AKILI ZA KIJIWENI: Pamba mmerudi, ligi si kama mlivyoiacha

Wanetu wa Pamba FC aka Wana Kawekamo au ukipenda unaweza kuwaita TP Lindanda baada ya msoto wa muda mrefu hatimaye wamefanikiwa kupanda Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kushika nafasi ya pili kwenye Championship.

Jamaa zetu wamesota sana kwani mara ya mwisho kwao kucheza Ligi Kuu ilikuwa ni mwaka 2001 ambapo tangu waliposhuka hapo hawajaweza kupanda tena.

Kuna nyakati walikaribia kwa kucheza mechi za mchujo wakashindwa kufanya hivyo na muda mwingine tuliona wakishuka hadi Ligi Daraja la Pili ambayo sasa inaitwa First League.

Hivyo kitendo cha kurudi Ligi Kuu kimewafurahisha wengi ukizingatia kwamba timu hiyo ilijenga jina kubwa katika ramani ya soka nchini Tanzania na Afrika Mashariki na Kati.

Hata hivyo, suala la kupanda ni jambo moja na kulinda nafasi katika Ligi Kuu ni jambo jingine hivyo Pamba FC inapaswa kuwa na umakini wa hali ya juu katika daraja ambalo inakwenda kushiriki.

Maisha ambayo iliyaacha kwenye ligi mwaka 2001 wakati inashuka sio sawa na sasa hivyo inapaswa kujipanga vilivyo ili iweze kuendana na ushindani na maendeleo ambayo ligi yetu imekuwa nayo katika miaka ya hivi karibuni.

Inapaswa kuhakikisha ina kikosi cha wachezaji bora na ambao wana uwezo mkubwa kiushindani ambao wataweza kukabiliana na wale wa timu mbalimbali ambao tunawashuhudia kwenye ligi yetu.

Wanatakiwa kuepuka kuingiza maslahi ya timu nyingine kwenye timu yao ili kuepuka mpasuko na migogoro ambayo inaweza kusababisha timu ikayumbayumba na kurudi kule ilikotoka.

Yapo mengi ya kuwashauri lakini binafsi nimeona niwape hayo mawili hapo juu ambayo ni muhimu kabisa.

Related Posts