Aliyekuwa kocha wa makipa wa Simba, Muharami Sultani ‘Shilton’ (40) na wenzake wanaendelea kusota rumande kwa siku 526 sasa kutokana na upelelezi wa shauri hilo kutokamilika.
Sultani na wenzake watano wanakabiliwa na mashtaka manane yakiwemo ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroine zenye uzito wa kilo 34.89 pamoja na kutakatisha fedha.
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisitu, Novemba 21, 2022 na kusomewa mashtaka yao.
Hata hivyo, tangu wafikishwe mahakamani hapo siku hiyo, hadi Jumanne Aprili 30, 2024 washtakiwa hao wamefikisha siku 526, sawa na mwaka mmoja na miezi mitano na siku 9 wakiwa rumande kutokana upelelezi wa shauri hilo kutokukamilika.
Licha ya upelelezi wa kesi hiyo ya Uhujumu Uchumi namba 71/2022 kutokukamilika, pia washtakiwa hao wanaendelea kusota rumande, kutokana na mashtaka yanayowakabili, hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.
Aprili 30, 2024, wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Mwanga aliieleza mahakama hiyo, kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika, hivyo waliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Mwanga alitoa taarifa hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Kutokana na maelezo hayo, hakimu Lyamuya aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 14, 2024 itakapotajwa na washtakiwa wapo rumande kwa sababu kesi ya kusafirisha dawa za kulevya haina dhamana kwa mujibu wa sheria.
Pia mashtaka ya kutakatisha fedha hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.
Washtakiwa hao wanatetewa na wakili Daudi Mzeri na kesi hiyo ilisikilizwa kwa njia ya video huku washtakiwa wakiwa rumande.
Mbali na Sultani, washtakiwa wengine ni mmiliki wa kituo cha Cambiasso Sport Academy kilichopo Tuangoma, Kambi Zubery Seif; Said Matwiko mkazi wa Magole; Maulid Mzungu maarufu Mbonde (54) mkazi wa Kisemvule ambaye ana undugu na mtuhumiwa Muharami.
Wengine ni John John maarufu Chipanda (40) mkazi wa Kitunda ambaye kazi yake ilikuwa ni kutafuta vijana wenye vipaji na kuwapeleka Cambiasso Sport Academy pamoja na Sarah Joseph.
Awali, washtakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka matano, lakini Septemba 23, 2023 Mkurugenzi wa mashtaka nchini (DPP) aliwabadilishia hati ya mashtaka kwa kuwaongezea mashtaka matatu likiwemo la kutakatisha fedha na kisha kuwasomea upya mashtaka yao.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka manane yakiwemo ya kusafirisha dawa za kulevya na kutakatisha fedha.
Shtaka la kwanza, ni kuongoza genge la uhalifu shtaka linalowakabili watu wote ambapo Inadaiwa tarehe tofauti kati ya mwaka 2016 na Novemba 4, 2022 maeneo tofauti na ndani ya mkoa wa Dar es Salaam na Pwani washtakiwa hao waliongoza genge la uhalifu kwa lengo la kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin Hydrochloride.
Shtaka la pili inadaiwa, Oktoba 27, 2022 katika eneo la Kivule Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam washtakiwa hao kwa pamoja walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin zenye uzito wa kilo 27.10.
Shtaka la tatu inadaiwa Novemba 4, 2023 washtakiwa, Zuberi, Zungu na Mtwiko katika eneo la Kamegele wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin zenye uzito wa kilo 7.79.
Katika shtaka la nne, tano, sita na saba ambayo ni ya utakatishaji fedha yanayomkabili mshtakiwa Kambi inadaiwa kuwa Aprili 15, 2021 katika wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam alinunua magari manne aina ya TATA yenye jina la Safia Group of Companies LTD huku akijua mali hizo zilipatikana kwa kosa la kuongoza genge la uhalifu.
Katika shtaka la nane inadaiwa kuwa Aprili 20, 2021 mshtakiwa Kambi alinunua gari aina ya TATA lenye jina la Safia Group of Companies LTD akijua mali hiyo ilipatikana kwa kosa la kuongoza genge la uhalifu.