Dar es Salaam. Miongoni mwa mambo yanayojitokeza kwa baadhi ya wajawazito katika kipindi cha miezi minne mpaka tisa, ni kuvimba pua, uso na wengine miguu.
Catherine Malya ni miongoni mwa wanawake waliobadilika mwonekano katika kipindi cha ujauzito wake.
“Nilivimba mwili mzima, pua ilikuwa kubwa, mdomo na uso vyote vilivimba, nilibadilika sana. Kitu pekee mume wangu alinisihi nisiwaze kuhusu hali hiyo, alinipa ujasiri sana,” anasema Catherine, mkazi wa Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam.
Anasema watu wanaomzunguka mjamzito wana nafasi kubwa ya kumsaidia na kumtia moyo, lakini pia alimtafutia mtaalamu wa afya kwa matibabu zaidi.
Simulizi hii inafanana na ile iliyoandikwa Desemba 16, 2022, mwanadada kutoka Uganda, Heyosato aliyeweka mitandaoni picha yake iliyoonesha mabadiliko ya mwili wake yaliyosababishwa na ujauzito wake.
Picha hiyo ilisambaa kwa kasi mitandaoni na ndani ya muda mfupi, wanawake kutoka mataifa mbalimbali walitoa shuhuda zao namna walivyobadilika baada ya kupata ujauzito na ilifikisha wafuatiliaji milioni 7.3 kwa saa chache.
Hata hivyo, wataalamu wa afya ya mama na mtoto wanasema changamoto kama hii huwakumba wanawake wengi na ni dalili ya changamoto kadhaa, ikiwemo matatizo ya figo na kifafa cha mimba vinavyoweza kumkuta mjamzito.
Daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama na uzazi, Isaya Mhando anasema mara nyingi hali kama hii inaweza kuwa ya kawaida kwa mjamzito kumkuta.
Anasema mjamzito anapobeba mimba ili mtoto aweze kulishwa vizuri kwenye mji wa mimba, lazima presha ya damu inayopita kule iwe ndogo ya chini, ili kuruhusu virutubisho vya chakula na oksijeni kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kwa urahisi.
Dk Mhando anasema maji yanayotengeneza damu huongezeka kwa asilimia 30 hadi 50, hiyo ndiyo huitwa hali ya kawaida ya ujauzito. Na wajawazito hawa huvimba miguu, uso na wakati mwingine pua au mdomo.
“Kuna ule uvimbe wa kutisha, lakini wengine wanavimba kidogo miguuni. Lakini uvimbe unaotokana na ugonjwa mara nyingi hutokana na shinikizo la damu linalosabishwa na kifafa cha mimba, ambacho mwanamke anaweza kuwa na shinikizo la damu la kawaida wakati wa ujauzito asivimbe sana uso,” anasema.
Dk Mhando anasema licha ya kwamba kuvimba ni kawaida, lakini hali hiyo pia inaweza kuwa ishara kuwa kuna shida ya kiafya kwa mjamzito.
Anasema kuna shinikizo linalosababishwa na kondo la nyuma ambalo huzalisha sumu.
“Sumu hiyo husababisha mishipa ya damu kuwa na mpenyo au ‘size’ ndogo na hii huathiri figo, ini na sehemu zote za mwili na kusababisha mwili wote kujaa maji kuanzia usoni, mgongoni mpaka miguuni na wengine huvimba mpaka mikono,” anasema daktari huyo.
Anasema hali ile huitwa shinikizo la damu linalosababishwa na kifafa cha mimba. “Na mara nyingi ukiona mjamzito amevimba uso, ni dalili kwamba figo za huyu mama zimeanza kushindwa kufanya kazi.”
Dk Mhando anasema kinamama hawa wanashauriwa kuwahi kliniki. Anasema kwa mujibu wa sera, mama anatakiwa kuhudhuria kliniki mahudhurio manane.
Anasema hudhurio la kwanza liwe chini ya wiki 12, la pili linatakiwa liwe wiki ya 20, hudhurio la tatu linatakiwa kuwa kwenye wiki ya 24 na la nne wiki ya 30, la tano 36, 38 pamoja na wiki ya 40, kila hudhurio lazima awe anaangaliwa hali yake.
“Wanaobainika mara nyingi hufanyiwa vipimo na kupata matibabu ili kuzuia asije kupata kifafa cha mimba, uwezekano wa kumpoteza mama na mtoto huwa mkubwa.
“Mama anatupa miguu, mikono na anakuwa kama amepoteza fahamu, mara nyingi hutokea kama mama hakupata matibabu ya awali kwenye kliniki ya mama na mtoto,” anasema Dk Mhando.
Anasema hali hiyo hutokea kwa wajawazito wenye historia ya tatizo, yaani kama kwenye familia, basi mama ana uwezekano wa kupata hilo tatizo.
Anasema wengine ni wale wenye mapacha tumboni au mimba wakati wa umri mdogo.
Pia huwakumba wanene kupita kiasi, wanaokuwa na shinikizo la damu linaloweza kubadilika na kutengeneza kifafa cha mimba au wenye kisukari.
“Tunashauri kabla ya kubeba mimba kama ana uzito mkubwa au kitambi, mama kama ana BMI zaidi ya 40 ana kitambi anashauriwa apunguze uzito wake kabla hajabeba mimba.”
Anasema kinamama wenye hiyo changamoto moja ya matibabu kliniki hupewa calcium inayosaidia kupunguza kifafa cha mimba, kipindi cha mwanzoni cha ujauzito wanaobainika kupitia kipimo cha damu kuna matibabu hupewa.
“Hatarini wapo wale wenye mimba za wiki 40, wiki ya 12 wengi wanasaidiwa na hivyo anaweza kuangaliwa na ikitokea presha yake ipo juu sana na kuna uwezekano wa figo kushindwa kufanya kazi, ukimzalisha mapema na kutoa ile plasenta unakuwa umemsaidia.
“Kama mama ana dalili za kupata kifafa cha mimba na ana hitilafu kwenye ogani mojawapo, tunatoa mimba hata kama mtoto hajafikia ili kuokoa uhai wa mama,” anasema Dk Mhando.
Gazeti la DailyMail la nchini Uingereza limeandika sababu za uvimbe, huanza lini na nini cha kufanya kupunguza hali hiyo.
Wakati wa ujauzito, mwili wa mama hupanuka ili kusaidia kijusi kinachokua.
Homoni za ujauzito, estrojeni na progesterone huongezeka katika mishipa ya damu na kusababisha uvimbe kuzunguka mwili mzima, ikiwa ni pamoja na pua kuvimba.
Kuvimba pua ndiyo dalili inayoogopwa zaidi, kwani husababisha ulemavu wa uso wa muda ambao humfanya mtu asitambulike.
Kuvimba kunaweza kuanza katika mwezi wa nne wa ujauzito, yaani ‘trimester ya 2’ na kuendelea zaidi hadi trimester ya tatu, yaani miezi tisa.
Mwili hutoa asilimia 50 zaidi ya damu na maji ili kusaidia mtoto anayekua wakati wa ujauzito.
Majimaji ya ziada husaidia kulainisha na kupanua mwili kwa ukuaji wa mtoto na kuandaa viungo vya mama kwa ajili ya kujifungua.
Maji ya ziada yanaweza kujilimbikiza kwenye kifundo cha mguu, mikono, uso na pua.
Jinsi ya kupunguza uvimbe
1. Hakikisha kila wakati unalala na mto mzuri ambao unaweza kuinua kichwa chako vizuri.
2. Punguza ulaji wa chumvi au vyakula vyenye chumvi nyingi ikiwemo chipsi.
3. Kunywa maji mengi wakati wote. Mwili wako unatengeneza damu zaidi katika hatua hii. Kwa hiyo maji mengi yanahitajika ili kuendelea kuzunguka vizuri.
4. Pendelea zaidi kufanya masaji ya uso. Tumia vidole vyako na zunguka maeneo yote ya mwili, kama una mtu karibu anaweza kukufanyia masaji ya miguu kwa uangalifu zaidi.
5. Fanya matembezi ya asubuhi au jioni.
6. Daima osha uso wako kwa maji baridi au vuguvugu asubuhi unapoamka.
7. Pendelea zaidi kuoga kwa maji baridi badala ya moto.