Mahakama ya UN yatoa hati ya kukamatwa rais wa zamani wa Jamhuri ya Afrika ya Kati

Mahakama Maalumu ya Jinai (CPS) inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa imesema, imetoa hati ya kukamatwa Rais wa zamani wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Francois Bozize kwa tuhuma za kuhusika na uhalifu dhidi ya binadamu unaodaiwa kufanywa na jeshi wakati wa uongozi wake.

Taarifa iliyotolewa na mahakama hiyo yenye makao yake mjini Bangui imebainisha kuwa, uhalifu unaodaiwa kufanywa ni pamoja na mauaji, kutoweka kwa kulazimshwa, utesaji, ubakaji na vitendo vingine visivyo vya kibinadamu, vilivyofanywa kati ya mwaka 2009 na 2013.

Uhalifu huo inasemekana ulifanywa na walinzi wa rais wa Bozize na vikosi vingine katika gereza la kiraia na katika kituo cha mafunzo ya kijeshi katika mji wa Bossembele.

Majaji wa CPS wamesema, kutokana na ushahidi mkubwa na madhubuti uliopo dhidi ya Bozize kuna uwezekano wa kumbebesha dhima ya kutenda jinai katika nafasi yake kama kiongozi wa ngazi ya juu na kiongozi wa kijeshi.

Kwa mujibu wa mahakama hiyo, waranti huo wa kimataifa dhidi ya Bozize ulitolewa tangu Februari 27, lakini uliwekwa hadharani jana Jumanne.

Bozize mwenye umri wa 77, alitawala Jamhuri ya Afrika ya Kati kuanzia Machi 2003 hadi Machi 2013 alipopinduliwa. Alinyakua madaraka pia kupitia mapinduzi ya kijeshi, na anaishi uhamishoni nchini Guinea-Bissau tangu Machi 2023.

Mahakama ya CPS imeitaka Guinea-Bissau kutoa ushirikiano wa kumkamata na kumkabidhi mtuhumiwa huyo.

Related Posts