Serikali ya Uingereza imesema hii ni mara ya kwanza kutumika kwa sheria yake mpya ya kimataifa ya vikwazo dhidi ya ufisadi kwa watu wanaokabiliwa na madai ya ufisadi nchini Uganda, na kwamba ni sehemu ya msako wa kimataifa.
Wanaolengwa na vikwazo vya Uingereza nchini Uganda
Among, ni mmoja wa watu watatu wanaolengwa na vikwazo vya usafiri vya Uingereza pamoja na kufungiwa kwa mali.
Walengwa wengine wawili ni Mary Goretti Kitutu na Agnes Nandutu waliokuwa mawaziri wanaohusika na eneo maskini la mpaka wa Uganda laKaramoja.
Bunge la Uganda lasema vikwazo vya Uingereza havina msingi
Taarifa iliyotolewa na bunge la Uganda, hata hivyo, imesema vikwazo hivyo vinatokana na kile ilichotaja kuwa dhana potofu.
Taarifa hiyo pia imesema kuwa Among hajawahi kushitakiwa kwa ufisadi katika mahakama yoyote ya kisheria kinyume na dhana inayoibuliwa katika taarifa iliyotolewa na Uingereza.
Soma pia:Waziri mwingine Uganda apelekwa rumande kwa wizi wa mabati
Kitutu na Nandutu walikabiliwa na madai ya kuiba mabati ya nyumba yaliokusudiwa kutumiwa na watu maskini chini ya mradi unaofadhiliwa na serikali ya Uganda .
Taarifa hiyo ya bunge haikusema iwapo linaamini Kitutu na Nandutu wameshashtakiwa ama la.
Bunge hilo limeongeza kuwa madai ya ufisadi yametumiwa kama mbinu ya kuficha sababu halisi ya vikwazo hivyo ambayo haijatajwa lakini iliyo wazi na iliyoitaja kuwa msimamo wake kuhusu sheria ya kupinga ushoga iliyopitishwa hivi majuzi.
Soma pia:Museveni asaini sheria ya mapenzi ya jinsia moja
Sheria hiyo, iliyopitishwa mwezi Mei mwaka 2023 na kuungwa mkono na Among, inatoa adhabu ya kifungo cha maisha gerezani kwa mahusiano ya kimapenzi ya jinsia moja na iliyo na vipengele vinavyofanya “ushoga uliokithiri” kuwa kosa linalobeba adhabu ya kifo.