Mwanamke Rwanda ataka kupambana tena na Kagame

KIONGOZI wa kihistoria wa upinzani nchini Rwanda, Victoire Ingabire Umuhoza, amefungua kesi katika Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) akitaka arejeshewe haki zake za kiraia, ikiwa ni pamoja na haki ya kugombea katika uchaguzi ujao. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa … (endelea).

Victoire Ingabire Umuhoza alifungua kesi hiyo mapema wiki hii. Anapinga serikali ya Rwanda kukataa kurejesha haki zake za kiraia.

Machi 2024, Mahakama Kuu ya Rwanda, katika hatua tata mahakama ilikataa ombi la Ingabire Umuhoza la kurekebishiwa madai yake.

Rais Paul Kagame

Mawakili wake wamesema, “hivyo mahakama ilimzuia kupata haki yake ya kiraia, ikiwa ni pamoja na haki ya kusafiri nje ya Rwanda na kushiriki katika uchaguzi wowote nchini Rwanda.”

Ingabire Umuhoza anawakilishwa na timu ya wanasheria wa kimataifa, ikiwa ni pamoja na wakili mashuhuri wa Rwanda, Gatera Gashabana, pamoja na wanasheria wa Kenya na Ulaya.

Uamuzi wa Mahakama Kuu unawakilisha “kipindi cha hivi karibuni zaidi katika mfululizo wa juhudi za kimfumo za Rwanda kumzuia Ingabire Umuhoza kushiriki, kwa vyovyote vile, katika maisha ya kisiasa ya Rwanda”, waliongeza.

Siku chache kabla ya kufungua kesi Ingabire aliliambia Shirika la Habari la Ufaransa Idhaa ya Kiingereza (RFI), “Nataka kupata haki zangu za kiraia. Chama changu hakiwezi kusajiliwa. Wanachama watatu wameuawa. Wanne wamepotea. Na tisa wako gerezani. Hakuna nafasi kwa upinzani nchini Rwanda.”

Akiwa na umri wa miaka 66, Rais wa Rwanda, Paul Kagame, afisa wa zamani wa kijeshi na waasi wa Kitutsi, atagombea nafasi ya urais kwa mara ya tano, baada ya kuwa mkuu wa nchi tangu 2000.

Ingabire aliondoka Rwanda Machi 1994 kwenda kusoma na kuishi Uholanzi, ambapo aliolewa baadaye.

Alianzisha chama cha siasa mwaka 2006 kisha akarejea Rwanda Januari 2010, baada ya miaka mingi ya uhamishoni, ili kushiriki katika uchaguzi wa Rais uliopangwa kufanyika baadaye mwaka huo.

Badala yake, alikamatwa na kuhukumiwa kifungo cha miaka 15 jela. Kesi yake ililaaniwa na mataifa mbalimbali kuwa ilichochewa kisiasa.

Alikata rufaa mbele ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu ambayo iliamua kwamba Serikali ya Rwanda ilikiuka haki zake za uhuru wa kujieleza na kujitetea.

Septemba 2018, Ingabire Umuhoza aliachiliwa huru kufuatia msamaha wa Rais, baada ya kutumikia kifungo cha miaka minane gerezani, mitano kati yake alikaa katika kifungo cha upweke.

Uamuzi huo unakiuka wajibu wa Rwanda chini ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, unaoitaka Rwanda kutii kanuni za msingi za demokrasia, utawala wa sheria na haki za binadamu.

Ukosefu wa demokrasia

Madai ya Ingabire Umuhoza mbele ya EACJ pia yanajumuisha maombi mengine ya kuondoa vikwazo vinavyomzuia kuondoka Rwanda.

Anatarajia kuhudhuria harusi ya mwanawe, kuzaliwa kwa mjukuu wake, au kumtembelea mume wake aliye mgonjwa sana huko Uholanzi.

Kimsingi inawasilisha “ombi la dharura la hatua za muda”, ili kuzuia “madhara yasiyoweza kurekebishwa yatakayosababishwa na hatua ya kumzuia kujiandikisha kama mgombea wa urais” kulingana na ratiba ya uchaguzi wa Urais uliopangwa kufanyika tarehe 15 Julai 2024.

“Paul Kagame ana nguvu zote mikononi mwake nchini Rwanda,” aliiambia RFI. “Idara ya haki haiko huru, wala Bunge na ni ikulu pekee ndio inaongoza nchi. Hii ni kidemokrasia ya wapi? Kagame alikuwa kiongozi wa Rwanda aliyehitajika baada ya mauaji ya kimbari, alirudisha utaratibu. Lakini sasa idadi ya watu imebadilika, ni ya vijana zaidi, na inahitaji aina tofauti ya uongozi”.

Related Posts