Mkurugenzi wa zamani ZBC ambwaga tena DPP kortini

Zanzibar. Jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani Tanzania, limeitupilia mbali rufaa iliyokuwa imekatwa na Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) dhidi ya aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC), Hassan Mitawi.

Kupitia rufaa namba 82 ya mwaka 2023, DPP alipinga hukumu ya Mahakama Kuu Zanzibar, iliyomwachia huru Mitawi na mtumishi mwingine wa ZBC, Mamy Matata ambaye sasa ni marehemu, waliokuwa wameshtakiwa kwa tuhuma za ukwepaji kodi.

Katika hukumu yao, jopo hilo la majaji, Winfrida Korosso, Rehema Kerefu na Gerson Mdemu waliyoitoa Aprili 30, 2024, walisisitiza Jaji aliyewaachia huru alikuwa sahihi kisheria kwa vile mashitaka dhidi ya wawili hao hayakuthibitishwa kwa viwango vya kisheria.

DPP katika sababu zake nne za rufaa, alikuwa anadai kuwa Jaji aliyewaachia alikosea kisheria alipohitimisha kuwa Mitawi na mwenzake hawakuwa wamefanya biashara yoyote ya uuzaji magari katika eneo la ZBC, ambalo ni eneo la kazi la Mitawi.

Pia, alisema Jaji alikuwa amekosea alipohitimisha kuwa mjibu rufaa wa pili, Mamy ambaye alifariki Aprili 19, 2023 hakuwa na mamlaka ya kuuza magari ambayo kisheria yalikuwa yanamilikiwa kihalali na mjibu rufaa wa kwanza, Hassan Mitawi.

Kupitia kwa wakili wa Serikali mkuu, Said Ali Saidi akisaidiwa na wakili Shamsi Yasin Saady, DPP pia alisema Jaji aliyesikiliza kesi alikosea kishera aliposema kosa la ukwepaji kodi halikuthibitishwa na pia kosa la matumizi mabaya ya ofisi halikuthibitishwa.

Aprili 22, 2024 siku rufaa hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kusikilizwa, Wakili wa wajibu rufaa, Salim Hassan Mnkonje akisaidiwa na wakili Abdulkhalid Mohamed Ally, aliijulisha mahakama kuwa Mamy alikuwa ni marehemu hivyo akaondolewa katika rufaa hiyo.

Tuhuma za Jamhuri zilisemaje

DPP katika kesi waliyofungua mahakama Kuu Vuga, walidai wawili hao walikuwa wameshtakiwa chini ya sheria ya Kuzuia Rushwa na Makosa ya Uhujumu Uchumi (Zaeca) ya 2012 na kwamba kosa la kwanza walilitenda mwaka 2014.

Kulingana na mwenendo wa kesi uliorejewa na majaji hao ni kuwa mwaka huo, siku tofauti katika eneo la ZBC huko Unguja, wawili hao kwa makusudi walifanya biashara ya kuuza magari bila kusajiliwa kama walipa kodi wala kulipa kodi Mamlaka ya Kodi Zanzibar.

Katika shtaka la pili lililokuwa kwa Mitawi pekee, lilihusu matumizi mabaya ya ofisi kinyume cha kifungu 61 cha Zaeca kwamba mwaka huo na eneo hilo, mjibu rufaa huyo alitumia madaraka yake kufanya biashara ya kuuza magari ili kujipatia manufaa.

Hata hivyo, wajibu rufaa hao walikanusha mashtaka hayo na upande wa mashtaka uliita mashahidi watano wakiwamo maofisa kutoka Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (Zaeca) kwa ajili ya kuthibitisha mashtaka hayo.

Ushahidi wa Jamhuri ulivyokuwa

Shahidi wa kwanza wa Jamhuri, Rashid Said Suleiman, Ofisa mchunguzi kutoka ZAECA, alieleza kuwa Februari 11,2014 saa 5:00 asubuhi akiwa katika majukumu yake ya kawaida, aliingia katika eneo la ZBC eneo la Mnazi Mmoja na kukuta magari tofauti tofauti.

Alieleza baadhi ya magari yalikuwa na usajili wa nje ya nchi, na hapo alishuku uwepo wake hapo ambapo katika kuchunguza alikutana na shahidi wa tatu, Ali Kombo ambaye ni mtumishi wa ZBC aliyemweleza magari hayo yanauzwa na akadai ni mali ya Mitawi.

Ofisa huyo akatoa taarifa hiyo Zaeca ambapo shahidi wa sita, Abubakar Mohamed Lunda alichukua taarifa hiyo kwa ajili ya uchunguzi ambapo alitembelea eneo hilo la ZBC alikokuta magari mbalimbali yakiwa na namba za usajili za nje ya Tanzania.

Baada ya kumhoji shahidi wa tatu na wa tano, Ahmed Haji Saadati ambaye ni mtunza stoo na Katibu wa Bodi ya Mapato Zanzibar, shahidi huyo wa sita alidai kujiridhisha kuwa magari aliyoyakuta katika eneo la maegesho ZBC, yanamilikiwa na Mitawi.

Ofisa huyo alitafuta namba ya mrufani wa pili (Mamy) na kumpigia na kujifanya anahitaji kununua gari na wakakutana Juni 3,2014, akampa funguo na kukagua gari mojawapo na hapo ndipo walipotokea polisi wawili wa kike na kumweka chini ya ulinzi.

Magari sita yalichukuliwa na kupelekwa kituo cha Polisi Madema ambapo kwa mujibu wa shahidi huyo, moja ya magari hayo lilikuwa ni BMW lenye namba Z992 EU.

Shahidi wa 4, Zuwena Omar Kesi ambaye ni Ofisa Biashara anayehusika kutoa leseni aliieleza mahakama kuwa hakuna kumbukumbu kuonyesha wajibu rufaa walikuwa ni wafanyabiashara, ushahidi kama huo ulitolewa na Saadati kutoka bodi ya mapato.

Katika utetezi wao mbele ya Mahakama Kuu ya Vuga, washtakiwa wote wawili walikanusha mashitaka hayo lakini Mitawi akakiri ni mkurugenzi mkuu wa ZBC na hutumia eneo la maegesho kuegesha magari yake, lakini akakanusha kutenda kosa lolote.

Alifafanua kuwa hakufanya biashara yoyote ya kuuza magari katika eneo hilo la ZBC na wala hakuwahi kukwepa kodi yoyote, kwani magari yake yalilipiwa kodi ndio yakatoka bandarini na kwamba yeye anamiliki namba ya Mlipa Kodi (TIN) namba 116-576-368.

Namba hiyo ilitolewa Machi 2,2012 na kueleza kuwa lilikuwa jambo la kawaida kwa watumishi wa ZBC kuegesha magari yao bure eneo hilo na  hakuwa na nia yoyote ya kufanya biashara kama Jamhuri ilivyodai.

Mrufani wa pili ambaye sasa ni marehemu, naye alikanusha mashitaka akisema kuna siku alipigiwa simu na mtu akisema anataka kununua gari lililoegeshwa ZBC, lakini akamwambia gari hilo sio lake bali linamilikiwa na mama yake na sio la baba yake.

Wakati huo yeye alikuwa Dar es Salaam, hivyo alisafiri hadi Zanzibar ambapo walikutana na mtu huyo na kumuonyesha gari hilo na akataka apewe nyaraka za umiliki ambazo hakuwa nazo, kwani zilikuwa kwa wakala Dar es Salaam na hapo ndipo akakamatwa.

Katika utetezi wake, alisema alipokamatwa hakuwa amefanya biashara yoyote kwa sababu kulikuwa hakuna mabadilishano ya fedha na utoaji wa stakabadhi ya mauzo.

Baada ya kukamilika kwa ushahidi wa pande zote mbili, Jaji aliyesikiliza shauri hilo aliona kuwa upande wa Jamhuri haukuwa umethibitisha shitaka hilo dhidi ya washtakiwa hao katika kiwango kinachokubalika kisheria bila kuacha mashaka, hivyo akawaachia huru.

DPP hakuridhika na uamuzi huo ndipo akaamua kukata rufaa mahakama ya rufani.

Baada ya kusikiliza mawasilisho ya hoja za rufaa za pande zote mbili, majaji hao walisema hoja iliyokuwa mbele yao ya kutolewa maamuzi ni kama upande wa mashitaka ulikuwa umethibitisha shitaka hilo pasipo kuacha mashaka kama sheria inavyotaka.

Hata hivyo, majaji hao walisema kabla ya kujadili hilo, ni muhimu kueleza kuwa hiyo ikiwa ni rufaa ya kwanza ikiwa katika mfumo wa kuisikiliza upya, hivyo mahakama ina wajibu wa kufanya tathmini ushahidi kwa ujumla wake na kutoa hitimisho sahihi.

Majaji walisema ushahidi unaonyesha kosa la kufanya biashara ya magari halikuthibitishwa kwa sababu hata Ofisa wa Zaeca aliyeweka mtego, hakutoa ushahidi wowote kuthibitisha kuwa alinunua gari mojawapo hapo ZBC na kwa thamani gani.

“Ushahidi wa shahidi wa 1 na wa 6 wa Jamhuri uliegemea katika mashaka ambao kwa mtazamo wa kisheria hauwezi kusemwa ulithibitisha mjibu rufaa wa kwanza (Mitawi) alikuwa na lengo la kufanya biashara ya kuuza magari eneo hilo la ZBC,”walisema.

“Ni kanuni ya msingi ya sheria kwamba mashaka hata kama yawe makubwa kiasi gani, hayatoshi kufanya mshtakiwa aonekane ana kosa analoshitakiwa nalo. Badala yake mashaka hayo yanampa faida mshitakiwa kwa ajili ya kuachiwa huru.”

“Katika mazingira haya, hatuoni tabu kukubaliana na wasilisho la wakili Mnkonje kuwa kwa kuwa mbele ya mahakama Kuu ya Vuga, DPP alishindwa kuongoza ushahidi ili kuthibitisha hoja ya mauzo ya magari, hakuna uhalali kumshutumu Jaji aliyewaachia.”

Majaji hao walisema wanakubaliana pia na wasilisho la wakili Mnkonje kuwa DPP alishindwa kuthibitisha shitaka la kwanza kwamba Mitawi alifanya biashara ya kuuza magari ZBC, hivyo kosa la pili la kukwepa kodi haliwezi kuthibitishwa.

Hii kwa mujibu wa majaji ni kwa sababu shitaka la pili lilitegemea kama shitaka la kwanza lingethibitishwa pasipo kuacha mashaka hivyo wakasema baada ya kupitia ushahidi wote kwa ujumla wake, wanaona shitaka dhidi ya mrufani halikuthibitishwa.

Related Posts