Mavunde: Tulitumia saa manane kumvuta GSM Yanga

UKIACHA mapenzi yake ndani ya klabu ya Yanga kama kuna jambo ambalo lilimtambulisha kwa ukubwa Antony Mavunde ndani ya klabu hiyo basi ni ile siku ambayo aliutambulisjha umma wa wanachama na mashabiki wa klabu hiyo juu ya ujio wa mfadhili wa timu hiyo     Ghalib Said Mohammed ‘GSM’.

Mavunde alimtambulisha tajiri huyo mbele ya uma wa Yanga wakati alipokuwa mmoja wa watu waliochangia kuitoa timu hiyo kwenye kina cha ukata wa fedha alipochangia kiasi cha sh 300 milioni kwenye tukio la Kubwa kuliko lililokuwa na malengo ya kusaka fedha za kusaidia kusajili kikosi kitakachorudisha makali ya klabu hiyo.

Baaada ya utambulisho huo baadaye GSM akaingia rasmi ndani ya Yanga na safari ya kuifanya klabu hiyo kuishi kibabe ndani ya mipaka ya Tanzania na nje ikaanzia hapo, hatua hiyo ikalipelekea Mwanaspoti kumtafuta na kufanya naye mahojiano na Mavunde ambaye pia ni Waziri wa Madini na Mjumbe wa Baraza la Wadhamini la timu hiyo.

“Ni kweli ilikuwa safari ya milima na mabonde kuifanya Yanga iweze kufikia hapa,mtakumbuka awali timu yetu ilikuwa chini ya Ufadhili wa ndugu yetu Manji (Yusuf) kabla ya kujitokeza kwa changamoto, lakini mambo yalibadilika na baadaye timu kukosa ufadhili na kupelekea kutokupata namna bora ya kukijenga kikosi,”anaeleza Mavunde safari ya kuikomboa timu hiyo kutoka kwenye hali ngumu ya ukata huku akiendelea kuelezea.

“Hali ile ililazimu kupatikana watu wachache wa kuiokoa Yanga wakati huo na mimi nikiwa miongoni mwao, kwahiyo niwashukuru kwanza viongozi wakati huo chini ya aliyekuwa katibu wetu kwa muda Kaya (Omari) kwa  kunihusisha kwenye jambo hili, bila kuwasahau niliofanya nao kazi kwa pamoja katibu wangu wa kamati ile Deo Mutta akiwemo pia kocha Mwinyi Zahera na Nahodha Ibrahim Hajib.

“Kazi yetu kubwa ilikuwa ni kuirudisha Yanga katika makali na heshima yake na hii ilianzia katika kamati ya hamasa ambapo mimi ndio nilikuwa mwenyekiti hivyo nafurahi kuona ile mipango ya wakati ule inafanikiwa,”.

MABADILIKO ULIIBUKIA HAPO
“Moja kati ya kazi yetu tuliyoifanya kamati ya hamasa wakati ule wakati tunakabidhi lile kalabrasha la utendaji wa kazi yetu ya kamati kwa mwenyekiti wa klabu Mzee MsolA (Dk Mshindo) ndani yake moja ya jambo ambalo tuliliopendekeza ilikuwa ni kuibadilisha klabu juu ya mfumo wa uendeshaji na tulifanya hivyo ili wakati mwingine huko mbele hali kama ambayo iliikumba klabu wakati ule isijirudie tena kupita kwenye changamoto kama zile.

“Nawashukuru SANA viongozi waliopita akiwemo Mzee Msola na hawa wa sasa kama Eng. Hersi (Said) na msaidizi wake Arafat (Haji) kwa kuendeleza na kukamilisha mipango hiyo na sasa tunaona namna mambo yanavyokwenda vizuri na kama ikikamilisha tutakuwa miongoni mwa klabu bora Afrika zinazoendeshwa kwenye mfumo wa kisasa.”

GHARAMA ZA KUENDESHA KLABU
“Wakati tunachangishana wanachama na mashabiki waliokuwa wakitoa pedha zao  japo zilikuwa ndogo ila zilitusaidia sana, ila tulitoka na funzo kubwa kipindi kile, tuwaheshimu sana watu wanaowekeza kwenye mpira, tunaona tu Simba au Yanga zinacheza kimataifa ila nyuma yake wapo ambao wanapambana kuhakikisha mambo yanaenda bila kujali wanaumia vipi.

KUMSHAWISHI GSM
“Haikuwa kazi rahisi kumpata GSM kwani wakati tunaenda kumuomba awe mdhamini alihitaji muda wa kufikiria zaidi ili aweze kuona ni kwa namna gani anaweza kukubaliana nasi kwani yeye ni mfanya biashara.

Ilichukua masaa nane kujenga hoja mimi pamoja na Maulid Kitenge kujenga hoja juu ya Ghallib kukubaliana nasi, lakini ukimuuliza sasa miongoni mwa maamuzi ambayo hatokaa ayajutie basi hili la kudhamini na kuifadhili Yanga litakuwa la kwanza.

“Ilikuwa ni safari iliyokuwa inahitaji umakini, nafurahi kwani sasa anatajwa sana kama mwekezaji kinara anayejulikana kwa kuisaidia Yanga hiyo ni zaidi ya faida kwake lakini kwa Yanga nadhani nao wanaona faida ya kuwa na mtu kama Ghalib kwa namna anavyojitoa kwa klabu hii, nafurahi pia kuona mapenzi ya Wanayanga kwake ni makubwa sana.”

MIPANGO YA GSM
“Mipango yake ni mingi sana na kama ikitimia  basi Yanga itakuwa mbali, naomba nisiiongelee sana mingine mtakuja kuyaiona wenyewe huko mbele, ila tu kuwa tuna viongozi mahiri ndani ya klabu yetu na wengine wakiwemo pia CAF kama Hersi kwetu ni faida kubwa na nyota njema ya maendeleo inaonekana.

MIPANGO YA UWEKEZAJI
“Swala la uwekezaji wa hisa kwa Mwanachama ni jambo linalohitaji elimu kubwa, kwahiyo kama watafanya hivyo juu ya 49% kuhusu wao basi watajitokeza kwa wingi kuwekeza katika Klabu yao.

“Hili sio jambo lililozoeleka kwa upande wa Nchi yetu kwani halijawahi kutokea hapo kabla, kwahiyo linahitaji kupewa kipaumbele kikubwa na kupewa uzito ili iwe rahisi kufanikisha hilo kinyume na hapo basi hawatafikia lengo.

“Kuna haja kubwa ya kuhakikisha elimu hii inafika kwa wanachama na mashabiki wetu ili nao wapate kuelewa kwa undanhi faida ya hili ambalo linasemwa sasa, kama wanachama hawatapata nafasi ya kulifahamu kwa undani maana yake safari hii itakuwa ndefu na nawaamini viongozi wetu watalifanya hili.

MIPANGO YA USAJILI
“Kuhusu usajili tunawaachia kamati ya utendaji ila mimi kama mjumbe kazi yangu ni usimamizi wa mali za Klabu na mfumo wa uendeshaji kama ambavyo mambo yanakwenda sawa  hili eneo la usajili kwangu mimi naona kila kitu kinakwenda vizuri kazi ya maboresho ya kikosi chetu inakwenda vizuri na matunda yake ni haya ambayo tunayaona timu kuendelea kufanya vizuri kwenye mashindano yake, nawapongeza sana viongozi wetu wa klabu.

“Itapendeza nikilisema hili kupitia uongozi wa Hersi wamekuwa ni vijana wenye uelewa mkubwa juu ya nini wanachokitaka na kipi kinatakiwa kufanyika kwa klabu yetu hivyo hakuna shida kila kitu naamini kinakwenda kuwa sawa kabisa chini ya uongozi wao na wanafanya kazi kubwa sana kwa muda ambao wamekaa madarakani tunaona namna ambavyo klabu inapiga hatua na kama kuna kitu kinatuivutia kama baraza la wadhamini na hii mipango ya kuifanya klabu kujiendesha kwa kipato chake.”

“Nyie wanahabari mmekuwa mashuhuda kwa mambo ambayo uongozi huu umeyafanya kwa kusaini mikataba mbalimbali yenye tija kwa Yanga ili isimame kiuchumi na kuiondoa kwenye hali ngumu ambayo ilipitia hapo nyuma.

YANGA LIGI KUU
“Kwa upande wangu naona timu imefanya vizuri mpaka sasa na hii imetokana ubora wa kikosi na benchi la ufundi japokuwa tuna alama nyingi na kushinda michezo mingi  bado haijafika ligi mwisho ila tunaimani na jinsi mwenendo wa timu unavyokwenda.

“Sasa Yanga ina umoja sana haina mipasuko sana, jambo ambalo linaiwezesha timu kuwa na utulivu mkubwa na kuzidi kuwa bora na kufanya vizuri kila shabiki, mwanachama na hata viongozi wao wako nyuma ya timu yao.”

DODOMA JIJI YUMO
“Mimi ni kiongozi wa Dodoma lazima niwe karibu sana na timu ya Dodoma Jiji kwani yenyewe ndio inawakilisha mkoa kwa ngazi kubwa ya kisoka hivyo kwa namna yoyote lazima ni hakikishe iko salama.

Changamoto hazikosekani ligi sasa imekuwa na ushindani na ni mkubwa hivyo tunaendelea kuipambania timu japo haiko kwenye nafasi mbaya ila matamani yetu ni kuona inaendelea kufanya vizuri na ninaamini itaendelea kusalia Ligi Kuu.”

MICHEZO IKO DAMUNI
Kama unadhani Mavunde anapenda soka pekee unakosea pale Dodoma ameshiriki kufanya mambo mengi ikiwemo michezo mingine

“Hapa Dodoma nimekuwa nikihamasisha kukuwa kwa michezo mingi, ukiacha mambo ya soka ambayo sio tu Dodoma Jiji tumeimareisha kuchezwa soka kuanzia ngazi ya chini kabisa mitaani mpaka Ndondo cup, hapa kama kuna timu itakosa jezi zangu sitegemi hilo.

“Ukiacha soka nimeshiriki kujenga ustawi mzuri wa michezo mingine, mmeona pale shule ya Kiwanja cha ndege nimejenga uwanja wa michezo mingine kama mpira wa pete, mpira wa kikapu na mingine kwa kuwajengea uwanja wa kisasa ambao wakati wowote kuanzia sasa utakamilika, lengo ni moja tu kupata wana michezo bora kuanzia mashuleni.

UWANJA WA YANGA
“Kati ya mafanikio makubwa yanayosubiriwa kwa hamu katika uongozi wa Hersi na Arafat ni kuhusiana na swala uwanja na bahati nzuri linaungwa mikono na wanachama, wadhamini na Serikali.

Sisi tuko tayari kuwapa sapoti kwani Klabu kubwa kama Yanga mpaka sasa inatakiwa iwe tayari ina uwanja wake unaojitegemea na hiyo ni shauku yetu kuona hilo likitimia nakwa mipango ambayo tunaiona tunaimani kwamba kila kitu kitakuwa sawa.”

UKARIBU NA AZIZ KI
“Aziz KI ni rafiki yangu na ni mchezaji mzuri sana na sio mara ya kwanza kwa yeye kuniahidi mabao, aliwahi kunipa mpira baada ya kufunga hatrick nadhani mnakumbuka.

“Siku hiyo alinisistiza sana niende uwanjani kumbe alikuwa na zawadi hiyo, amekuwa mchezaji mzuri mwenye uwezo wa kubadilisha mchezo hivyo namtakia kila la kheri katika michezo yote atakayocheza.”

Related Posts