Unguja. Zaidi ya watu 5,000 wanakadiriwa kukabiliwa na tatizo la afya ya akili Zanzibar.
Hata hivyo, kutokana na udhaifu wa usajili wa wagonjwa, idadi inaelezwa yaweza kuwa mara mbili zaidi.
Hayo yamebainika leo Aprili 30, 2024 katika mkutano wa wauguzi na waandishi wa habari kuhusu kazi zitakazofanyika kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wakunga Mei 5, na siku ya wauguzi Mei 12, 2024 visiwani hapa.
Mratibu wa Afya ya Akili kutoka Wizara ya Afya Zanzibar, Suleiman Abdu Ali amesema tatizo la afya ya akili linaonekana kuongezeka kila siku licha ya kutokuwa na takwimu sahihi kutokana na kutokuwa na mfumo mzuri wa usajili wa wagonjwa.
“Tunasema tatizo linaongezeka kwa sababu vituo vyetu vya huduma vinaendelea kupokea wagonjwa wapya kila siku, mfano hospitali ya Kidongo Chekundu inapokea wastani wa wagonjwa wapya kati ya 100 hadi 150 kwa mwezi, zaidi wakiwa ni vijana na watoto,” amesema.
Kwa upande wa Pemba kwa mwaka 2021 amesema waliona wagonjwa wapya 132 kwa mwezi, lakini mwaka 2023 waliona wagonjwa 1,039 wapya kutoka hospitali za Wete, Mkoani, Chake Chake, Vitongoji na Micheweni kisiwani Pemba.
Amesema takwimu hizo hazikuangalia hospitali na vituo vingine vya afya na hospitali za Kivunge na Makunduchi.
Mratibu huyo amesema kazi hiyo kwa kiasi kikubwa inafanywa na wauguzi kwani mpaka sasa hakuna daktari bingwa wa magonjwa ya akili kisiwani Pemba.
Amesema Wizara ya Afya kupitia Shirika la Kuimarisha Huduma za Afya Zanzibar (HIPZ) tangu miaka ya 2017 imefanya juhudi ya kuongeza uelewa wa afya ya akili Zanzibar na kupunguza unyanyapaa kwa kuwapatia wafanyakazi 55 utaalamu maalumu wa utoaji elimu ya afya ya akili.
Wataalamu hao wapo kwenye wilaya zote za Unguja na Pemba.
Amesema katika kukabiliana na tatizo hilo, zipo jitihada zinafanyika ikiwa ni pamoja na kuwapatia wahudumu wa afya 310 mafunzo maalumu ya tiba ya kisaikolojia kwa watu wanaosumbuliwa na wasiwasi na sonona au msongo wa mawazo.
Mwaka 2023 jumla ya watu 883 walipatiwa huduma mbalimbali Unguja na mwaka huu 2024 zaidi wa watu 608 tayari wameshapatiwa huduma Pemba na huduma bado inaendelea.
Amesema katika huduma hizo, wauguzi hukumbana na changamoto kadhaa kama vile ufinyu wa elimu ya utambuzi, wauguzi wakiwa ndio jeshi la msatri wa mbele kwenye afya, bado wanakosa kipaumbele cha kutosha kwenye elimu.
Amesema huwa wanapokea lawama tu pale wanapokosea kutokana na sababu za kibinadamu kama vile uchovu uliotokana na kufanya kazi kwa saa 24.
Kwa upande wa afya ya uzazi, Ofisa uzazi salama kitengo shirikishi cha afya ya uzazi na mtoto, Safia Haidhuru Ramadhan, amesema kwa takwimu za mwaka 2022 vilitokea vifo vya uzazi 52 ikilinganishwa na vifo 70 vilivyotokea mwaka 2021.
Kwa upande wa vifo vya watoto vilivyotokana na changamoto za uzazi kwa mwaka 2022 vilitokea 1,727 kiwango ambacho kinaonekana kuwa bado kipo juu.
Ametaja baadhi ya changamoto za vifo hivyo ni mama kupoteza damu nyingi, kuchelewa kufika katika vituo vya afya, na lishe duni ya wajawazito.
Amesema asilimia kubwa ya wajawazito wanakuwa na damu pungufu kutokana na mlolongo mzima wa masuala ya uzazi.
Mkunga Bingwa Wizara ya Afya, Margaret Sylivester Tayari, amesema changamoto nyigine inatokana na uwiano wa wauguzi na wanawake wanaotakiwa kuhudumiwa.
“Kwa kawaida muuguzi mmoja anatakiwa ahudumie mgonjwa mmoja, na mama akiwa kwenye uchungu anatakiwa apimwe kila baada ya nusu saa lakini kama unakuta chumba kimoja kina vitanda zaidi ya vitano na kila kitanda kina wajawazito wawili hadi watatu muuguzi hawezi kuwaangalia kwa ufanisi,” amesema Margaret.
Mwenyekiti wa Baraza la Wauguzi na Ukunga, Sharifa Awadh Salmin amesema katika kipindi hiki cha wiki mbili watajitahidi kuifikia jamii kubwa zaidi kutoa elimu na kufanya shughuli za matibabu.
“Itatolewa elimu ya lishe, afya ya uzazi na afya ya akili kwa vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 25, uchangiaji damu na uzinduzi wa jumuiya ya wakunga kabla ya kufikia kilele Mei 12, 2024,” amesema.