Arusha. Serikali imeonyesha kukerwa na utitiri wa vyama vya kitaaluma vilivyopo nchini kwa sasa na kuagiza uchunguzi wa kina.
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene akimtaka Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Juma Mkomi kuunda kikosi kazi cha kuchunguza.
Simbachawene ameyasema hayo leo Alhamisi, Mei 2, 2024 wakati akifungua mkutano wa 11 wa wanachama wa Jumuiya ya Kiafrika ya Utumishi wa Umma na Uongozi (AAPAM) Tawi la Tanzania unaofanyika jijini Arusha .
Amesema hivi karibuni kumetokeza utaratibu wa kila taaluma kutaka kutengeneza mashirikisho, jumuiya na vyama vya kitaaluma ambazo zimekuwa nyingi na zinachukua muda wao mwingi kuhangaikia taratibu za usajili badala ya kuhudumia wananchi.
“Hivi vyama malengo yake ni kukusanya maduhuri na waliojindaa kuwa viongozi pamoja na kujiaminisha wanataka kutetea kada husika, lakini wana tamaa na madaraka na ndio maana hata kabla ya kupata usajili wanaanza kugombana huko huko,” amesema Simbachawene.
Kauli hiyo ya Simbachawene imefuata zikiwa zimepita siku tano tangu vyama 19 vya wafanyakazi wa sekta binafsi vikieleza dhamira ya kuanzisha shirikisho lao, kwa sababu ya kile walichodai kutengwa na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (Tucta).
Mwenyekiti wa mpito wa vyama hivyo 19 vilivyo nje ya Tucta, Michael Pamaga alisema baada ya kubaini kutengwa kwenye matukio muhimu kama Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani , wameona njia sahihi ni kuanzisha shirikisho lao ambalo litakuwa linatetea maslahi ya wafanyakazi hususani wa sekta binafsi nchini.
Kwa mujibu wa tovuti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, hadi Agosti 2020, jumla ya vyama vya wafanyakazi vilivyosajiliwa vilikuwa 32. Vyama vilivyo kwenye shirikisho la Tucta viko 13 na vingine 19 siyo wanachama wa shirikisho hilo.
Akizungumza kwenye mkutano wa AAPAM, Simbachawene amesema tangu vimeanzishwa vyama hivi, harakati zimekuwa nyingi kwa kuwa kila kada sasa wanataka kuanzisha, mara madaktari, wahasibu, makatibu muhtasi, walimu, na vingine. Amesema hekaheka zimekuwa nyingi, hata utawala na rasilimali watu, kuna chama huko mtaani kinapambana kujisajili.
“Sasa unajiuliza, mwisho wa haya yote itakuwa ni nini kama sio kuathiri utoaji wa huduma kwa wananchi, kwa sababu harakati zimekuwa nyingi kuliko utendaji kazi na uzalishaji wa huduma,” amesema waziri huyo.
Amemwelekeza Katibu Mkuu wa ofisi yake kutengeneza kikosi kazi kuchunguza utitiri wa vyama hivyo na vina siri gani, na baada ya hapo kutengeneza mwongozo mpya wenye masharti ya jinsi ya kuanzisha, sababu zake na namna ya kudhibiti.
“Naona hili jambo linapoelekea litatufikisha pabaya, hivyo wacha tuvichunguze lakini, pia tutengeneze mwongozo.
“Na bahati mbaya zaidi mnapounda hivi vyama mnachanganya watumishi wa umma na wa sekta binafsi, siri za Serikali zitabaki salama? Mparaganyiko huu wa nini sasa, hamtekelezi majukumu yenu wala utekelezaji wa wajibu wa kitaaluma wa kuhudumia wananchi bali ni kukusanya maduhuri na baadae kununuliana fulana siku ya wafanyakazi, sitaki kuona tena,” amesema.
Mbali na hilo, amesema Serikali itaanza kuwachukulia hatua za kisheria maofisa utumishi na rasilimali watu wanaohujumu mfumo mpya wa Usimamizi wa Utendaji Kazi kwa Watumishi wa Umma( PEPMIS).
“Yapo pia malalamiko ya uvunjifu wa maadili na ukiukwaji wa taratibu za kiutendaji ikiwemo baadhi yenu kuingia kwenye mfumo wa taarifa za mtumishi (new HCMIS) na kusimamisha mishahara au kufanya makato ya mishahara bila kufuata taratibu ,” amesema na kuongeza;
“Sasa mfahamu kuwa katika sheria zetu za Tehama na za kiutumishi zinatambua hayo kuwa ni makosa makubwa, tena ni jinai. Hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa wale watakaobainika kuchezea mifumo ya serikali kuanzia sasa ambayo inatusaidia kuboresha ufanisi.”
Awali, Rais wa AAPAM, Tawi la Tanzania, Leila Mavika amesema lengo la mkutano huo mbali na kubadilishana uzoefu katika utendaji kazi, pia ni kujadiliana changamoto wanazokabiliana nazo kazini na namna ya kuzitatua.