Dar es Salaam. Chadema imemaliza ngwe ya pili ya maandamano mikoani wakiibua mambo manne, likiwamo suala la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ugumu wa maisha, Tume ya Uchaguzi na Katiba mpya.
Maandamano ya sasa ni matokeo ya Azimio la Mtwara lililofikiwa katika mkutano wa Kamati Kuu ya Chadema iliyoketi Machi, 2024 mkoani Mtwara na kuazimia yafanyike mikoa yote nchini kuanzia Aprili 22 hadi Aprili 30, 2024.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliyetembea zaidi ya kilomita 117, alianza kuongoza maandamano Bukoba mkoani Kagera Aprili 22, kisha akaenda Kahama, Geita na Bariadi, mkoani Shinyanga.
Alienda Musoma (Mara), Sengerema (Mwanza) na baadaye Tanga na kuhitimisha Moshi mkoani Kilimanjaro.
Makamu Mwenyekiti-Bara wa chama hicho, Tundu Lissu alitembea jumla ya kilomita 50 akianzia Babati mkoani Manyara Aprili 26, kisha mjini Singida, Dodoma akamalizia Morogoro.
Akiwa wilayani Babati, Lissu aliibua hoja ya Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar, akisema japo umetimiza miaka 60, umejaa dosari.
Alihoji sababu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano kutoka upande wa Zanzibar na kutoa amri zinazoathiri upande wa Tanganyika, wakati Zanzibar kuna Rais wake na Watanganyika hawana haki wanazopata Wazanzibari.
‘‘Anaweza kutoka alikotoka akaja akawavuruga watu huku. Kusingekuwa na huo Muungano asingefanya hivyo, kwa sababu asingekuwa Rais wetu,” alisema Lissu. Alirudia kauli hiyo akiwa mkoani Singida, Dodoma na Morogoro.
Hata hivyo, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye akiwa bungeni Aprili 29,2024 alimjibu Lissu akimtaka aache ubaguzi kwa kauli hiyo.
“Leo anatokea tu mwanasiasa kwa kutaka tu madaraka, yuko tayari kuligawa Taifa letu na anasema kwa kusisitiza, huyu ni Mzanzibari, huyu ni Mtanganyika, tukiruhusu haya tunataka kuligawa Taifa letu,” alisema Nape.
Licha ya kujibiwa, suala la Muungano pia lilijadiliwa na Mbowe alipohutubia mkutano wa hadhara mjini Musoma, akisisitiza msimamo wa chama hicho wa kuwa na Muungano wa Serikali tatu.
“Naomba watuelewe vizuri, sisi si kwamba hatuutaki Muungano, tunataka na tunaupenda, ila tunachotaka ni utaifa wetu utambuliwe kama ilivyo kwa wenzetu, kwa sababu wao licha ya kuwa ni wachache, lakini wana Serikali yao. Wana Bunge lao na wana Rais wao, sisi vya kwetu viko wapi?” alihoji Mbowe.
Katika mikutano yao, Mbowe na Lissu walisisitiza mabadiliko ya Katiba ili kupunguza madaraka ya Rais.
Akihutubia mkutano wa hadhara Bukoba mkoani Kagera Aprili 22, 2024, Mbowe alieleza kukerwa na kauli ya baadhi ya viongozi wa Serikali na chama kilichopo madarakani kuwa kila fedha zinazotolewa kwa ajili ya maendeleo nchini, ni za Rais Samia Suluhu Hassan.
Lissu akiwa mkoani Morogoro alisema: “Katiba ikitoa utaratibu unaowapa hawa wenye madaraka mamlaka ya kufanya wanavyopenda, matokeo yake ni kwamba walioingia madarakani wakiwa wema, wakajikuta kwamba wanaweza kuitajirisha bila kuhojiwa na mtu watajitajirisha.”
Ugumu wa maisha / Katiba mpya
Akiwa mkoani Dodoma, Lissu alisema kuna uhusiano wa Katiba mbovu na ugumu wa maisha unaowakabili wananchi.
Alisema Katiba imempa Rais madaraka makubwa yakiwamo ya kutoza kodi, kupanga kikokotoo vinavyolalamikiwa na wananchi na hatimaye kuwafukarisha.