MKUU wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo amewaonya viongozi wa serikali za vijiji na mitaa mkoani humo, kutowauzia wananchi na wageni vitambulisho vya uraia (NIDA) kwani watakaobainika kuchukuliwa hatua kali. Anaripoti Ibrahim Yassin, Songwe… (endelea).
Akizungumza jana Jumatano na wananchi wa kijiji cha Itale kata ya Itale, Chongolo amesema kutokana na mkoa huo kupakana na nchi mbili Zambia na Malawi viongozi hao wanatakiwa kujiepusha na tamaa ya kuwauzia wananchi vitambulisho vilivyotolewa bure na serikali.
Chongolo amesema mkoa huo umepokea vitambilisho 365,000 ambavyo vitagawiwa bure kwa wananchi waliojiandikisha hivyo kiongozi atakayebainika kuwatoza wananchi kwa gharama yoyote atashughulikiwa.
Amewaonya viongozi hao kuacha tabia ya kuwapa vibali wananchi kutoka nchi jirani kwa lengo la kupata vitambulisho vya uraia kwani inahatarisha usalama wa nchi pamoja na kupunja keki ya watanzania ikiwepo upatikanaji wa mbolea ya ruzuku.
“Acheni kuwaruhusu wananchi wasio raia wa Tanzania kuwapa vibali vya uraia sambamba na kuwapa upenyo wahamiaji haramu kupata utambulisho hivyo tukikukamata utawajibika kwa mujibu wa sheria,” amesema Chongolo.
Amewataka watumishi wa Nida kwenda vijijini kuwasajili wananchi ambao hawana vitambulisho kwani zoezi hili bado ni endelevu nchini na kuacha kutoa barua za kuwaruhusu wananchi kutoka nchi jirani kujiandikisha kupata vitambulisho vya uraia.
“Wananchi wote waliosajiliwa na ambao hawajasajiliwa wanahaki ya kupata vitambulisho ili kuwarahisishia kupata huduma za jamii ambazo zinahitaji kuhudumiwa kwa kutumiwa vitambulisho hivyo,” amesema Chongolo
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Ileje, Faida Mgomi amesema watahakikisha wanawadhibiti na kuwachukia hatua viongozi watakaobainika wanauza vitambulisho hivyo.