Arusha. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amewasili katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha ambapo anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani yanayofanyika kitaifa jijini humo.
Awali Rais Samia Suluhu Hassan, alitarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo.
Leo Mei Mosi, 2024 maadhimisho hayo yameanza ambapo kwa sasa maandamano ya wafanyakazi kutoka sekta mbalimbali nchini yanaingia uwanjani hapo, yakiwa na ujumbe mbalimbali ikiwemo suala la nyongeza ya mshahara.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi Digital, baadhi ya wafanyakazi wamesema wana matumaini ya kupata habari njema kutoka kwa Rais Samia.
Rais wa Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Tumaini Nyamhokya amesema wana matarajio makubwa ya kupokea tamko la Rais Samia kwa wafanyakazi kupandishwa kiwango cha mishahara ili kukabiliana na gharama za maisha.
“Sisi kama watetezi wa masilahi ya wafanyakazi ni jukumu letu kuikumbusha Serikali na waajiri wetu juu ya mambo haya, kuwa mishahara ikiwa bora itawezesha mafao kuwa bora, tukiwa kazini na wakati wa kustaafu,” amesema