SERIKALI imeanza kufuatilia watu, vikundi na taasisi zinazotoa kinyume cha sheria mikopo yenye masharti magumu na riba kubwa maarufu kama kausha damu, kwa ajili ya kuwachukulia hatua za kisheria. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).
Akizungumza bungeni jijini Dodoma, leo tarehe 2 Mei 2024, Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, amesema Serikali inachukua hatua hiyo ili kuwalinda wananchi wanaoathirika ikiwemo kutaifishiwa mali zao kwa kushindwa kuirejesha mikopo kutokana na masharti magumu.
Mbali na msako wa watoaji hao mikopo ya kausha damu pasipo kuwa na leseni kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dk. Mwigulu amesema Serikali inafuatilia benki na taasisi za fedha ndogondogo zilizosajiliwa na kuwa rasmi, ambazo zinatoa mikopo yenye masharti magumu na kwamba ikibainika wanatenda makosa hayo, watanyang’anywa leseni zao.
“BoT inafuatilia kwa karibu mwenendo wa mikopo ya kidigitali iliyoidhinishwa na ikibainika kuwa kuna ukiukwaji wa leseni ya utoaji mikopo hiyo hatua stahiki itachukuliwa ikiwa pamoja na kuwafutia leseni. BoT imeshafuta baadhi ya leseni za watoa huduma ndogondogo za kifedha baada ya kubainika kwamba wanakiuka taratibu na masharti yanayotolewa,” amesema Dk. Mwigulu.
Dk. Mwigulu amewashauri wananchi kuchukua mikopo katika taasisi za fedha na benki rasmi ambazo zimesajiliwa na Serikali.
Kauli hiyo ya Dk. Mwigulu imekuja baada ya kuibuka mjadala bungeni kuhusu athari wanazopata baadhi ya wananchi hususan wanawake kutokana na mikopo hiyo ambayo kwa sasa inatolewa hadi kwenye mitandao ya simu.