Siku hii ni muhimu si tu kwa taasisi mbalimbali za umma na binafsi kwasababu sheria za ajira huwabana kuhakikisha wazingatia taratibu na kanuni zilizowekwa bali pia kwa wafanyakazi ambao kwa asilimia kubwa hutumia muda mwingi mahali pa kazi.
Uwepo wa maadhimisho maalum ya siku hii ni muhimu kwasababu kila mwaka umekuwa ukiwakumbusha na kuwahamasisha waajiri kuboresha mazingira yao ya kazi ili kuleta ufanisi zaidi na kulinda afya na usalama wa wafanyakazi wao.
Suala la afya na usalama mahali pa kazi hutofautiana kutoka sekta moja kwenda nyingine kutokana na aina ya shughuli wanayoifanya. Lakini hii sio sababu ya kwamba taasisi moja kuzingatia zaidi kanuni na taratibu zilizowekwa kuliko nyingine, zote zinapaswa kutimiza vigezo kwa mujibu wa sheria zilizowekwa.
Maadhimisho ya mwaka 2024 yanaongozwa na kauli mbiu inayosema ‘Kuangazia Athari za Mabadiliko ya Tabianchi kwa Usalama na Afya Kazini’. Kwa mujibu wa Shirika Kazi Duniani (ILO) kauli hii mbiu imetokana na ukweli kwamba mabadiliko ya tabianchi duniani yamekuwa yakiathiri wafanyakazi kupitia hatari zinazozidi kuongezeka kama vile joto kali, mionzi, matukio yanayosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa, uchafuzi wa hali ya hewa, magonjwa yanayosababishwa na mionzi nakadhalika.
Kwa Puma Energy, dira yetu ya Afya, Usalama, Usalama, na Mazingira (HSSE) ni “Kuwezesha na kuendeleza wafanyakazi wetu kuwa mstari wa mbele katika masuala ya Afya, Usalama, Ulinzi, na Mazingira ili Kuziwezesha Jamii Zetu.” Hii inamaanisha kwamba tunaendelea kujitolea kila wakati kuendeleza wafanyakazi wanaohusishwa, wanaowezeshwa, na wanaoshirikishwa kuweka kipaumbele kuhusu afya na usalama wao, pamoja na wa wengine.
Akizungumzia kuhusiana na umuhimu wa maadhimisho ya siku hii, Meneja wa Masuala ya Afya, Usalama, Ulinzi, na Mazingira (HSSE) wa Puma Energy Tanzania, Bw. Ambokege Minga ameelezea kuwa wamewekeza nguvu kubwa sio tu katika kuhakikisha kuwa kampuni inazingatia kanuni na taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa sheria bali pia hutoa elimu ya kina kwa wafanyakazi na washirika wote katika uendeshaji wa shughuli zake nchini.
“Kampuni inaongozwa kwa mujibu wa amali ambazo zinawataka wafanyakazi na washirika wote kuzifuata katika uendeshaji wa shughuli zetu za kila siku. Tunajivuna kuwekeza nguvu kubwa katika kutoa elimu na kuwahamasisha wafanyakazi kuzingatia masuala ya afya na usalama mahali pa kazi na kuwa mabalozi kwa wenzao nchini kote. Tumewapatia nguvu ya kusimamia na kutoa taarifa muda na mahali popote ambapo wataona kanuni za afya na usalama zitakapokiukwa,” aliongezea Bw. Minga.
Bw. Minga aliendelea kuwa uzingatiaji wa afya na usalama hauishii kwa wafanyakazi pekee bali pia hata kwa wakandarasi wanaofanya nao kazi pamoja na wageni wanaowatembelea. Lengo ni kuhakikisha hakuna mtu yoyote anayeumia au kupata madhara pindi anapofanya nao kazi au awapo maeneo yao ya kazi.
Puma imeongezea kuwa inatoa vifaa vya kuwakinga wafanyakazi wake na hatari ambazo zinaweza kujitokeza wakiwa mahali pa kazi kama vile vikingamwili. Pia, inawahamisha kutoa taarifa pindi wanapoona sheria zinakiukwa.
“Tunajivunia kuwa mpaka sasa tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa kufikia malengo makubwa ya masuala ya afya na usalama kwasababu hatujapa kesi za ajali au vifo mahali pa kazi kuanzia mwaka kuanza mpaka sasa hivi. Tunafanya jitihada kubwa katika kutoa elimu, kuwalinda na kuwahamasisha wafanyakazi wetu wote katika shughuli zetu za upokeaji, utunzaji, na usafirishaji wa mafuta kwa maendeleo ya wananchi na taifa zima kwa ujumla,” aliongezea Bw. Minga.
Kwa upande wake Mtaalamu wa Udhibiti wa Mazingira ya Usalama wa Afya na Ubora wa Puma Energy Tanzania, Bi. Rehema Madoffe amemalizia kwa kusema kuwa, “tunahakikisha wafanyakazi wote wanakuwa na bima za afya bora ambazo huwalinda pindi wanapokumbwa na changamoto za kiafya. Pia, mahali pa kazi kuna miundombinu imejengwa kwa uthabiti na ubora ili kukabiliana na changamoto mbalimbali kama vile majanga ya moto.
Kwa kuongezea, wafanyakazi hupatiwa mafunzo kukabiliana na majanga ya moto ambapo kila mwezi kwa baadhi ya maeneo yetu ya kazi huwa tunafanya mafunzo ili kujiandaa pindi tunapokumbwa na majanga ya aina yoyote.”