Kigoma. Baada ya kusimama kufanya kazi kwa miaka 20 kutokana na uchakavu, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limefufua boti ya MV Bulombora ambayo mbali ya shughuli za uvuvi, kusafirisha watu, itatumika katika shughuli za ulinzi kwenye Ziwa Tanganyika.
Boti hiyo inayofanya kazi chini ya Kikosi cha JKT 821 cha Bulombora ina uwezo wa kubeba abiria kati ya 30 hadi 60 huku mizigo ikiwa ni kati ya tani 60 hadi 80.
Akizindua boti hiyo Aprili 30, 2024, Brigedia Jenerali Hassan Mabena amesema boti hiyo itatumika katika shughuli za ulinzi wa Ziwa la Tanganyika hususan kupamba na wavuvi haramu na wahalifu wanaoleta vurugu na kuwafanyia fujo wavuvi.
Amesema msukumo wa kuitengeneza boti hiyo, ulitokana na mkakati kabambe wa JKT wa kuhakikisha kuwa wanafanya uzalishaji mkubwa katika eneo la kilimo, mifugo na uvuvi.
“Ukiangalia mkao wa kikosi 821 (Bulombora) upo pembezoni kabisa mwa Ziwa Tanganyika na ndani ya hili kuna fursa nyingi sana zikiwemo za usafirishaji upande mmoja wa ziwa kwenda mwingine. Lakini kuna shughuli za uvuvi,”amesema.
Amesema mkuu wa kikosi aliyekuwepo wakati huo (hakumtaja), alipeleka ombi la ukarabati makao makuu ya JKT na yeye kama Mkuu wa Tawi la Utawala la JKT, aliliangalia na kulipeleka kwa wataalamu ambao waliliangalia na kuona inawezekana.
Amesema baada ya kukamilika kwa hilo na kuonekana inaweza kukarabatiwa walipeleka ombi hilo kwa Mkuu wa Jeshi la JKT ambaye aliona kuna uwezekano mkubwa wa kuifufua boti hiyo.
Amesema boti hiyo ina uwezo wa kuchukua watu 30 hadi 60 kwa mara moja na mizigo ya tani 60 hadi 80 na kwamba itakwenda kupunguza changamoto ya usafiri kwa watu wanaotumia Ziwa Tanganyika.
Amesema pia kukarabatiwa kwa boti hiyo, kutaongeza ajira kwa sababu shughuli zitakazofanyika sio zitafanywa na wana JKT bali na watu wengine.
Amefafanua sehemu ya fedha zitakazopatikana kutokana na shughuli ya boti hiyo zitapelekewa serikalini kama maduhuli.
Brigedia Jenerali Mabena amewataka viongozi wa kikosi hicho kuifanyia boti hiyo matengenezo kila inapotakiwa kwa sababu kwa kufanya hivyo chombo hicho kitadumu.
Amesema ni imani yake kuwa boti hiyo itafika miaka 50 na kwa kipindi hicho watakuwa wameleta vyombo vingine vingi ili kusaidia uzalishaji mkubwa kwenye eneo hilo la samaki na kusafirisha watu, ili kuhakikisha wanafika kwa usalama.
Mkuu wa Kikosi cha 821 KJ Bulombora, Luteni Kanali Juma Hongo amesema watamalizia kulipa Sh28 milioni zilizobakia baada ya chombo hicho kufanya kazi ndani ya mwaka mmoja.
Amesema kuwa watalipa fedha hiyo, kutokana na mapato ya ndani ya kikosi hicho.
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya HB Experts LTD, waliokarabati meli hiyo, Hemed Rashid amesema walianza matengenezo ya boti hiyo, Agosti 29, 2022 kwa gharama ya Sh320.48 milioni na hadi jana walikuwa wamelipwa Sh291.9 milioni.
Amesema katika ukarabati huo wamebadilisha boti hiyo kwa asilimia 75 na kuwataka kikosi hicho kuzingatia muda wa matengenezo.
Rashid amesema kuwa endapo itatunzwa vizuri na kuzingatia matengenezo kama yanavyoshauriwa na wataalamu, boti hiyo inaweza kudumu kwa zaidi ya miaka 20.