MZEE WA UBISHI WA KALIUA: Aziz KI anabeba tuzo hizi bila ubishi

Hakuna kitu kibaya kwenye mpira wetu kama kutengeneza balansi. Kutengeneza ulinganifu. Kocha wa timu ya taifa ikiita wachezaji, kila mtu anaangalia ulinganifu wa wachezaji wa Simba na Yanga. Bodi ya Ligi na TFF kwenye tuzo zao nao wanapita mlemle.

Ni mwendo wa kuhakikisha kunakuwa na usawa kwa wachezaji wa Simba na Yanga. Hili limepitwa na wakati. Mpira wetu unakua kwa kasi sana.

Ni muhimu na fikra za wadau wa soka nazo zikakua. Ligi yetu inaelekea taratibu kwenye 10 la mwisho. Baada ya mechi tatu au nne tayari tunaweza kuwa tushampata bingwa wa ligi yetu kwa msimu wa 2023/2024.

Kuna kila dalili Yanga atakuwa bingwa. Kuna kila dalali Aziz KI atakuwa mchezaji bora wa ligi yetu. Kuna kila dalili Aziz KI atakuwa kiungo bora wa ligi yetu. Kuna kila dalili Aziz KI atakuwa mfungaji bora. Kuna kila dalili Aziz KI atakuwa mchezaji mwenye nidhamu.

Naomba kwa mwaka huu, tusije tena na stori za kubalansi. Kama akitokea mchezaji mmoja ameshinda tuzo hata sana, apewe tu stahiki yake. Nilipenda sana msimu uliopita kuona Saido Ntibazonkiza akishinda tuzo nne. Huku ndiko tunataka kuona mpira wetu ukielekea.

 Wachezaji wetu wazawa kuna muda baadhi wamekuwa wakipewa tuzo hata wasizostahili kwa utamaduni uleule wa kutaka na kubalansi wageni na wazawa. Ndugu zangu, hatuwezi kuwakuza wachezaji wetu wa ndani kwa kuwapa tuzo wasizostahili. Kama Aziz KI anatakiwa kushinda tuzo sita apewe tu zote.

Kama kwenye kikosi bora cha msimu Klabu ya Simba imetoa mchezaji mmoja awe huyohuyo. Tuache mambo ya kubalansi. Yanatupotosha. Kuna muda tunawapa watu wajina yasiyokuwa yao. Kuna muda tunawapa watu thamani wasiyostahili kabisa.

Wakati anatambulishwa msimu wa 2022/2023, Stephen Aziz KI matumaini yalikuwa makubwa kwake kwa sababu wengi walikuwa washauona ubora wake akiwa na Klabu ya Asec Memosas ya nchini Ivory Coast. Mara chache sana tumepata wachezaji wa aina yake nchini. Mchezaji mwenye umbo kubwa mwenye kasi, ufundi mguuni na mwenye uwezo wa kufunga mabao.

Sio rahisi. Aziz KI ni mchezaji mwenye kila kitu. Alipaswa kutambulishwa na Yanga msimu huu. Baada ya kusuasua msimu uliopita, Aziz KI ameonyesha ubora wake. KI amekuwa mtu mpya kabisa. Kama Yanga atatwaa ubingwa msimu huu, basi ndiye mbeba maono ya klabu. Kama Yanga itatoa mchezaji bora bila shaka jina lake litakuwa juu.

Kama Yanga itatoa kiungo bora kiukweli hakuna mwenye namba bora zaidi yake. Ni Stephen Aziz KI. Mtu na nusu. Hakuna kitu kigumu kwenye michezo na burudani kama kumpa mchezaji bora mwenye nidhamu.

Ustaa unaleta majivuno sana. Ni kazi sana kuwa tegemezi kwenye timu halafu ukawa na nidhamu. Wengi hilo limewashinda. Aziz KI ana yote mawili kwa wakati mmoja. Mkataba wa muda mMrefu unahitajika kwa mchezaji wa aina hii.

 Hawa ndiyo mfano wa wachezaji wa kigeni tunaohitaji kuwaona kwenye ligi yetu. Mchezo wa soka ni mchezo wa maoni.

Namuona Aziz KI akishinda tuzo nyingi sana msimu huu. Apewe tuzo anazostahili. Hakuna haja ya kubalansi. Hawa ndiyo aina ya wachezaji wa kigeni wanatakiwa kwenye ligi. Wachezaji wanaokuja kuongeza thamani. Wachezaji wanaokuja kuichangamsha gemu.

Hakuna kitu kigumu kama kumpata mchezaji mwenye uwezo na nidhamu. Huwezi kusikia kirahisi Aziz KI amechafua hali ya hewa mitandaoni. Huwezi sikia Aziz KI amegomea mazoezi. Huwezi.

Amekuwa na msimu bora sana na uwezekano ni mkubwa akashinda tuzo zaidi ya tano msimu huu. Mara nyingi sana tunajifunza kwa mataifa yaliyotuzidi. Tuzo nyingi kwa wenzetu hutolewa mechi chache kuelekea msimu kumalizika.

Nadhani inatakiwa na sisi twende huko. Hakuna haja ya kusubiri miezi mwili baadaye ndiyo kutoa tuzo. Wachezaji na makocha wakati mwingine wanashindwa kuhudhuria sherehe za tuzo kwa sababu ya kuchelewa. Bado ya Ligi na TFF wanapaswa kulitazama hili kwa umakini na usasa.

 Inapendeza sana kuona washindi na washiriki wote wapo siku ya sherehe. Kumekuwa na vipengele vingi sana kwenye tuzo zetu na wakati mwingine inachosha tu. Hakuna haja kila mtu apate. Washinde wanaostahili tu. Aziz KI amekuwa na msimu mzuri sana pale Yanga. Amefunga sana msimu huu.

Amepigania sana jezi yake ya kijani na njano. Kacheza mechi nyingi sana msimu huu kuliko msimu uliopita bila kuumia. Kwa kiwango alichoonyesha namuona akizoa tuzo za msimu huu. Wachezaji wetu wazawa wana kitu cha kujifunza kwa Aziz KI.

Msimu uliopita kulikuwa na minong’ono mingi sana kutoka kwa wachezaji wakidai hawajapewa pesa zao za tuzo. Ni vyema TFF na Bodi ya Ligi wakaweka wazi ukweli juu ya hili jambo. Kama tuzo zinakwenda sambamba na pesa, washindi wapewe chuo mapema.

 Baada ya ligi kumalizika wapo wachezaji ambao mikataba yao itakuwa imeisha. Wapo wachezaji wanaouzwa na makocha kwenda nchi nyingine. Ni vyema kutoa tuzo na pesa kama zipo mapema ili kila mtu kabla ya ligi kumalizika awe amepata chake.

Mpira wetu unaonekana kukua sana uwanjani. Ushindani wa Simba na Yanga kimataifa umeongezeka. Hakuna anayetolewa hatua za awali kizebe. Hakuna mnyonge tena. Ushindani wa Taifa Stars pia umeongezeka. Safari tunazokwenda Afcon sio kwa bahati mbaya. Ni ubora umeongezeka.

Ni muhimu sasa kupiga hatua kama hizo kwenye uongozi. Lazima tuanze sasa kuwa na viongozi wengi wenye ubora wanaoendana na kazi ya ukuaji wa soka.

Tunahitaji watu ambao wanatazama tuzo za wenzetu kimataifa na namna zinavyoandaliwa. Mambo ya kutoa tuzo baada ya ligi kumalizika ni ya kizamani. Mambo ya kuweka vipengele vingi ili kila mmoja ashinde ni mambo pia ya kizamani.

Tuzo sio kwa ajili ya kila mtu. Ni watu wachache maalumu ambao walikuwa na mchango mkubwa kwa timu kwenye msimu husika. Tusione aibu kumpa Aziz KI tuzo nyingi, anastahili. Amekuwa nguzo muhimu sana kwa Klabu ya Yanga msimu huu. Ni kama amezaliwa upya. Apewe tu maua yake ambayo anastahili.

Related Posts