KOCHA wa Yanga Miguel Gamondi, amevunja ukimya kwa kusema namna anavyoshangazwa na maisha ya mastaa wa timu hiyo kambini kwa muda wa mwaka mmoja aliokaa na timu hiyo, huku akifichua nyakati ngumu anazokutana nazo pale timu uinapotoka sare au kupoteza mchezo.
Gamondi aliyetua Yanga mwanzoni mwa msimu huu akimpokea Nasreddine Nabi aliyemaliza mkataba na kutimkia FAR Rabat ya Morocco, amekuwa na mafanikio makubwa katika msimu wa kwanza wa kazi hiyo ikiwamo kuifinisha timu hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa baada ya miaka 25 kupita tangu 1998.
Lakini amekionmgoza kikosi hicho kutinga robo fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) ikitetea kiti, lakini katika Ligi Kuu ameiweka kileleni ikifikisha pointi 62 kutokana na mechi 24, ikishinda michezo 20 na sare mbili na kupoteza pia mara mbili na sasa inahitaji pointi 11 tu itangaze ubingwa kwa msimu wa tatu mfululizo.
Akizungumza na Mwanaspoti, kocha huyo amesimulia namna anavyoshangazwa na maisha ya wachezaji wa timu hiyo kambini akisema ndio chachu ya Yanga kufanya vizuri, huku akisema nyakati ngumu pekee ambayo amekuwa akikutana nayo ni pale timu inapopoteza au kupata sare ndipo anaona wachezaji morali iko chini.
“Ushindani wa wachezaji, wote wanatamani kucheza hata wale ambao hawachezi wanaishi na kiu ya kutafuta nafasi na siku akiipata anatamani kufanya kweli,” amesema Gamondi raia wa Argentina na kuongeza;
“Utani na kuishi kwa kupendana kwenye timu hakuna makundi, kila mchezaji anaonekana kutaniana na kuishi kwa upendo na wenzake ndio maana wakishinda mechi kubwa ni rahisi kuona wanacheza muziki kwa pamoja.”
Gamondi ameongeza kwa kusema; “Nawapongeza pia, viongozi wangu kwa kutambua majukumu yao kwa kuwapa stahiki zao wachezaji na kufanya kila kitu, ikiwemo kutengeneza utulivu wa timu na mambo haya yanaleta uwepesi wa majukumu kwa makocha na ndio maana hali ya kupigania ushindi imekuwa kubwa.”
Usiku huu Gamondi atakuwa na kazi ya kukabiliana na Tabora United katika mechi ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho itakayopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, huku ikiwa na rekodi ya kuitambia timu hiyo pambano la duru la kwanza la Ligi Kuu kwa bao 1-0 lililopigwa Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.
Mechi nyingine za leo za hatua hiyo kuwania kucheza nusu fainali itazikutanisha Ihefu na Mashujaa na ile ya Coastal Union dhidi ya Geita Gold, huku Azam na Namungo zitavaana Ijumaa.