Sengerema. Wakati baadhi ya vijana nchini wakilia ukosefu wa ajira baada ya kuhitimu masomo katika vyuo vya kati na vyuo vikuu, kwa Anordy Theonest (25), hali ni tofauti.
Alihitimu stashahada ya ualimu mwaka 2018 katika Chuo cha Ualimu Vikindi kilichopo Mkuranga mkoani Pwani, lakini muda mfupi baada ya kuhitimu akageukia ushonaji viatu kukabiliana na ukosefu wa ajira.
Theonest alihitimu chuo wakati wa utawala wa Serikali ya awamu ya tano iliyopunguza kiwango cha kuajiri watumishi wa umma ikiwamo kwenye kada ya walimu huku wengine wakiondolewa kwa kuwa na vyeti feki au elimu ya darasa la saba.
Utafiti wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi wa mwaka 2020/21 uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (OCGS) kwa kushirikiana na wadau wengine, unaonyesha kiwango cha ukosefu wa ajira kwa vijana wenye miaka 15 hadi 35 kimeongezeka kutoka asilimia 12.1 mwaka 2014 kufikia asilimia 12.6 mwaka 2020/21.
Kijana huyo ana familia ya mke na mtoto mmoja, ni mzaliwa wa Wilaya ya Muleba mkoani Kagera ambaye alisoma Shule ya Msingi Magata na kuhitimu mwaka 2011, kisha kujiunga na sekondari ya Kishoju na kuhitimu mwaka 2015.
Theonest suala la kuajiriwa kwake siyo kipaumbele, hivyo hajahangaika kutafuta kazi serikalini, badala yake aliamua kujiajiri kwa kuanza kushona viatu ili kujipatia kipato cha kukidhi mahitaji yake na familia yake.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Aprili 30, 2024, Theonest amesema katika harakati za kusaka maisha huku, akisubiri ajira ya ualimu serikalini na sekta binafsi, mwaka 2019 alikwenda Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza kisha kuanza shughuli ya kushona viatu, kung’arisha na kutengeneza zipu za mabegi yaliyoharibika.
Katika kijiwe chake alichokiita “Kwa Ticha Shoe Shine” kilichopakana na maduka makubwa ya mahitaji mbalimbali pembezoni mwa barabara inayoelekea stendi ya mabasi ya zamani wilayani humo, Theonest pia anauza vitu vidogo vidogo ikiwamo leso na soksi.
Amesema kutokana na changamoto za ajira serikalini aliamua kuanzia biashara hiyo ili impatie kipato akiamini kushona viatu na kung’arisha ni hitaji ambalo kwa baadhi ya watu ni la lazima.
Theonest amesema katika kazi yake hiyo alianza na mtaji wa Sh1,500 ambayo alinunua uzi Sh1,000 na sindano ya kushonea viatu Sh500.
Anavyonufaika na kazi hiyo
Kazi anayofanya, amesema inamwingizia fedha si chini ya Sh20,000 kwa siku na gharama za kushona kiatu na kunga’arisha jozi moja ya viatu inaanzia Sh500 hadi Sh2,000 kutokana na marekebisho anayoyafanya.
“Familia yetu ya baba na mama haijutii mimi kuwa fundi viatu licha ya kunisomesha chuo cha ualimu, hii ni kutokana na wao wanaona changamoto ya ajira, kupitia kazi yangu wanapata manufaa ya kuwasaidia maisha huko kijiji magata wilayani Muleba,” amesema Theonest.
Ameongeza kutokana na faida anayoipata kwenye kazi yake hiyo hana mpango wa kuomba kazi serikalini hata nafasi zikitangazwa kwa kuwa kazi hiyo inamtimizia mahitaji yake, familia na wazazi wake.
Amesema changamoto anayokutana nayo kwenye kazi yake ni baadhi ya wateja wake kuchelewa kufuata viatu vyao akidai hata hivyo anaichukulia kama fursa kwa kuwa muaminifu na kutumia lugha nzuri kuwafanya warudi hata siku nyingine.
“Katika maisha unatakiwa kuchukua changamoto kama fursa ya mafanikio, usikate taama na kubagua kazi, kazi yoyote unapoifanya kwa malengo inakuletea manufaa,”amesema Theonest.
Amesema malengo yake ni kuwa mfanyabiashara mkubwa wa viatu hapo baadaye, baada ya kuona kazi yake inamlipa akitumia kauli mbiu ya ‘kambi ni popote na mfungwa hachagui gereza.’
Theonest ametoa ushauri kwa wasomi wenzake kujipambanua kutafuta maarifa nje ya mfumo wa ajira serikalini kwa kutafuta kazi za kufanya ikiwamo biashara na kilimo hata kwa mtaji mdogo ili waendeshe maisha yao.
“Dhana ya kutembea na vyeti kwenye makorido ya ofisi mbalimbali wanachelewa na kupoteza muda, wangeutumia muda huo, elimu yao kwa kujiajiri wenyewe mahali walipo,” amesema.
Joseph Igobeko, mkazi wa Sengerema amesema elimu ni kupata uelewa na ufahamu juu mambo mbalimbali katika jamii na kumsaidia mtu kuendesha maisha yake na ya watu wanaomzunguka.
Amesema suala la ajira linategemea malengo ya mtu, akidai kama ajira azieleweki ni vizuri kutafuta shughuli zingine hata za ujasiriamali kujiingizia kipato.
“Hivyo, wasomi ambao hawajapata ajira wajikite kufanya kazi za kujiajri kwenye kazi zingine mfano kilimo, ufugaji, biashara ndogodogo hii itawaletea manufaa katika maisha yao kuliko kusubiri ajira serikalini ambayo kwa sasa imekuwa changamoto kubwa kwa vijana wasomi hapa nchini,” amesema.
Mama lishe anayeuza vyakula wilayani humo, Amina Amos amesema wasomi wengi wanaogopa kujishughulisha na ujasiriamali mdogo mdogo kisa watachekwa jambo aliloliita ni kutojiongeza na kuishi maisha yasiyo yao (halisi); akidai mwisho wa siku wanaishia kusumbua wazazi na walezi wao hata kwa mahitaji madogo madogo.
“Tunawashauri kufanya biashara wasiogope kuwa watachekwa, hakuna mtu anayefanikiwa bila kupitia changamoto mbalimbali na manufaa yeyote yanapitia changamoto,” amesema Amina.