Gamondi adai Pacome bado, mwenyewe afunguka

KOCHA wa Yanga, Miguel Gamondi amemtazama nyota wake Pacome Zouzoua kwa dakika 20 alizompa katika mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Tabora United na kusema bado anahitaji muda wa kurejea katika makali yake.

Pacome alianza kuomba kutumika tangu mchezo wa watani wa jadi Aprili 20, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkapa lakini kocha huyo hakutaka kuharakisha urejeo wake hata katika michezo mingine miwili iliyofuata dhidi ya JKT Tanzania na Coastal Union kwa kile alichoona bado hakuwa fiti tangu alipopata majeraha ya goti Machi 17.

Gamondi ambaye alimpa nafasi Pacome katika dakika ya 70 kwa kumtoa Stephane Aziz KI aliyefunga bao la kwanza kwa Yanga, amesema bado nyota huyo hayupo fiti.

 “Anahitaji muda wa kuwa sawa kwa sababu ametoka kuuguza majeraha na taratibu anaweza kurejea kwenye kiwango chake,” amesema kocha huyo ambaye timu yake imetinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) baada ya kuifunga Tabora United mabao 3-0, Azam Complex, Dar es Salaam.

Pacome alionekana kuwa na matumaini ya kupata nafasi katika mchezo huo tangu wakati ambao walikuwa wakipasha misuli joto na wenzake kabla ya mchezo kuanza.

Yote hiyo ilitokana na jina lake kuwa miongoni mwa wachezaji ambao walikuwa katika mpango wa kutumika katika mchezo huo baada ya kukosa michezo saba iliyopita sawa na dakika 630 katika mashindano yote.

Akiwa na bandeji ya bluu katika mguu wake ambao aliumia goti Machi 17, fundi huyo alionekana kuwa na furaha usoni wakati akifanya mazoezi mepesi kabla ya kuingia na kugusa mpira mara 12.

Pacome hakuonekana kukaa sana na mpira mguuni, alionekana kuuachia kwa haraka huku wenzake wakionekana kuwa msaada karibu yake. Bao la tatu la Yanga lilifungwa na Joseph Guede wakati Muivory Coast huyo akiwa uwanjani.

Baada ya mchezo huo kumalizika, Pacome amesema ni furaha kwake kurejea uwanjani baada ya kuwa nje kwa zaidi ya wiki sita.

“Naamini nitaendelea kupewa nafasi taratibu, ninafuraha sana kucheza kwa mara ya kwanza huku nikiwa sehemu ya wachezaji ambao wameipambania timu kuvuka hatua ya robo fainali,” amesema.

Baada ya kuitandika Tabora United mabao 3-0  katika mchezo wa robo fainali Fainali ya michuano hiyo, Yanga itacheza nusu fainali dhidi ya Ihefu.

Ihefu imetinga hatua hiyo baada ya kuifunga Mashujaa ya Kigoma kwa mikwaju ya penalti 4-3 baada ya kutoka suluhu katika dakika 90.

Related Posts