Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imebaini uwepo wa mgandamizo mdogo wa hewa ambao utachangia uwepo wa mvua kubwa na upepo katika mikoa mitano nchini.
Mikoa inayotarajiwa kupata mvua hizo ni Mtwara, Lindi, Pwani, Morogoro, Dar es Salaam na maeneo ya jirani.
Taarifa hiyo imetolewa na TMA leo Mei mosi, 2024 ikielezea uwepo wa mgandamizo mdogo wa hewa katika bahari ya hindi mashariki mwa Pwani ya Mtwara.
“Mifumo ya hali ya hewa iliyopo kwa sasa inaonyesha kuwa mgandamizo mdogo wa hewa unatarajiwa kuimarika na kufikia hadhi ya Kimbunga kamili hadi kufikia Mei 2, 2024,” imeelezwa kwenye taarifa hiyo.
TMA imesema wakati mgandamizo huo mdogo wa hewa ukiendelea kuimarika, unatarajiwa pia kusogea kuelekea baadhi ya maeneo ya Pwani ya Tanzania kuanzia usiku wa kuamkia Mei 3 2024.
Mgandamizo huo mdogo wa hewa unatarajiwa kuendelea kuwepo katika maeneo ya ukanda wa Pwani hadi Mei 6, 2024.
“Hata hivyo, mgandamizo huo mdogo wa hewa unatarajiwa kupungua nguvu baada ya Mei 6, 2024,”imebainishwa taarifa hiyo.
Mamlaka hiyo imewataka wananchi kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka TMA pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalamu katika sekta husika, ili kujikinga na athari zinazoweza kujitokeza.”
Taarifa ya TMA iliyotolewa Aprili 29, 2024 ilieleza hali ya upepo mkali itaendelea kuwepo hadi Mei mosi, 2024 na huenda ikasababisha mvua kuanzia Mei 4 hadi 7, 2024 kwenye mikoa ya Pwani ya Kusini.
Taarifa ilieleza upepo mkali unaoendelea katika maeneo mengi nchini umesababishwa na kuimarika kwa migandamizo mikubwa ya hewa iliyopo katika ncha ya Kusini mwa Bara la Afrika, ambayo kukoma kwake ndiko kunawezesha mifumo iliyokuwa inaleta mvua kuimarika.
“Hali ya upepo mkali inaenda kukoma ndani ya siku tatu zijazo (kuanzia leo Aprili 29 hadi Mei mosi) na ndiyo itasababisha mvua kurudi kwenye maeneo ya Pwani ya Kusini kuanzia Mei 4 hadi 7.”
Meneja wa Utabiri wa TMA, Dk Mafuru Kantamla alisema mifumo inaonyesha dalili za mvua kwenye Pwani ya Kusini inayohusisha mikoa ya Lindi, Mtwara, Dar es Salaam na Pwani ambayo ipo jirani na Bahari ya Hindi.
“Kuna viashiria za mvua zinakuja kwenye mfumo kuanzia Mei 4 hadi 7, maeneo ya Pwani ya Kusini bado kuna mvua, tunaendelea kufuatilia siku zikikaribia kama mifumo haitabadilika tunaweza kutoa angalizo au tahadhari kwenye mikoa ya Lindi na Mtwara,” alisema.
Alisema wakati msimu wa masika ukielekea ukingoni, baadhi ya maeneo yanatarajiwa kuwa na upungufu wa mvua, huku yale ya mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Dodoma, Singida, Mbeya, Rukwa, Songwe, Iringa, Njombe na Ruvuma mvua ni kama zimeisha.
“Tukiangalia kwenye utabiri zilipaswa kuisha wiki ya pili na ya tatu ya Aprili, lakini hivi sasa kuna misimu miwili inaendelea, ambayo ni ya mvua za msimu zinazoanza Novemba hadi Aprili na za masika zinazoanza Machi hadi Mei,” amesema.
Kilichoshuhudiwa mpaka sasa
Akiwa Bungeni Dodoma, Aprili 25, 2024 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alizitaja athari za mvua zilizoanza kunyesha nchini kuanzia mwaka jana kuwa zimesababisha vifo, uharibifu wa mazao, makazi, mali za wananchi, miundombinu kama vile barabara, madaraja na reli.
Waziri Mkuu Majaliwa kupitia taarifa yake alisema zaidi ya kaya 51,000 na watu 200,000 waliathirika na watu 155 kupoteza maisha na wengine 236 wakijeruhiwa.
Pia nyumba zaidi ya 10,000 ziliathirika kwa viwango tofauti, miundombinu ya shule, zahanati, nyumba za ibada, barabara, madaraja, mifugo na mashamba yenye mazao mbalimbali zilitajwa kuathirika.