Uhaba wa mabeki wazawa wenye uwezo wa juu, uzoefu pamoja na kutokuwa tayari kuwanufaisha wapinzani iwapo wawili hao wataondoka, ni sababu tatu za msingi zilizofanya uongozi wa Yanga kuanza mazungumzo ya haraka na mabeki wake Bakari Mwamnyeto na Kibwana Shomari kwa ajili ya kuwashawishi waongeze mikataba licha ya uwepo wa wachezaji wa nafasi nyingine ambao mikataba yao inaelekea ukingoni.
Mikataba ya Mwamnyeto anayecheza nafasi ya beki wa kati na Kibwana anayecheza beki ya pembeni, itamalizika mwishoni mwa msimu huu na kila mmoja kwa sasa yuko huru kufanya mazungumzo na kusaini mikataba ya awali ya timu nyingine kwa mujibu wa kanuni.
Ukiondoa Mwamnyeto na Kibwana, wachezaji wengine wa Yanga ambao mikataba yao itafikia tamati mwishoni mwa msimu huu ni Denis Nkane, Farid Musa, Joyce Lomalisa na Skudu Makudubela.
Hata hivyo bado mazungumzo baina ya Yanga na Nkane pamoja na Faird bado hayajaanza tofauti na Kibwana na Mwamnyeto ambao uongozi wa timu hiyo umelazimika kufanyanhivyo haraka ili kuzuia wasijiunge na timu nyingine kutokana na ubora wao.
“Miongoni mwa timu ambazo zinawahitaji wachezaji hawa ni washindani wetu kwenye mbio za ubingwa sasa ukiruhusu waondoke maana yake, mpinzani wako ananufaika kwa kuimarika huku wewe ukipunguza ubora katika kikosi chako na uwezekano wa kupata aliye bora zaidi yao ukiwa ni finyu.
“Nkane na Farid hakuna presha kubwa juu yao kwa vile nafasi wanazocheza tuna machaguo mengi lakini kwenye ukuta ni muhimu sana kupalinda,” alisema mmoja wa viongozi wa Yanga.
Gazeti hili linafahamu kuwa kati ya wachezaji ambao mikataba yao inaelekea ukingoni, Yanga haina mpango wa kubaki na Lomalisa na Makudubela ambao tayari wanafahamu kuwa hawatokuwa sehemu ya kikosi cha timu hiyo msimu ujao.
Kumekuwa na tetesi kuwa Bakari Mwamnyeto amekuwa katika rada za Simba ambayo inajipanga kuimarisha safu yake ya ulinzi ambayo msimu ujao inaweza kutokuwa na Enock Inonga ‘Varane’ anayeripotiwa kuwa mbioni kujiunga na AS FAR ya Morocco.
Hata hivyo, meneja wa Mwamnyeto, Carlos Sylivester licha ya kukiri kuwa kuna ofa za kumhitaji mchezaji huyo kutoka ndani na nje ya nchi, Yanga iko katika nafasi nzuri ya kumbakiza.
“Siwezi kusema ofa nyingine zimetoka wapi ila zipo hadi za nje lakini klabu yake imeonyesha nia ya kumbakisha na tayari tumeshaanza mazungumzo kwa ajili ya mkataba mpya na yanaendelea vizuri,” alisema meneja huyo.
Mwamnyeto ni miongoni mwa wachezaji waliokuwa nguzo imara kwa Yanga ilipotinga hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita na akiwa nahodha tayari ameshaiongoza timu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara mbili, Kombe la Shirikisho la CRDB mara mbili na Ngao ya Jamii mara mbili.
Beki wa kati mzawa ambaye anaonekana kuwa kiwango bora kwa sasa nje ya wale wanaocheza katika klabu kubwa za soka nchini ni Lameck Lawi wa Coastal Union ambaye hata hivyo inaripotiwa kuwa ameshaaziingiza vitani Azam FC, Simba na Ihefu ambazo zinawania saini yake huku klabu yake ikiweka dau la zaidi ya Shilingi 150 milioni ili imuuze.
Kwa upande wa Kibwana Shomari, meneja wake George Job alilithibitishia gazeti hili kuwa wameanza majadiliano na Yanga na yanaonyesha muelekeo wa beki huyo kubakia.
“Yanga wameonyesha ‘interest’ (nia) ya kumuongezea mkataba na tayari tumeshakutana nao kufanya mazungumzo ambayo siwezi kusema tumekamilisha kwa vile kila upande unaangalia nini unachokihitaji kwa mwenzake lakini yanaonyesha mwanga mzuri.
“Kuhusu ofa kutoka nje ya Yanga tunayo moja tu ingawa kuna klabu nyingine imeulizia hadhi ya mkataba wake hivyo hatuwezi kuihesabu kama imetuma ofa,” alisema Job.
Shomari ni miongoni mwa mabeki wachache ambao wana uwezo wa kucheza nafasi nyingi tofauti kwa ufasaha ambapo anaweza kutumika beki wa kulia au kushoto pamoja na ile ya winga.