SERIKALI KUANZA UJENZI WA DARAJA LA MTO ATHUMANI

Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema Serikali ipo katika hatua za mwanzo za maandalizi ya ujenzi wa daraja la mto Athumani lililopo wilayani Ngorongoro mkoani Arusha.

Akijibu swali bungeni leo, Mhe. Kasekenya amesema katika bajeti ya mwaka wa fedha 2024/25, Serikali imepanga kujenga na kukamilisha daraja hilo ili kunusuru maisha ya wananchi wa maeneo hayo hususan nyakati za mvua.

Amesema ujenzi huo unazingatia umuhimu wa daraja hilo linalounganisha barabara inayoelekea katika kiwanda cha magadi ambacho kipo kwenye hatua za ujenzi na kikikamilika kitatoa fursa za kiuchumi.

“Niwahakikishie wabunge na Wananchi wa eneo husika kwamba daraja la mto Athumani limepewa kipaumbele na Serikali na tayari Wizara imeshapeleka maombi ya fedha za ujenzi wa daraja hilo pamoja na madaraja mengine madogo kumi na tatu, ” amesisitiza Naibu waziri Kasekenya.

Naibu Waziri Kasekenya alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Zaytun Seif Swai alietaka kujua ni lini Serikali itaanza ujenzi wa daraja la Mto Athumani mkoani Arusha.

Daraja la Mto Athumani lipo katika barabara ya mkoa (Reginal Road) ya Mto wa Mbu-Selela-Engaruka-Ngaresero-Sale-Wasso-Loliondo yenye urefu wa (KM 217), katikati ya Kijiji cha Selela na Engaruka mkoani Arusha.

IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI

WIZARA YA UJENZI

Related Posts