Kwa mara ya kwanza tangu kutokea kwa mkasa wa Mai Mahiu ambapo bwawa lilivunja kingo zake na kusababisha mauti ya zaidi ya watu 70, Rais Ruto alifanya ziara kwa mara ya kwanza, alipokutana na waathriwa.
Rais akitoa mwelekeo kuhusu mvua kubwa zinazoshuhudiwa maeneo mengi nchini Kenya. Amewataka wakazi walio kwenye sehemu hatari kuhamia nyanda za juu.
“Masaa 48 kutoka kesho kila mtu awe ametoka hiyo sehemu, kote nchini. Kwa sababu tena hatutaki kupoteza wananchi. Kupoteza watu 170 sio jambo dogo, na kwa sababu hiyo lazima tuchukue hatua.”, alisema Ruto.
Rais akiongeza kwamba asasi husika za serikali zimekamilisha kazi ya kuangazia maeneo hayo hatari, yakiwemo karibu na mito, mabwawa, na maeneo yenye hatari ya kukumbwa na mmomonyoko wa ardhi.
Maafisa wa kijeshi, pia watakuwa wanazamia shughuli hiyo ya kusaidia waathiriwa, wakishirikiana na vijana wa NYS, walioathirika wakiahidiwa makao mbadala, na kusaidiwa na serikali katika gharama ya mazishi.
”Ilikuwa ni shida kidogo na imetatuliwa”
Hata hivyo, kiongozi wa Azimio Raila Odinga amekosoa serikali kwa kushindwa kuweka mikakati ya kukabiliana na mafuriko. Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Raila amesema kuwa iwapo serikali ingezingatia onyo la idara ya Utabiri wa Hali Anga na kuweka mipango, maafa na uharibifu yangepunguzwa kwa kiwango kikubwa.
Waziri wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen amesema uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta umejaa maji sababu ya mabomba machache ya kutoa maji.
“Nimekuja kusimama na wafanyibiashara na kuwaambia kuwa uwanja wetu uko sawa. Ilikuwa ni shida kidogo na imetatuliwa.”
Hatua za haraka
Hapo jana Jumanne Rais aliongoza kikao cha dharura cha baraza la mawaziri, kujadili mikakati itakayotumika kukabiliana na mafuriko hayo. Baadhi ya waathiriwa walikuwa wamelalamikia kutelekezwa na serikali, wakijihusisha kwenye shughuli za uokozi bila kutumia vifaa maalum.
Idara ya kutabiri hali ya hewa nchini, imesema mafuriko yanatarajiwa kuendelea kwa siku zijazo, mabwawa ya Masinga, na Kiambere yakifikia viwango vya kihistoria.