Shirika la habari la AFP limeripoti kuwa vituo vya kura vilifungwa mwendo wa saa kumi na mbili jioni na baada ya hapo kura zikaanza kuhesabiwa. Taarifa ya tume ya uchaguzi nchini humo ilikuwa imesema kwamba huenda matokeo ya awali yangelianza kutolewa jana jioni.
Makamu wakuu wa mikoa 179 wachaguliwa
Zoezi hilo ni la kuwachagua wabunge 113 na pia kwa mara ya kwanza, makamu wakuu wa mikoa 179 katika wilaya tano ambao pamoja na madiwani watachagua baraza jipya lililoundwa la seneti.
Kulingana na chama tawala chaGnassingbe, UNIR, hatua hiyo inaifanya Togo kuwa na uwakilishi zaidi lakini vyama vya upinzani viliwahamasisha wafuasi kupiga kura dhidi ya kile walichokitaja kuwa mapinduzi ya kitaasisi.
Soma pia:Kampeni zamalizika Togo kabla ya uchaguzi muhimu wa Jumatatu
Baada ya kupiga kura hapo jana, Jean- Pierre Fabre, kiongozi wa chama kikuu cha upinzani, National Alliance for Change, alisema walikuwa na kampeini nzuri ya uchaguzi na kwamba wanalaani kasoro za uongozi uliopo madarakani huku akiongeza kuwa raia wa Togo watafanya maamuzi bora.
Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi ECOWAS, ilikuwa imesema kuwa itatuma timu ya waangalizi nchini Togo kufuatilia zoezi hilo la uchaguzi.
Wakati wa kupiga kura, tume ya uchaguzi nchini humo, ilikataa kuruhusu Baraza la Maaskofu wa nchi hiyo kupeleka waangalizi wa uchaguzi kote nchini humo.
Soma pia:Togo: Wabunge sasa kumchagua Rais katika katiba mpya
Kwa upande wake, shirika la kutetea haki la Amnesty International limetoa wito kwa serikali ya nchi hiyo kukomesha ukandamizaji unaoongezeka.
Upinzani Togo haufurahii haki ya kujieleza
Mkurugenzi wa shirika hilo kwa Afrika Magharibi na Kati Samira Daoud, amesema nchini Togo,sauti za upinzani hazifurahii haki yao ya kujieleza na mikutano ya amani. Daoud ameongeza kuwa imekuwa vigumu kuchangia kwa njia huru kwenye mjadala kuhusu katiba mpya kutokana na uoga wa hatua za kisasi.
Wabunge waliidhinisha nafasi inayofanana na ya waziri mkuu
Kura hiyo imefanyika baada ya wabunge mwezi huu kupiga kura kuidhinisha kuwepo kwa nafasi inayofanana na ya waziri mkuu ambayo kulingana na wapinzani, iliundwa ili kumsaidia Rais Gnassingbe kuepukana na ukomo wa kukaa madarakani.
Tayari Gnassingbe, mwenye umri wa miaka 57, ameshashinda katika chaguzi nne ambazo zote zilipingwa na vyama vya upinzani kutokana na kile walichokiita kuwa ni dosari. Kulingana na katiba ya awali, Gnassingbe angeweza kugombea urais mwaka 2025 pekee katika muhula mmoja uliosalia.