Dar es Salaam. Serikali imesema marekebisho ya kanuni za Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) yatafanyika kuiweka sukari kuwa sehemu ya usalama wa chakula.
Mbali na hilo, yatafanyika marekebisho ya Sheria ya Sukari Na.6 ya mwaka 2001 kwenye sheria ya fedha ya mwaka 2024 kwa ajili ya kuiwezesha NFRA kununua na kuhifadhi sukari kwenye Hifadhi ya Chakula ya Taifa ili kunusuru hali ya upatikanaji wake inapotokea kudorora kwa soko la bidhaa hiyo.
Hayo yamo katika hotuba ya Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya wizara hiyo kwa mwaka 2024/2025 aliyowasilisha bungeni leo Mei 2, 2024.
Amesema hatua hiyo inalenga kuondoa uhodhi kwa baadhi ya wenye viwanda, bila kuathiri dhamira ya Serikali ya kulinda viwanda vya ndani.
“Serikali itaendelea kuvilinda viwanda vya ndani na kuwalinda wakulima wa miwa lakini ulinzi huo hautakuwa kwa gharama ya kuwatesa Watanzania milioni 61.7,” amesema.
Kupitia Bunge, Bashe amewaeleza wamiliki wa viwanda nchini kuwa sukari ni chakula cha Watanzania masikini na ni suala la usalama wa nchi.
“Hivyo, Serikali haitavumilia wala haitaruhusu tena tatizo lililotokea kujirudia, ni wajibu wetu kuvilinda viwanda vya ndani lakini ni wajibu wetu pia kuwalinda Watanzania na usalama wa nchi,” amesema.
Pia amewataka wenye viwanda wafanye mabadiliko ya chama chao cha wazalishaji (Tanzania Sugar Producers Associations) ili kuhakikisha umoja huo unakuwa na uwakilishi wa wazalishaji wakubwa na wadogo kama ambavyo Serikali inawaelekeza.
Bashe amesema wakati wa utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2023/2024 Serikali ilikabiliwa na tatizo la upungufu wa sukari kutokana na mvua za EL-Nino na tabia za wafanyabiashara kutengeneza uhaba wa sukari kwa kutokuingiza sukari ya kuziba pengo kulingana na vibali vya uagizaji walivyopatiwa, hivyo kupandisha bei ya sukari.
Amesema kiasi cha sukari walichoingiza nchini hawakukisambaza kama ilivyokusudiwa ili kutatua changamoto ya upatikanaji wa bidhaa hiyo.
Hali hiyo, amesema ilisababisha kupanda bei na hadi Januari 22, 2024 wastani wa bei ya jumla kwa wazalishaji wakubwa ilikuwa ni kati ya Sh3, 800 na Sh4,000.
Kwa wauzaji wa jumla kati ya Sh4,500 na Sh5,000 na bei ya rejareja kati ya Sh6,000 na Sh10,000 kwa kilo moja katika maeneo mengi, hali ambayo ilikuwa inahatarisha usalama wa nchi na uchumi.
Amesema ili kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa sukari, Wizara ya Kilimo ilitangaza bei elekezi ya sukari nchi nzima kupitia Gazeti la Serikali Na. 3. Toleo la 105 la Januari 23, 2024.
Bei elekezi iliyotangazwa ni kati ya Sh2,600 na Sh2,900 kwa jumla na kati ya Sh2,700 na Sh3,200 kwa rejareja.
Kupitia NFRA amesema wizara ilitoa idhini ya uingizaji wa tani 410,000 za sukari ulioanza Januari 2024 na utakamilika Desemba 2024.
“Uingizaji wa sukari utaratibiwa na Serikali kwa kuzingatia ugavi na mahitaji na uwezo wa viwanda vya sukari kurudi
katika uzalishaji,” amesema.