Wakulima 15,000 kunufaika na huduma za ugani kidijitali

Dodoma. Jumla ya wakulima 15,000 katika mikoa ya Dodoma na Singida watanufaika na mfumo wa huduma za ugani kidijitali kwa ajili ya kuongeza tija kwenye kilimo.

Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Ugani wa Wizara ya Kilimo, Upendo Mndeme aliyezindua kuanza kazi kwa mfumo huo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli.

Mndeme ametaja changamoto kwenye matumizi ya akili bandia (artificial intelligence) na kuwataka wahusika kuwa makini na taarifa potofu kwa wakulima.

 “Kuna changamoto kwenye matumizi ya akili bandia, inawezekana mkulima akatuma swali si sahihi, kwa hali hiyo majibu atakayopata yatakuwa si sahihi na yeye bila kujua akayatumia na kuyasambaza kwa wenzake.”

“Au inawezekana mtu anayetoa majibu kwa mkulima akawa si mtaalamu wa kilimo na hivyo kumpa mkulima taarifa zisizo sahihi naye akizisambaza kwa wenzake kunaongeza shida kwa wakulima,” amesema Mndeme.

Ameshauri taarifa za wakulima ziwe zikihuishwa kila msimu, kwa sababu wakulima wanalima mazao kulingana na soko la wakati huo.

“Unaweza ukaona amejaza analima mahindi, lakini msimu mwingine akaona mahindi hayana soko akaamua kulima zao lingine, ni muhimu taarifa zikawa zinaboreshwa kila msimu,” amesema.

Akijibu hoja hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Biztech, Mahmaoud Shoo amesema taarifa zitakazopelekwa kwa wakulima zitakuwa zimeshirikisha wataalamu wa mamlaka husika za Serikali.

“Hatutapeleka taarifa kwa wakulima bila kushirikisha wataalamu. Pia, tutatoa elimu kwa wakulima ya namna ya kuweka taarifa zao sahihi na hasa mazao wanayolima na namna ya kuomba ushauri kidijitali,” amesema.

Shoo amesema kwenye kuhudumia wakulima hao 15,000 kwenye mikoa ya Singida na Dodoma watakuwa na watu maalumu kwa ajili ya kutoa elimu kwa wakulima.

Mkulima Lucy Milunga (30) anayetoka Kijiji cha Vililunze wilayani Chamwino alisema mfumo huo utawasaidia kuondokana na shida ya kuwasubiri kwa muda mrefu maofisa ugani.

Amesema mfumo utawaweza kupata taarifa mara moja kwa kuwa akifika shambani na kukuta tatizo anapiga picha na kutuma kwenye mfumo, ndani ya muda mchache anapata majibu ya kutatua changamoto yake.

Hata hivyo, Milunga ametahadharisha wahusika wa mfumo kuweka taarifa sahihi ambazo zitawasaidia wakulima badala ya kuwaongezea matatizo.

Pia, aliwataka wakulima wenzake kuweka taarifa sahihi wanapojisajili kwenye mfumo.

Katibu Tawala msaidizi sekta za uchumi na uzalishaji mkoani Singida, Stanslaus Choaji amesema mfumo huo ni utekelezaji wa programu ya kuendeleza sekta ya kilimo awamu ya Pili (ASDP II), unaofanywa na Serikali kwa kushirikisha sekta binafsi.

Amewataka wakulima kutulia maanani mfumo huo kwa sababu utawaweza kuwa na kilimo chenye tija.

Katibu Tawala msaidizi sekta za uchumi na uzalishaji Mkoa wa Dodoma, Aziza Mumba amesema mfumo huo unajibu changamoto za wakulima kuhusu taarifa za hali ya hewa na afya ya udongo.

Amesema kwa kutumia mfumo huo mkulima pia atakuwa na uwezo wa kupata soko la mazao yake kwa kutumia simujanja badala ya kupoteza muda mwingi wa kutafuta wateja.

Herman Bashiri, ambaye ni meneja wa maendeleo ya biashara wa taasisi inayosaidia kilimo ya Pass  amesema taasisi hiyo imekuwa ikitoa dhamana ya mikopo kwa wakulima kuanzia asilimia 20 hadi asilimia 60.

Amesema taasisi hiyo imekuwa ikitoa dhamana ya mikopo kwenye maeneo ya kilimo, mazao ya misitu, mifugo na ufugaji wa samaki.

Related Posts

en English sw Swahili