Simba, Azam vitani tena kunasa saini ya kiungo fundi

JINA la kiungo Najimu Musa lipo mezani kwa timu za Simba, Azam na KMC huku kila timu ikihitaji saini ya mchezaji huyo kwa msimu ujao.

Kiungo huyo mzawa anayekipiga Tabora United ni miongoni mwa wachezaji waliomvutia kocha aliyeondoka Simba, Abdelhack Benchikha na kuwaeleza viongozi wa timu hiyo kumsajili kwaajili ya msimu ujao kwani anaamini angeongeza kitu kikosini hapo.

Wakati Benchikha akionyesha kuhitaji saini ya kiungo huyo anayemudu kucheza namba nane na namba 10, Mwanaspoti limedokezwa kuwa kocha mkuu wa KMC Abdi Hamid moallin tayari atuma baadhi ya viongozi wa timu hiyo kuongea na Najimu atue kikosini hapo kwa msimu ujao.

Inaelezwa Moallin anafurahia zaidi uchezaji wa Najimu akimfananisha na nahodha wa KMC kwa sasa Awesu Awesu hivyo anaamini akitua kwa watoza ushuru hao wa Kinondoni watatengeneza safu bora zaidi ya kiungo.

Katika hatua nyingine Mwanaspoti limeelezwa Azam nayo inamuwinda Najimu na inasikilizia msimu uishe ili iingie kazini kupambania saini yake.

Huu ni msimu wa kwanza kwa Najimu kucheza Ligi Kuu kwani alipanda na Tabora United kutoka Championship msimu uliopita.

Moja ya watu wa karibu na Najimu, aliliambia Mwanaspoti, kiungo huyo msimu ujao hatakuwa Tabora tena bali atajiunga na moja ya timu kati ya hizo tatu za Dar es Salaam.

“Dogo hana presha na ana uhakika wa kucheza Dar es Salaam msimu ujao. Kuna ofa za timu zote hizo lakini hadi sasa hajaamua atacheza wapi jambo ambalo ameuachia uongozi wa timu umalizane na wanaomtaka kwanza,” alisema.

Related Posts