SPOTI DOKTA: Mei mosi na tishio afya za wachezaji

Kila Mei Mosi kwa mwaka inaadhimishwa siku ya kimataifa ya wafanyakazi duniani. Chini ya mwamvuli wa Umoja wa Mataifa (UN), Tanzania na nchi duniani iliyoazimisha siku hiyo hapo jana.

Wadau na wamichezo nao ni sehemu ya maadhimisho hayo ambayo kitaifa yalifanyika jijini Arusha. Sikuya wafanyakazi iliwekwa mahsusi ili kutambua michango ya wafanyakazi duniani na vilevile ni moja ya matukio makubwa kimataifa kutambua mchango wa wafanyakazi.

Vilevile ni moja ya matukio ambayo ni fursa ya kutambua bidii na kujitolea kwao. Itakumbukwa katika tasnia ya michezo duniani ni moja ya wafanyakazi ambao wana mchango mkubwa kiuchumi duniani.

Afya ya mfanyakazi katika eneo la kazi ni muhimu kwa maslahi yake na mwajiri wake. Ndio maana nchi zote zilizopo chini ya Umoja wa Mataifa zina sera bora kwa ajili ya kulinda afya ya mfanyakazi.

Eneo la kazi la mwanamichezo ni viwanja vya michezo, maeneo anayojifunzia mchezo husika na mazingira ya klabu anayoishi wakati anasubiri kufanya majukumu ya klabu.

Mfanyakazi ambaye ni mchezaji anaweza kufanya kazi saa 100,000 katika utumishi wake lakini hazionekana ni saa nyingi endapo tu mazingira ya kazi yanapokuwa tishio kwa afya yake.

Mfano kama mchezaji atacheza au kufanya mazoezi katika uwanja usio na ubora anaweza kujiweka katika hatari ya kupata majeraha yatokanayo na michezo. Itakumbukwa kuwa mazingira ya kazi yanaweza kuwa tishio katika afya ya akili na mwili endapo mwajiri hatazingatia sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa kulinda afya ya mfanyakazi.

Hapa tunapata picha kuwa mchezaji naye ni mfanyakazi wakati anatimiza majukumu yake katika eneo lake la kazi anakutana na matishio mbalimbali ikiwamo kuumia.

Kama ilivyo kwa wafanyakazi wa viwandani wanavaa vifaa vya kujikinga na ajali, vivyo hivyo mchezaji awapo uwanjani huvaa vikinga majeraha ikiwamo viatu na vikinga ugoko.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), mazingira salama kiafya eneo la kazi ni yale yasiyo na tishio kwa afya au pasipo kuumwa au majeraha kwa mfanyakazi.

Kwa kutambua jambo hilo, Shirikisho la Soka Duniani (Fifa)lina miongozo yake ya ujenzi wa viwanja ambavyo ni salama kwa afya na usalama wa mwanamichezo. Hata klabu inapojenga au inapokodi hoteli au majengo kwa ajili ya wanamichezo kuishi ni lazima izingatie vigezo vya usalama wa afya ya mfanyakazi wake ambaye ni mwanamichezo.

Mfano klabu inahitajika kumuweka mchezaji wake katika makazi ambayo ni rafiki kiafya. Makazi hayo huhitajika kuwa na hali ya hewa nzuri yasiyo na msongamano. Vilevile viwanja vyote vya kuchezea au mazoezi vinahitajika kuwa na huduma ya kwanza na vifaa vya uokoaji.

Lengo kuu la mambo hayo siyo tu kujali usalama wa mtazamaji michezo, bali pia kujali afya ya mwanamichezo ambaye katika huwajibika kucheza.

Mwamichezo yeyote iwe binafsi au ambaye ameajiriwa na klabu ana haki zake zote za msingi ikiwamo kuhakikishiwa usalama wa afya yake ili aweze kuwajibika katika kazi yake michezo bila kuwa na tishio. Ifahamike kuwa kama mwanamichezo atakuwa na tishio kiafya katika mazingira ambayo anacheza ina maana kuwa hatakuwa sawa kiafya kiakili na kimwili. Hii inapotokea mchezaji hatakuwa salama kiafya, hivyo ataathirika na huduma anayotoa ambayo ndio maslahi ya klabu anayoshiriki. Ndio maana mchezaji hupimwa afya wakati wa kununuliwa huku pia klabu huwa na wataaalamu wa afya wanaolinda afya ya mchezaji.

Kwa wanamichezo kuna tishio?

Mchezaji anapata matishio mbalimbali wakati anacheza, vifaa anavyotumia, eneo analofanyia mazoezi, makazi anayoishi na wakati pia anaposafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Pamoja na ukweli kuwa katika michezo kuna sheria na kanuni zinazotumika wakati michezo inapofanyika na kusimamiwa na waamuzi, sheria hizo na kanuni zipo ambazo moja kwa moja zinahusika kumlinda mchezaji asipate madhara kiafya. Mfano mchezaji wa soka anapiga kiwanja kwa miguu kwa kumrukia mwenzake hupewa kadi nyekundu.

Hiyo ni kwa sababu aina hiyo faulo inaweza kuwa tishio kubwa kwa afya ya mchezaji ikiwamo kuvunjika au kupata majeraha ya kuchanika tishu laini. Mwanamichezo wakati anashiriki michezo anapata majeraha mbalimbali ambayo yanachangia kupata tishio kiafya. Kwa upande wa tishio la afya wakati anacheza au wakati anafanya mazoezi mchezaji anaweza kutumia vifaa duni ambavyo vinaweza kumfanya kupata majeraha kirahisi.

Kwa upande wa eneo analocheza au kufanyia mazoezi kama mchezaji atacheza viwanja visivyo na ubora anaweza kupata tishio kiafya kwani anaweza kupata majeraha kirahisi kutokana na uduni wa eneo husika.

Mfano kama uwanja hautakuwa na nyasi bora huku ukiwa hauko bapa ina maana mchezaji anaweza kupata majeraha wakati anacheza ikiwamo kujipinda vibaya kwa viungo vya mwili au kuanguka kirahisi. Kwa upande wa makazi kama yatakuwa si mazuri ina maana hataweza kupumzika na kulala vizuri. Hapa moja kwa moja ni tishio kubwa kiafya hatimaye kushindwa kufanya kazi yake.

Michezo huwa inahusisha kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Hapa mwanamichezo ambaye kwa nchi kama za afrika zenye klabu nyingi zisizo na fedha za kutosha zinatumia usafiri wa barabara. Mchezaji anasafiri mara nyingi sana, hivyo kuwa pia katika hatari ya kupata ajali wakati wa kusafiri na vyombo vya moto hasa magari. Hili ni tishio kwa afya hasa kwa wanamichezo wa nchi za Afrika.

Mienendo na mitindo binafsi ya mwanamichezo kama itakuwa mibaya inaweza kuwa tishio zaidi kwa afya hatimaye kushindwa kufanya kazi ya kucheza. Mienendo na mitindo hiyo ni pamoja na ulevi, uvutaji tumbaku, utumiaji dawa za kulevya, ulaji holela wa vyakula, anasa na uvivu wa kutofanya mazoezi. Ifahamike kuwa michezo ni kazi pia, hivyo wanamichezo na klabu wanapaswa kuzingatia miongozo na kanuni zinazolinda afya ya mchezaji wakati anatimiza majukumu yake.

Related Posts