Blinken amelitaka pia kundi la Hamas kukubali pendekezo la usitishwaji mapigano lililowasilishwa hivi karibuni na Israel.
Blinken amekutana kwa mazungumzo na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na kumsisitizia kuhusu suala zima la kuruhusu kuingizwa misaada zaidi ya kibinaadamu katika ukanda wa Gaza, lakini akamdhihirishia pia msimamo wa Marekani wa kupinga operesheni ya kijeshi ya Israel katika mji wa Rafah, wanakoishi Wapalestina zaidi ya milioni moja waliokimbia mapigano katika sehemu zingine.
Soma pia: Netanyahu aapa kuushambulia mji wa Rafah
Hapo jana, Netanyahu aliapa kuushambulia mji huo wa Rafah bila kujali iwapo kutafikiwa au la makubaliano hayo ya usitishwaji mapigano na kusisitiza kuwa ni lazima alitokomeze kabisa kundi la Hamas ambalo limeorodheshwa na Umoja wa Ulaya, Marekani, Ujerumani na mataifa kadhaa ya Magharibi kama kundi la kigaidi.
Katika ziara yake ya saba huko Mashariki ya Kati tangu kuanza kwa mzozo huo Oktoba 7, Blinken amekutana na Netanyahu kwa muda wa saa mbili na nusu mjini Jerusalem, katika juhudi zake za kupiga jeki makubaliano ya usitishwaji mapigano kwa siku 40 kati ya Israel na kundi la Hamas ambayo pia yatahusisha kuachiliwa kwa mateka na wafungwa wa Kipalestina.
Msimamo wa Hamas na juhudi za kidiplomasia
Afisa mwandamizi wa Hamas amesema kundi hilo litatoa jibu kuhusu pendekezo hilo “ndani ya muda mchache”, lakini akasisitiza kuwa usitishaji wowote wa mapigano unatakiwa kuwa wa kudumu. Suala linalopingwa vikali na Israel na ambalo limekuwa kiini cha mvutano kati ya pande hizo mbili.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Stephane Séjourné amewasili mjini Cairo na kukutana na mwenzake wa Misri Sameh Shoukri. Séjourné amesema wanalenga kushirikiana na nchi za kiarabu ili kufanikisha makubaliano kati ya Israel na Hamas huko Gaza lakini akasisitiza kuwa bado kuna kazi ya ziada inayotakiwa kuendelea kufanyika.
Kwa upande wake, Kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei amesema hivi leo kuwa juhudi zinazoendelea za kuyataka mataifa ya kiarabu kurekebisha mahusiano yao na Israel, kamwe haziwezi kutatua mgogoro unaoendelea huko Mashariki ya Kati.
Vuguvugu la kuwaunga mkono Wapalestina
Maandamano ya kuwaunga mkono Wapalestina yameshuhudiwa kwenye vyuo vikuu katika nchi za Marekani, Ufaransa na Lebanon. Wapalestina pia katika Ukanda wa Gaza wametaja kufurahishwa na hatua ya wanafunzi hao kuwaunga mkono kama anavyoeleza Awni Khattab:
” Hii ni shinikizo la wananchi kwa serikali, na serikali lazima zizingatie matakwa ya watu wao na kutambua haki ya watu wa Palestina. Sisi ni watu kama wengine. Hakuna nchi inayokaliwa kwa mabavu isipokuwa Palestina. Katika kila pembe ya dunia, sisi ndio nchi pekee inayokaliwa kwa mabavu, tunatumai kuwa dhuluma dhidi ya watu wa Palestina na taifa la Palestina itakomeshwa.”
Maandamano hayo ambayo awali yalikuwa ya amani sasa yameanza kugeuka kuwa ya vurugu hasa huko Marekani ambapo Polisi ililazimika kuwatawanya waandamanaji na kuwakamata wengine karibu 300 katika chuo kikuu cha Columbia mjini New York na chuo chengine jimboni California.
(Vyanzo: Mashirika)