Dar es Salaam. Baada ya mfululizo wa mvua kwa takriban miezi saba, baadhi ya mikoa nchini inatarajiwa kukumbwa na kimbunga Hidaya kwa siku tano mfululizo.
Iwapo hali hiyo itajitokeza, itakuwa mara ya tatu kwa Tanzania kukumbwa na kimbunga tangu nchi ikiwa chini ya mkoloni, kama ilivyoelezwa na Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk Ladislaus Chang’a.
Kwa mujibu wa Chang’a, kimbunga kama hicho kiliwahi kutokea mwaka 1952 mkoani Lindi, wakati huo Tanzania ikiitwa Tanganyika na kingine kilitokea miaka ya 1800.
Kutokana na matarajio ya uwepo wa kimbunga hicho, wataalamu wanapendekeza iwapo nyumba zilizopo maeneo yatakayoathiriwa si imara, ni vema wakazi wake wakahama kwa muda, huku wakisisitiza baadhi ya shughuli kusimama.
Taarifa kuhusu matarajio ya kimbunga Hidaya zimetolewa leo Mei 2, 2024 na TMA, ikieleza kitakuwa na nguvu ya kati na umbali wa kilomita 506 Mashariki mwa Pwani ya Mtwara.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mwenendo wa mfumo wa hali ya hewa baharini unaonyesha uwezekano wa kimbunga hicho kusogea karibu na Pwani ya Tanzania kuanzia usiku wa Mei 2, 2024 na kuendelea hadi Mei 6, 2024.
Uwepo wa kimbunga hicho, TMA inasema utaathiri mifumo ya hali ya hewa na kusababisha vipindi vya mvua kubwa na upepo mkali katika mikoa kadhaa.
TMA inataja mikoa hiyo ni Mtwara, Lindi, Pwani, Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, na Visiwa vya Unguja na Pemba. Pia maeneo mengine ya jirani.
Kutokana na hali hiyo, mamlaka hiyo imeshauri wananchi wa mikoa husika na wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali baharini, kuchukua tahadhari na kufuatilia taarifa za TMA.
“Pia, wanapaswa kupata ushauri na miongozo ya wataalamu wa sekta husika, ili kujikinga na athari tarajiwa,” imeeleza taarifa hiyo.
TMA imesema kutokea kimbunga hicho kunatokana na kuimarika kwa mgandamizo mdogo wa hewa, ambao iliuripoti Mei 1, 2024.
Kama nyumba si imara ondoka
Mwanazuoni wa Chuo Kikuu Mzumbe mkoani Morogoro, Profesa William Mwegoha amesema katika hali kama hiyo yeyote mwenye makazi anayodhani si stahimilivu ni vema ahame kuepuka athari.
Amesema kimbunga kama hicho kinachoambatana na mvua kubwa huwa hatari kwa uharibifu wa majengo.
Hatari zaidi, amesema inatokea pale nyumba iliyopo katika eneo litakaloathiriwa ama imechoka au haina uimara wa kustahimili upepo na mvua kubwa.
“Mvua inalegeza udongo, upepo unasukuma nyumba, ni vitu ambavyo vikishirikiana kama nyumba si imara dakika chache inaanguka, kwa hiyo ni vema kuondoka,” amesema.
Kama kitatokea bila mvua kubwa, Profesa Mwegoha ameshauri wananchi wa maeneo yatakayoathiriwa wasitishe shughuli zao za siku zote, badala yake watulie nyumbani.
Muhimu zaidi kwa mujibu wa Profesa Mwegoha aliyebobea katika taaluma ya mazingira, ni kufuatilia taarifa za mamlaka mbalimbali ili kujua uelekeo na mwenendo wa kimbunga hicho.
“Ukifuatilia taarifa utajua wakati gani kinatarajiwa kutokea na eneo litakaloathirika zaidi na kuhakikisha maeneo hatarishi sana, watu watulie maeneo waliyopo, au kama kuondoka basi waondoke haraka,” ameeleza.
Akifafanua, Dk Chang’a amesema watumiaji wa bahari wanapaswa kuchukua tahadhari kwa sababu upepo mkali na mvua kubwa inatarajiwa kunyesha.
Alieleza athari pia zitarajiwe hata katika maeneo ambayo hayakubainishwa kwa kile alichofafanua kutokea kwa kimbunga huathiri mifumo ya hali ya hewa, hivyo kusababisha athari kusambaa.
“Kwa sababu kimbunga kinavyotokea unaweza kukuta ukanda wa Ziwa Victoria nao ukaathirika kutokana na mifumo ya hali ya hewa kuathiriwa,” amesema.
Katika hali kama hiyo, amesema TMA inafanya ufuatiliaji wa mara kwa mara kwa saa 24 na itakapoonekana haja ya kutoa taarifa watafanya hivyo.
Amewasihi wananchi kuendelea kufuatilia taarifa hizo ili kujiepusha na athari.
Pamoja na yote, amesisitiza wananchi wasiwe na taharuki, badala yake waendelee kutekeleza maelekezo ya kitaalamu kama wanavyoshauriwa.
Kwa siku kadhaa TMA imekuwa ikitoa tahadhari ya hali ya upepo mkali iliyoelezwa huenda ikasababisha mvua kuanzia Mei 4 hadi 7, 2024 kwenye mikoa ya Pwani ya Kusini.
TMA ilisema upepo mkali unaoendelea katika maeneo mengi nchini umesababishwa na kuimarika kwa migandamizo mikubwa ya hewa iliyopo katika ncha ya Kusini mwa Bara la Afrika ambayo kukoma kwake ndiko kunawezesha mifumo iliyokuwa inaleta mvua kuimarika.
“Hali ya upepo mkali inaenda kukoma ndani ya siku tatu zijazo (kuanzia leo Aprili 29 hadi Mei Mosi) na ndiyo itasababisha mvua kurudi kwenye maeneo ya Pwani ya Kusini kuanzia Mei 4 hadi 7,” alisema Meneja wa Utabiri wa TMA, Dk Mafuru Kantamla.
Alisema mifumo inaonyesha dalili za mvua kwenye Pwani ya Kusini inayohusisha mikoa ya Lindi, Mtwara, Dar es Salaam na Pwani ambayo ipo jirani na Bahari ya Hindi.
Mvua za El Nino zilizonyesha nchini zimesababisha mafuriko katika mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Morogoro, Pwani na maeneo mengine.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa bungeni Dodoma, Aprili 25, 2024 alielezea changamoto za hali ya hewa na kubainisha mafuriko na maporomoko ya udongo katika maeneo mbalimbali nchini yaliyosababisha athari kubwa.
Alizitaja athari hizo kuwa ni pamoja na vifo, uharibifu wa mazao, makazi, mali za wananchi, miundombinu kama vile barabara, madaraja na reli, huku zaidi ya kaya 51,000 na watu 200,000 waliathirika.
Watu 155 walifariki dunia na wengine 236 kujeruhiwa kutokana na madhara ya mvua.
Nyumba zaidi ya 10,000 ziliathirika kwa viwango tofauti, miundombinu ya shule, zahanati, nyumba za ibada, barabara, madaraja, mifugo na mashamba yenye mazao mbalimbali ziliathirika.