Arusha. Mratibu wa Mpango wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) katika Halmashauri ya Jiji la Arusha, Amani Mlay na wenzake wawili wamepandishwa kizimbani wakikabiliwa na makosa tisa likiwamo la matumizi mabaya ya nyaraka kwa nia ya kumdanganywa mwajiri, wizi na kusaidia kufanyika uhalifu.
Watuhumiwa hao wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Arusha leo Alhamisi Mei 2, 2024, mbele ya Hakimu Mkazi, Devotha Msoffe wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi.
Mbali na Mlay, wengine waliofikishwa mahakamani hapo ni Cecilia Zumba na Gerson Mollel.
Awali kabla ya kuwasomea makosa hayo, Wakili kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini Tanzania (Takukuru), Sifaeli Mshana aliieleza kuwa shauri hilo limefikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza, lakini bado hawajapata kibali cha Mkurugenzi Mkuu wa Mashitaka nchini (DPP) cha kuipa mahakama hiyo mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo.
Akisomea mashitaka ya kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 11512/2024, Mshana amedai kosa la kwanza linalomkabili Mlay ni la matumizi mabaya ya nyaraka ambazo alilenga kumdanganya mwajiri wake na kosa hilo amedai kuwa Mlayi alilitenda Mei 25, 2023.
Amedai kuwa, Mlay akiwa Mratibu wa Tasaf wa Jiji la Arusha kwa nia ya kumdanganya mwajiri, alitumia nyaraka iliyokuwa na kichwa cha habari ‘Barua ya ombi la Sh64.2 milioni kwa ajili ya manunuzi ya vifaa vya umaliziaji ujenzi wa uzio wa Shule ya Msingi Shangarao, mtaa wa Shangao Kata ya Moivaro.’
Kosa la pili ni la matumizi ya nyaraka kwa nia ya kumdanganya mwajiri, anadaiwa akiwa Mratibu wa Tasaf, Mei 25, 2023 alitumia nyaraka “delivery note”, yenye namba 0133 ambayo maelezo yake ni ya uongo, ikionyesha kuwa kampuni ya Cecy Electro Plumbing amewasilisha kwenye menejimenti ya kamati hiyo vifaa vya ujenzi.
Ametaja vifaa hivyo kuwa ni nondo 500 zenye ukubwa wa milimita 12, nondo 500 za mililita nane, awamu saba za kokoto, awamu sita za mchanga, awamu 20 za kwarukwaru, mifuko 350 ya saruji, matofali 4,000, pisi 41 za mbao, mabeleshi matatu na toroli moja, kwa lengo la kumdanganya mwajiri.
Ametaja kosa la tatu ni la matumizi mabaya ya nyaraka akilenga kumdaganya mwajiri, anadaiwa Mei 25, 2023 alitumia nyaraka ‘invoice’ namba 0136 iliyokuwa na maelezo ya uongo ikionesha kampuni ya Cecy Electro Plumbing anadai Sh64.2 milioni kwa ajili ya umaliziaji wa ujenzi wa uzio wa Shule ya Msingi Shangarao, Mtaa wa Moivo Kati.
“Kosa la nne, ni matumizi mabaya ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri wake inayoonesha Mei 24, 2024 aliwasilisha nyaraka ya kuonyesha muktasari wa kikao cha kamati ya usimamizi wa mradi wa umaliziaji uzio wa Shule ya Msingi Shangarao kilichofanyika tarehe hiyo kikionyesha kumpa mkandarasi huyo zabuni ya mradi huo,” amedai wakili huyo.
Pia, ametaja kosa la tano linalomkabili mshitakiwa wa pili, Cecilia ni kusaidia kutenda uhalifu. Anadai kati ya Mei Mosi 2023 hadi Desemba 31,2023 alimsaidia Mlay kutumia nyaraka kwa nia ya kumdanganya mwajiri, ambaye alimpatia nyaraka ambayo haijajazwa kitu akimsaidia kutenda uhalifu.
Kosa lingine la sita linalomkabili Cecy ni kusaidia kufanya uhalifu, anadaiwa kati ya Mei Mosi 2023 na Desemba 31,2023, alimsaidia Mlay kufanya kosa kwa kutumia nyaraka kwa nia ya kumdanganya mwajiri wake, alimpa nyaraka ambayo haijajazwa (invoice) ya kampuni ya Cecy Electro Plumbing iliyomsaidia kumdanganya mwajiri wake.
Kwa upande wake mshtakiwa Mollel anadaiwa kutekeleza kosa la saba la kusaidia kufanya uhalifu. Anadaiwa kati ya Mei Mosi 2023 hadi Desemba 31, 2023 alimsaidia Mlay kutumia nyaraka kumdanganya mwajiri kwa kusaini kama mwenyekiti nyaraka ya muhtasari wa kikao cha kamati ya usimamizi wa mradi wa umaliziaji uzio wa Shule ya Msingi Shangarao kilichofanyika Mei 24, 2023.
Wakili huyo ameieleza mahakama kuwa kosa la nane la wizi linawakabili watuhumiwa wote, wanadaiwa kati ya Mei Mosi 2023 hadi Desemba 31, 2023, waliiba Sh62.9 milioni mali ya Halmashauri ya Jiji la Arusha.
Hali kadhalika wakili huyo amedai kosa la tisa linawakabili watuhumiwa wote. Amedai kuwa watuhumiwa wameisababishia mamlaka hasara.
Amedai kati ya kipindi tajwa hapo juu, washtakiwa walishindwa kuchukua hatua stahiki na kusababisha Jiji la Arusha lipate hasara ya Sh62.9 milioni.
Baada ya kusomewa makosa hayo, Hakimu Devotha aliwataka watuhumiwa hao kutojibu chochote hadi mahakama hiyo itakapopata kibali cha kusikiliza kesi hiyo.
Wakili George Njooka anayemtetea Mollel katika kesi hiyo aliomba shauri hilo lipangiwe tarehe ya karibu kwa sababu anaendelea kukamilisha taratibu za kukidhi masharti ya dhamana.
Hakimu Msofe aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 6, 2024 itakapotajwa tena.