Simba imeanza maisha mapya baada ya kocha Abdelhak Benchikha kuondoka kwa ilichoelezwa kuwa ni matatizo ya kifamilia na timu kukabidhiwa kwa Juma Mgunda na Selemani Matola, uamuzi ambao kwa hakika umewapa matumaini makubwa mashabiki kutokana na rekodi za kocha huyo mzawa aliyejipatia sifa kama “mzee wa acha boli litembee.”
Mgunda amerejea kikosini kama kaimu kocha mkuu, wadhifa ambao aliwahi kuushika kabla ya ujio wa kocha Mbrazili Roberto Oliveira ‘Robertinho’, ambaye naye alifutwa kazi baada ya Simba kufungwa mabao 5-1 na Yanga katika Kariakoo Dabi ya Novemba 5, 2023.
Baada ya Robertinho kufutwa kazi ndio akatua Benchikha, ambaye naye ameondoka ghafla. Kuna nini Simba? Kuna mambo mengi yanayoizunguka timu hiyo ya Msimbazi kwa sasa ambayo mengi tumeyaeleza hapa katika makala zetu zilizotangulia, lakini moja kubwa zaidi tunalosisitiza ni la timu kushindwa kumalizia nafasi nyingi inazotengeneza.
Simba ilishika nafasi ya pili kwa kutengeneza nafasi nyingi za hatari (19) katika Ligi ya Mabingwa Afrika nyuma ya vinara na mabingwa watetezi Al Ahly ya Misri waliotengeneza nafasi 25. Yanga ilishika nafasi ya saba kwa kutengeneza nafasi 13 za hatari.
Kiungo wa Simba, Clatous Chama ndiye aliyeongoza kwa kutengeneza nafasi nyingi kubwa za hatari (5), akilingana na Stephane Aziz Ki wa Yanga miongoni mwa mastaa wote waliocheza Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu ukijumuisha wa klabu zote — iwe Al Ahly, Mamelodi Sundowns na kila klabu iliyoshiriki.
Kuna ushahidi mwingi kwambwa Simba imetawala asilimia kubwa ya mechi ilizocheza kwa kupiga mashuti mengi zaidi, yaliyolenga lango mengi zaidi, kona nyingi zaidi na kadhalika na bado ikakosa matokeo chanya ikithibitisha tatizo ni umaliziaji.
Iliipigia Al Ahly mashuti 19 Kwa Mkapa huku saba yakilenga lango na kutawala umiliki kwa asilimia 62 kwa 38 za mabingwa hao wa Afrika, ambao walipiga mashuti matano tu, manne yakienda nje ya lango na moja pekee lililolenga lango likawa bao lililoizamisha Simba 1-0 katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa. Simba ikatawala umiliki wa mpira tena kule Cairo katika mechi ya marudiano lakini ikalala 2-0.
Katika Dabi ya Kariakoo ya mzunguko wa pili, Simba ilipiga mashuti 10 dhidi ya mashuti 7 ya Yanga, huku kila timu mashuti yake manne yakilenga lango. Bado ni Yanga iliyoshinda mechi hiyo kwa 2-1. Hili ni tatizo kubwa ambalo linapaswa kufanyiwa kazi Simba.
Na ndio maana ujio wa Mgunda unawapa matumaini sana Wanamsimbazi kwa sababu ya rekodi ya kocha huyo ambaye enzi zake akicheza soka la ushindani alikuwa mshambuliaji, wakitumai anaweza kuimarisha sehemu ambayo ina shida na anaifahamu vyema kwa sababu yeye alikuwa mdunguaji.
Baada ya kurithi mikoba ya Benchikha, Mgunda ameanza na sare ya kufungana mabao 2-2 na Namungo katika mechi ya Ligi Kuu Bara juzi.
Mchezo huo ni wa kwanza kwa Mgunda tangu arejee, lakini ni wa 17 kwake katika Ligi Kuu Bara ukijumuisha na aliyoiongoza timu hiyo kabla ya kurithiwa na Robertinho ambapo kati ya hiyo ameshinda 11, sare mitano na kupoteza mmoja tu huku timu hiyo ikifunga jumla ya mabao 41 na kuruhusu nyavu zake kutikishwa mara 10.
Rekodi hii ya mabao inaleta mzuka wa aina yake Simba kwa sababu chini yake timu ilikuwa ikifunga mabao na ilikuwa ikijilinda vyema, tofauti na hii Simba ya Robertinho na Benchikha kwa pamoja ambayo katika mechi 21 za ligi msimu huu imefunga mabao 41 na kuruhusu mabao 23.
Mabao 41 yaliyofungwa chini ya Mgunda, yalikuwa na mgawanyiko mzuri katika kila eneo ambapo wachezaji wa safu ya ushambuliaji walifunga mabao 19, viungo mabao 18 huku mabeki wa kikosi hicho wakifunga manne.
Kiungo mwenye mabao mengi wakati wa utawala wa Mgunda ni Pape Sakho aliyeondoka kikosini humo ambaye ana mabao matano akifuatiwa na Mghana, Augustine Okrah aliyepo Yanga msimu huu ambaye alifunga matatu sawa na Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’.
Kwa upande wa washambuliaji anayeongoza ni John Bocco aliyefunga mabao tisa ikiwemo ‘hat-trick’ mbili alizofunga akianza na ya ushindi wa 4-0, dhidi ya Ruvu Shooting (Novemba 19, 2022) na 7-1 mbele ya Tanzania Prisons Desemba 12, 2022.
Nyota mwingine anayefuatia kwa kufunga mabao mengi tofauti na Bocco ni Mzambia, Moses Phiri aliyeondoka ambaye alifunga mabao saba.
Mabao manne yaliyofungwa na mabeki chini ya uongozi wa Mgunda ni ya Shomari Kapombe na Henock Inonga ambao kila mmoja wao amefunga mawili.
Ushindi mkubwa Mgunda alioupata akiwa na Simba ni wa mabao 7-1, dhidi ya Tanzania Prisons Desemba 12, 2022, yaliyofungwa na John Bocco na Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’ waliofunga matatu kila mmoja wao yaani ‘hat-trick’ na beki, Shomari Kapombe.
Mgunda amerejea kwa mara ya pili ndani ya timu hiyo baada ya awali kuteuliwa Septemba 7, 2020 akichukua nafasi ya kocha, Zoran Manojlovic Maki aliyedumu kwa miezi miwili tu tangu alipoteuliwa Juni 28, 2022 akirithi mikoba ya Mhispania, Pablo Franco.
Mgunda anayesimamia kikosi hicho kwa sasa akiwa na Selemani Matola ndiye aliyeandika rekodi ya kocha mzawa kuipeleka timu hiyo makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika tangu mara ya mwisho alipofanya hivyo, Tito Mwaluvanda akiwa na Yanga 1998.
Akizungumzia hilo, Mgunda aliwahi kukaririwa akieleza sababu kubwa ya upatikanaji wa mabao katika maeneo tofauti ni kutokana na kutoa uhuru kwa kila mchezaji kwani anaamini suala la kufunga mabao sio la washambuliaji pekee uwanjani.
“Huwezi kupata nafasi ukaacha kufunga kwa sababu washambuliaji ndio kazi yao, naamini katika ushirikiano wa mchezaji na mchezaji kwani hiyo ndio silaha ya kufanya kitu kilichokuwa bora zaidi kwa manufaa yetu ya timu kwa kiujumla,” alisema.
Kwa takwimu za Mgunda, na tatizo sugu la umaliziaji lililopo Simba, mashabiki wana kila sababu ya kupata matumaini anaporejea kocha huyu mzawa.