Wahamasishwa kukopa bodaboda na bajaji kujikwamua kiuchumi

Dar es Salaam. Katika kukabiliana na tatizo la ajira nchini, vijana wametakiwa kujitokeza kuomba mikopo ya pikipiki na bajaji za kufanyia biashara kwa lengo la kujikwamua kiuchumi.

Hayo yamezungumzwa na Mkurugenzi wa masoko wa Kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (METL) na Mo Finance, Fatema Dewji alipokuwa akizindua rasmi kampuni ya mikopo Mo Finance itakayokuwa ikitoa mikopo ya vyombo hivyo.

Fatema amesema kwa zaidi ya muongo mmoja sasa, kampuni hiyo ya bajaji imebadilisha maisha ya Watanzania wa hali ya chini kwa asilimia kubwa, katika kujikimu kiuchumi.

“Tumegundua changamoto kubwa wanayokumbana nayo vijana wengi ni umiliki wa vyombo hivi ambayo ni matokeo ya kuwa na kipato cha chini, hivyo ili kuwasaidia kujikwamua kiuchumi ni kuwawezesha kumiliki vyombo vyao wenyewe,” amesema Fatema.

Ameongeza kuwa “Kwa kupitia kauli mbiu ya Mo Finance ya ‘Kukuwezesha kwenye Uhuru wa Kifedha’ tumelenga kuwakwamua kiuchumi vijana wengi wa mtaani kupitia mikopo hii itakayozalisha ajira nyingi nchini.”

Amesema, hii ni mara ya kwanza kwa kampuni ya METL kujihusisha na mikopo, huku akisisitiza kamba haijawahi  kuwa wala hakuna kampuni nyingine yoyote kwa jina lao au Mkurugenzi Mkuu, Mohammed Dewji au chapa ya Mo inayotoa mikopo ya aina nyingine yoyote.

Fatema ametoa msisitizo huo huku akiwaasa wananchi kuepuka na udanganyifu wowote unaotumia chapa hizi kuwatapeli Watanzania.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Madereva na wamiliki pikipiki mkoa wa Dar Es Salaam (CMPD), Michael Massawe amesema wamefurahishwa huduma hiyo kwani inakwenda kupunguza idadi ya uhalifu mitaani, kwa kuzalisha ajira nyingi zaidi.

Related Posts