Achana na shangwe la kupanda Ligi Kuu Bara linaloendelea jijini hapa, mabosi wa Pamba Jiji tayari wameshapata pa kuanzia wakati wakipiga hesabu za mambo watakayoanza nayo msimu ujao.
Pamba Jiji imerejea Ligi Kuu mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kumaliza katika nafasi ya pili kwenye Ligi ya Championship ikivuna pointi 67 katika mechi 30, nyuma ya vinara na mabingwa, Ken Gold waliomaliza na alama 70.
Mjumbe wa bodi ya Pamba Jiji, Evarist Hagila, alisema mafanikio ya msimu huu ni matunda ya kazi kubwa waliyoifanya misimu minne iliyopita akiwa mwenyekiti wa klabu hiyo.
“Niwaahidi mashabiki na wadau wa soka tutatengeneza timu ya kiwango chenye hadhi ya Ligi Kuu, tuliihitaji Pamba Jiji na sasa tumeipata hivyo tuunganishe nguvu ya pamoja,” alisema Hagila ambaye ana uzoefu wa Ligi Kuu akiwa miongoni mwa vigogo wa Simba.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, alisema pia mipango yao ya muda mfupi ni kuutumia Uwanja wa Nyamagana kwa mechi zao za nyumbani isipokuwa dhidi ya Simba na Yanga.
Mtanda aliuagiza uongozi wa Halmashauri ya jiji hilo kuukarabati uwanja huo kwa kuongeza majukwaa likiwamo jukwaa kuu litakalopewa jina la Amos Makalla na kufunga taa ili mechi za usiku zichezwe uwanjani hapo.
“Malengo yetu mengine ni kununua basi kubwa la timu, hili la sasa litatumiwa na mashabiki, pia tutajenga hosteli za kisasa za timu ambazo wachezaji watakaa ili timu iishi maeneo bora na yenye hadhi ya jiji la Mwanza,” alisema Mtanda.
Mtanda ambaye ni mlezi wa timu hiyo, alisema watapambana kuepuka siasa za Simba na Yanga kwenye klabu hiyo ili zisiwagharimu na yeyote atakayeleta Usimba na Uyanga ndani ya Pamba ataondolewa.
“Timu itaendeshwa kisasa na kitaalam kwa kufuata miongozo ya soka, sisi (wanasiasa) kazi yetu ni kuja kuuliza na kuombwa ushauri tunataka timu iwe huru menejimenti ijiendeshe, kazi ya usimamizi na uendeshaji siyo ya Mkuu wa Mkoa,” alisema Mtanda.