Serikali imalize mgogoro wa kikokotoo – ACT

Dar es Salaam. Chama cha ACT Wazalendo kimeitaka Serikali kumaliza mgogoro wa kikokotoo cha pensheni za wastaafu, kwa kurejesha kanuni za zamani za mafao zilizotumika kabla ya mwaka 2017.

Kauli inakuja wakati maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) kitaifa yakiwa yamefanyika jijini Arusha na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali, huku mgeni rasmi akiwa Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango.

Katika tamko la siku ya wafanyakazi lililotolewa leo Jumatano, Mei Mosi 2024 na Kiongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu amesema wastaafu walipwe asilimia 50.5 ya pensheni kama kiinua mgongo.

“Zirejeshwe kanuni za zamani za kukokotoa mafao zilizotumika kabla ya mwaka 2017. Tunatambua kuwa hapa nchini Tanzania hali ya wafanyakazi si nzuri. Kwa kipindi kirefu wamekuwa wakipunjwa masilahi yao kutokana na sera, sheria na kanuni kandamizi,” amesema.

Semu ameitaka Serikali kulipa madeni yote ya wafanyakazi yanayohusisha malimbikizo ya mishahara, likizo, kujikimu, uhamisho na posho za kisheria.

“Serikali na sekta binafsi zipeleke michango yote ya wafanyakazi kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii ikiwamo kwenye Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), ili mifuko hiyo iweze kuwahudumia wafanyakazi,” amesema.

Pamoja na hayo Semu amesema Serikali iache kuingilia vyama vya wafanyakazi nchini, huku akivisihi vyama hivyo kuendelee kupigania masilahi ya wafanyakazi.

Katika taarifa yake, amewatia ari wafanyakazi waendelee kufanya kazi kwa bidii na wasichoke kupambania haki na masilahi yao kila wanapopata nafasi.

“Chama cha ACT Wazalendo kinaungana na wafanyakazi wote kuadhimisha siku hii ni muhimu inayowaleta pamoja wafanyakazi katika kutafakari hali yao, masilahi na stahiki zao. Wafanyakazi ndio wajenzi wa nchi kwa kukuza uchumi, kuimarisha huduma na uzalishaji wa mahitaji ya msingi,” amesema na kuongeza;

“Tunataka wakati wote masuala ya wafanyakazi yawekewe taratibu, kanuni, sheria na miongozo yenye masilahi kwao. Vile vile, tunapigania kuhakikisha kuwa masilahi yao yasiamuliwe na utashi wa Rais.”

Related Posts