CRDB yaamriwa kumlipa fidia Sh300 milioni Balozi wa Tacaids

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeiamuru Benki ya CRDB kumlipa fidia ya Sh300 milioni, Balozi wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids), Zawadi Bahenge kwa kutumia picha yenye  sura yake kwenye matangazo ya kibiashara bila ridhaa yake.

Pia mahakama imeiamuru benki hiyo kuondoa picha zote za balozi huyo wa Tacaids kwenye mabango yake ya kibiashara yaliyosambazwa nchi nzima.

Mahakama imefikia uamuzi huo katika hukumu iliyotolewa jana Aprili 30, 2024 na Hakimu Mkazi Mkuu, Rahim Mushi, katika kesi ya madai aliyofunga Bahenge dhidi ya benki hiyo akiilalamikia kwa kutumia picha yake kwenye matangazo ya kibiashara katika kampeni ya ‘Tupo kuijenga biashara yako’ bila ridhaa yake.

Katika hukumu pamoja na amri ya malipo ya fidia, gharama za kesi na kuondoa picha za Bahenge kwenye mabango yake nchini kote, pia mahakama imeiamuru CRDB kutotumia picha zake wakati wowote bila ya kuingia mkataba naye.

“Ifahamike kutumia picha ya mlalamikaji kwenye matangazo ya kibiashara umeingilia faragha yake bila ya ridhaa yake,” amesema Hakimu Mushi katika hukumu hiyo na kuamuru:

“Hivyo mahakama hii inakuamuru (benki ya CRDB) kumlipa mlalamikaji Zawadi Bahenge fidia ya Sh300 milioni na picha za mlalamikaji ziondolewe mara moja kwenye mabango ya kibiashara yaliyosambazwa nchi nzima.”

Akizungumzia hukumu hiyo, wakili wa Bahenge, Ferdinand Makole kutoka kampuni ya uwakili ya Case & Law Attorneys, amesema mteja wake alifungua kesi baada ya kubaini CRDB inatumia picha yake bila ridhaa yake.

Amesema benki hiyo ilikuwa inatumia picha za mteja wake kwenye matangazo ya kibiashara katika kampeni ya ‘Tupo kuijenga biashara yako’ yaliyosambazwa nchini nzima bila ya kuingia naye mkataba wa makubaliano.

Wakili Makole amedai mteja wake aliingia mkabata na benki wa kutumia picha za mteja wake kwenye kampeni ya ‘Ulipo Tupo’ kuanzia mwaka 2019 hadi mwaka 2021.

Amedai baada ya mkataba kuisha benki ya CRDB hawakuziondoa picha za mteja wake kwenye matangazo ya kibiashara yaliyosambazwa nchi nzima.

Badala yake waliendelea kuzitumia picha hizo kwenye kampeni mpya ya ‘Tupo kuijenga biashara yako’ kuanzia mwaka 2021 hadi sasa.

Amesema mteja wake alipoona picha zake zikiendelea kutumika aliifuata benki hiyo ili wafanye mazungumzo kwa namna watakavyoweza kuendelea kuzitumia kwa kuingia mkataba mpya, lakini viongozi wa benki hiyo walikataa.

Kutokana na hilo, Februari 6, 2023 aliamua kufungua kesi ya madai dhidi ya benki hiyo, akiiomba mahakama iiamuru imlipe fidia ya madhara ya jumla na itoe amri ya kuondoa picha zake kwenye mabango ya kibiashara kote nchini na kutotumia popote bila kushirikishwa.

Hukumu hiyo ni miongoni mwa ambazo zimetolewa na mahakama tofauti nchini katika siku za hivi karibuni zikiamuru kampuni kadhaa kuwalipa fidia watu mbalimbali kwa makosa ya matumizi ya picha za sura zao, kwenye matangazo ya kibiashara bila ridhaa yao.

Desemba 16, 2022 Mahakama ya Wilaya ya Arusha iliiamuru Kampuni ya Multichoice kuwalipa fidia ya jumla ya Sh450 milioni wanariadha watatu wa kimataifa wa Tanzania, Alphonce Simbu, Failun  Matanga na Gabriel Geay, kwa kutumia picha za sura zao katika matangazo ya kibiashara bila ridhaa yao.

Agosti 10, 2022 Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni iliamuru Kampuni ya udalali ya Dexter Insurance kumlipa dereva wa Kampuni ya New Force, Waubani Linyama maarufu ‘Ndugu abiria’, fidia ya Sh150 milioni kwa kosa la kutumia picha yake kibiashara bila idhini yake.

Aprili 28, 2023 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliamuru Kampuni Twiga Cement iwalipe watu watano, Christopher Chambo, Eliudi Chambo, Fred Roman, Naki Lobora na Yusuf Magaya, fidia ya Sh50 milioni kwa kitendo cha kuwapiga picha bila ridhaa yao na kuzitumia katika matangazo ya biashara.

Related Posts