SIMBA imeanza maisha mapya bila ya Abdelhak Benchikha aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo ikipata sare ya 2-2 na Namungo mjini Lindi katika Ligi Kuu Bara, huku kocha wa zamani wa klabu hiyo Mbrazili, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ akituliza upepo akisema kwa sasa inatakiwa kufanya mambo mawili tu hali iwe shwari.
Simba imeachana na Benchikha aliyedumu kwa siku 156 tu akimrithi Robertinho, ikielezwa ni sababu ya kifamilia na timu kuachiwa Juma Mgunda akisaidiana na Seleman Matola na jana usiku ilivaana na Namungo kwenye Uwanja wa Majaliwa, Lindi na kutoka sare hiyo iliyoifanya ifikishe pointi 47 kupitia mechi 22.
Robertinho aliyefurushwa baada ya kipigo cha mabao 5-1 katika Dabi ya Kariakoo iliyopigwa Novemba 5 mwaka jana, amekuwa akiifuatilia timu hiyo na kujua kila linaloendelea kwa sasa na kusema Msimbazi ili watulize mambo ni lazima wafanye mambo mawili tu.
Akizungumza na Mwanaspoti kutoka Brazili, Robertinho aliyeongoza timu hiyo katika mechi 18 za Ligi Kuu na kupoteza moja tu dhidi ya Yanga, ameyataja mambo hayo mawili ya kufanywa na klabu hiyo kuwa ni, kutengeneza mfumo mzuri wa kupatikana kwa wachezaji sahihi ambao makocha watawahitaji kuendana na falsafa zao.
Robertinho amelitaja jambo la pili kuwa ni kutofanya uamuzi kwa presha ya matokeo kama ambavyo ilivyomfuta kazi yeye kisa matokeo ya mchezo mmoja hatua ambayo inaigharimu timu.
“Simba kuna namna wanatakiwa kwanza kubadilisha mfumo wa upatikanaji wa wachezaji mfumo uliopo sasa hauwapi nafasi makocha kupata wachezaji wanaowahitaji kulingana na falsafa zao, hili ni tatizo na lazima libadilishwe ili mambo yaende sawa,” amesema Robertinho na kuongeza;
“Wapo wachezaji unaambiwa tu, huyu tumemsajili au tunamleta huyu, lakini akija unaona bado hawapo sawa kuendana na unachotaka. Jambo jingine naliona ni kutofanya uamuzi kwa presha, angalia mimi, unawezaje kumuondoa kocha ambaye amekaa na timu kwa miezi 11 bila kupoteza mchezo? Unapoteza mechi moja unaondolewa sidhani kama iko sawasawa.
“Huwezi kuona kocha anapoteza mechi moja tu, inafuta matokeo mazuri ya mechi zaidi ya 14 alizocheza bila kupoteza sidhani kama hiyo iko sahihi. Katika soka kuna makosa hata Simba tumewahi kumfunga mtu mabao saba tena Ligi ya Mabingwa Afrika,” amesema Robertinho aliyewahi kuzinoa timu za Gor Mahia, Rayon Sports na Vipers.
“Hii timu ya sasa inatakiwa kufumuliwa, sio kitu rahisi kwa kocha kuipa mafanikio ambayo klabu inayataka kwa aina ya wachezaji waliopo sasa na hata hawa ambao wameletwa kuna wachezaji umri wao umekwenda hawatakiwi katika soka la sasa ambalo kila mmoja anatakiwa kukimbia,” ameongeza Robertinho aliyeiongoza Simba kwa muda wa miezi minne tu ikiwa ni sawa na siku 118 akitokea Vipers ya Uganda.
Akiwa na Simba kocha huyo aliifikisha timu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita na pia aliipa Ngao ya Jamii iliyokuwa ikishikiliwa kwa misimu miwili mfululizo na Yanga ikiivua taji kwa penalti 3-1 katika fainali ya michuano hiyo iliyochezwa jijini Tanga.
Simba sasa iko katika mikono ya kocha Juma Mgunda ambaye ndiye alimkabidhi timu Mbrazili huyo baada ya yeye kuiongoza kwa kipindi cha miezi minne kasoro kwani alitumika siku 118.