Wasichana wapewa mbinu kumudu masomo ya sayansi

Unguja. Wakati masomo ya sayansi yakitajwa kuwa magumu hususani kwa wanafunzi wa kike, imeelezwa ni rahisi zaidi kwa sababu yanahitaji kujua tu kanuni na si kukariri.

Kutokana na hilo, wasichana wametiwa moyo kupenda masomo ya sayansi.

Hayo yamebainika wakati wa kufunga mafunzo na mashindano ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kwa wasichana yaliyoandaliwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech).

Mashindano hayo yaliyoanza katika kanda tano za mikoa yote ya Tanzania, yalishirikisha wasichana 244 lakini walichaguliwa 31 ambao walikutana Unguja katika mashindano ya mwisho.

Kikubwa kinachoangaliwa ni kubuni na kutengeneza mifumo inayotatua changamoto za jamii.

Akifunga mafunzo leo Aprili 30, 2024 Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Zanzibar, Dk Khalid Salum Mohamed amesema uzuri wa masomo ya sayansi yanatumia kanuni na hazibadiliki.

“Kilichopo ni hofu tu ya kuingia katika masomo ya sayansi lakini mimi ninachoamini hakuna kitu rahisi kama sayansi, ukishazielewa kanuni zake hazibadiliki, ndiyo hizohizo sasa wewe hakikisha unazijua zikishakaa kichwani wala huna sababu ya kusoma sana,” amesema.

“Ukishajua kanuni ni rahisi kufanya hesabu yoyote unayoletewa, huna sababu ya kukesha ukisoma namba na muda wa kusoma unakuwa mdogo, kwa hiyo wanawake nataka niwatie moyo msiogope kusoma sayansi,” amesema Dk Khalid ambaye kitaaluma amesoma Shahada ya Uzamivu (PhD) ya Uchumi wa Kilimo.

Amewataka wahusika kuhakikisha kunakuwa na kanzi data ya wasichana wanaoshiriki mafunzo hayo na kuwafuatilia walipo kwa sababu ni rahisi mtu anakuwa na ubunifu mzuri lakini akifikia mahali akishapewa mafunzo anatelekezwa na ubunifu huo unapotea.

Ameshauri kuwe na kiunganishi  cha kuwaunganisha na soko la ajira, iwe ni sekta binafsi au serikalini.

Amesema katika utaratibu wa uwezeshwaji nao wafikiriwe jambo litakalowasaidia kujiajiri au kuajiri wenzao.

“Tunaweza kuwa tunasomesha vijana wengi lakini mwishowe kama hatujui walipo, hatujui wanachokifanya na vijana hawa wanapotea, wanashughulika na mambo mengine ile taaluma na uwezo wa ubunifu unapotea. Hili naomba tushirikiane, vijana hawa wawezeshwe,” amesema.

Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasilino kwa Wote (UCSAF), Justina Mashiba amesema sababu ya kuanzisha programu hiyo ni kwamba, wameona watoto wengi wa kike wanakimbia masomo ya sayansi, hivyo kupitia mpango huo utawahamasisha na kuwajengea ujasiri wa kushiriki masomo hayo.

“Tunataka tuwafanye watoto wa kike waende kwenye Tehama na ndiyo sababu kubwa ya kuanzisha mafunzo ya aina hii,” amesema.

Kwa mujibu wa Mashiba, wana jumla ya watoto 954 ambao tayari wameshapewa mafunzo hayo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Costech, Dk Amos Nungu amesema wana miradi ya Sh1 bilioni inayoendelea, kati ya hiyo, miradi ya Sh700 milioni ni ya utafiti na mingine ya Sh300 milioni ni ya ubunifu.

Amesema lengo ni kuhamasisha watoto wa kike kwenye masomo ya STEM yaani sayansi, teknolojia, uhandisi na hesabu, kutambua kuwa si magumu kama wanavyofikiria.

Christina Massawe kutoka Mkoa wa Pwani aliyeshiriki mashindano hayo amesema wamebuni mfumo wa kuweka mji safi (Autosmart Dustibin) baada ya kuona kuna changamoto ya uchafuzi wa mazingira, hivyo kupitia mfumo huo unaweza kusaidia kutunza usafi wa miji.

Olga Mmole kutoka mkoani Ruvuma, amesema wamebuni mfumo wa ‘Smart City’ ambao unasaidia kupunguza ajali, kwani dereva hawezi kupita eneo ambalo hajaruhusiwa.

Wanafunzi wote 31 walipewa zawadi za kompyuta mpakato.

Related Posts