja na watu wengine wanaofika ufukweni kuangalia.

Zipo nchi nyingi unakochezwa mchezo wa kuogelea ikiwamo Tanzania Bara, lakini kwa Zanzibar ni tofauti kutokana na uchezaji wake ulivyogeuka na kuwa kivutio kwa watalii.

Wapo vijana ukiwaona kwa nje ni watu wa kawaida, lakini wamefanikiwa kupitia makachu na miongoni mwao ni Adil Omary Nassor anayeingiza mkwanja wa maana.

Wakiwa wamepata umaarufu ndani na nje ya nchi, kina Adil kwa namna wanavyojirusha kwenye maji huku nyakati nyingine wakiwa wameshika mabango yanayoonyesha ukarimu wa Watanzania kwa watanii, ni burudani tosha.

Mwanaspoti lilitaka kujua mchezo huo ulivyo na pia ulianzishwa lini, kanuni na changamoto zake na majibu ya Adil yalikuwa haya:

Adil anasema, “mchezo huu ulianza tangu enzi za wazee wetu kwani wao walikuwa wanacheza tu kwa kupenda na hakukuwa na mitandao ya kijamii kuonyesha wanachofanya na walikuwa wakicheza kama kujifurahisha hasa wakati wa jioni wanapomaliza shughuli.

“Lakini miaka miwili iliyopita tukaanza na tulikuwa tunaruka bila hata mabango wala kulipwa, ila baadaye tukaanza kuruka huku tukisema ‘welcome Zanzibar’ ili Wazungu na wageni wengine waweze kutuelewa kwa wepesi.

“Ndipo baadaye tukaona tunatazamwa na kuonekana katika mitandao ya kijamii kama mojawapo ya vijana wanaovutia watali Zanzibar ndio wazo la kugeuza starehe hiyo kuwa kipato lilivyoanza.”

Makuchu huchezwa jioni na siri pekee ni hii.

 “Sababu za mchezo huu kuchezwa kuanzia jioni ni moja tu huo ndio muda mzuri wa kupumzika. Watu wengi kuanzia saa 10 Jioni wanapenda kusogea maeneo ya ufukweni.

“Japo hata mchana tupo ila hakuna wingi wa watu ukilinganisha na muda wa jioni, ambapo hata watalii wameshatembea na huo ndio muda wao wa kuburudika na kula vyakula vinavyouzwa hapa Forodhani.”

Adil anaeleza kua sio wakati wote kuna wageni Zanzibar hasa wa mataifa tofauti, lakini huja kutokana na majira ya mwaka.

Anasema kipindi kizuri cha makuchu kuwaingizia fedha ni Juni, Septemba, Desemba na Februari wakati huo wageni huwa wengi.

“Pia tunafanya kwa kikundi na huwa tunagawana hivyo ikija taasisi au watalii, basi tunafanya nao kazi kwa kugawana pesa kwani huwezi kufanya kazi peke yako hata kama wewe ndio unayeruka,” anaasema Adil.

“Kipindi cha wageni wengi ndio tunagombaniwa sio watalii kwa sababu wao wana-kuwa wengi kuliko hata sisi kwani hatufikii hata 40 katika kikundi chetu na hatutaongeza mtu.”

Adil anasema aliwahi kupata majeraha wakati akicheza kama beki nne katika soka kwenye timu yake ya mtaani na kumfanya autose mchezo.

“Sikuachana na mpira kwa kutaka ila wakati naanza kuchipukia katika timu za mtaani nilivunjika mguu hali iliyonifanya nisitake kuendelea na safari ya soka kwani nilikaa ndani muda mrefu nikijiuguza.

“Changamoto nyingine ya mpira wa miguu ni upatikanaji wa ajira mpaka mtu kama mimi nije kutoka na kufanikiwa sio rahisi kama wengi wanavyodhani, kwani kwa upande wetu sio mchezo unaoonekana kama kazi itakayokutoa. Kidogo sasa hivi kuna mabadiliko,” anasema.

“Upande wa kazi nilikuwa nimeajiriwa ‘airpot’ lakini sikuendelea kutokana na kazi hii ambayo kwangu inanipa furaha na muda wa kupumzika.”

Adil anasema moja kati ya changamoto ambayo awali walikuwa wakikutana nayo ni ile ya watu kupoteza maisha au kupata majeraha makubwa.

“Wapo wenzetu ambao walipoteza maisha na mara nyingi wanaokumbana na changamoto hizo ni wale ambao hawana uzoefu.

“Wazoefu tunapata majeraha. Wapo waliowahi kuvunjika uti wa mgongo au hata kujigonga kwani unaporuka chini huwa kuna mawe. Kwa hiyo unaweza ukafikia jiwe au wenzako wakakurukia ukiwa ndani ya maji,” anasema.

“Hakuna kesi yoyote ikitokea umepoteza maisha ila kama ltatokea tukio kama hilo, basi huwa panafungwa kwa muda halafu watu wanaendelea kucheza inapofika muda wa jioni.”

Adil anasema kuna faida kubwa ambazo amezipata kutokana na kipato. “Uzoefu nilionao sasa ni mkubwa hivyo hata wageni wakija sina shida, naongea lugha nne tofauti na Kiingereza na zote nimejifunza hapa, hivyo wanafurahia kufanya kazi na mimi kwani tunaelewana,” anasema.

“Nimeshawahi kufanya kazi zaidi ya moja za wageni wanaokuja hapa kufanya matangazo na wakanilipa zaidi ya milioni, hivyo kwa mwezi ni ndogo kipindi cha wageni napata zaidi ya hapo, lakini msimu ambao sio wa wageni napata milioni moja na laki tano.

“Pia tunalipwa kwa dola ndio maana tunapata pesa nyingi zaidi kwani wageni hawafanyi malipo kwa fedha zetu, jambo ambalo linatunufaisha zaidi.”

Kama ilivyo katika michezo mingine huwa na kanuni, lakini makuchu ni tofauti kwani mchezaji huyo anasema tangu alipoanza hajawahi kusikia.

“Huu mchezo hauna kanuni ila anatakiwa acheze mtu mwenye uzoefu mkubwa ili asipate matatizo, lakini uwe miongoni mwa wanakikundi

Adil anaeleza namna vijana wanavyonufaika na mchezo huo ambao umekuwa kivutio kikubwa kwa watu wengi wanaokwenda Zanzibar kwa ajili ya utalii.

“Nimekutana na watu wengi wakubwa kuliko hata nilivyodhani kwani nimefanya kazi na watu wa nje, mabalozi wa nchi mbalimbali na marais pia kwani video wanazoondoka nazo zimekuwa kumbukumbu ya kila anayekuja kutaka kutufahamu na kuja kukaribishwa nasi,” anasema.

Anasema pia vijana wengi wanaocheza makuchu wamejikuta wakiwa na mahusiano na wageni hasa Wazungu na miongoni mwao wapo waliowahi kuchukuliwa na kwenda ughaibuni.

Related Posts