Kama watu wote ulimwenguni watakuwa na matumizi ya rasilimali za kiikolojia kama ya Ujerumani, basi watu watahitaji dunia tatu ili kuwa na rasilimali za kutosha kukidhi mahitaji yao kwa uendelevu.
Matumizi haya makubwa kupitiliza yanajitokeza wakati mahitaji ya taifa hilo ya rasilimali za kiikolojia na huduma zikizidi kiasi kinachoweza kuzalishwa na dunia kwa mwaka.
Watumiaji wabaya zaidi wa malighafi za kiikolojia kama vile Qatar na Luxembourg, tayari walishavuka viwango vyao mwezi Februari.
Mataifa mengine kama vile Cambodia na Madagaska yanatarajiwa kuendelea kuwa na matumizi yasiyovuka viwango.
Soma pia:Idadi ya watu wanaofunga ndoa Ujerumani yapungua
Uzalishaji na matumizi ya nyama Ujerumani ni moja ya vyanzo vya taifa hilo kuwa na matumizi makubwa ya rasilimali za kiikolojia za dunia, kulingana na shirika la Global footprint Network.
Takriban asilimia 60 ya ardhi maalumu kwa kilimo nchini humo, inatumika kuzalisha mazao kwa ajili ya kuwalisha wanyama, na mamilioni ya tani za vyakula hivyo, zinasafirishwa kutoka nchi nyingine.
GIZ: Bidhaa zilizoingizwa nchini zilichngia uharibifu
Shirika la maendeleo la kimataifa la Ujerumani la GIZ linasema kuwa, idadi jumla ya bidhaa zinazoagizwa Ujerumani zilisababisha uharibifu wa hekta 138,000 za misitu ya kitropiki kote duniani kati ya mwaka 2016 hadi 2018.
Mataifa yanayoendelea ambayo yanaishi ndani ya viwango vinavyostahili vya matumizi ya rasilimali za kiikolojia ndiyo yanayobeba athari za nchi zenye matumizi makubwa kupitia uharibifu wa mazingira na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.
Jumanne wiki hii, chama cha marafiki wa dunia BUND kiliyakosoa matumizi mabaya ya ardhi, maji na malighafi. Mwenyekiti wa shirika hilo Olaf Bandt alisema kuwa dunia imeelemewa.
Aliongeza kuwa nchi yenye matumizi makubwa ya rasilimali kama Ujerumani inaendesha shughuli zake vibaya na bila kujali.
Chama hicho cha BUND kinatoa wito kwa serikali ya Ujerumani kuanzisha sheria mpya za kulinda rasilimali kwa ajili ya udongo na ardhi, kilimo na ufugaji, maeneo ya uvuvi, maji, misitu na mbao.
Soma pia:Baerbock: Mataifa ya Ghuba na China kuchangia katika mfuko wa fidia
Faharasa iliyochapishwa Alhamisi wiki hii inaonesha kuwa, matumizi haya makubwa ya rasilimali za kiikolojia hayamaanishi kuwa raia wa nchi husika wana maisha bora.
Faharasa hiyo imetolewa na taasisi ya Hot or Cool ya mjini Berlin inayokusanya data kuhusu ustawi, matarajio ya umri wa kuishi na kiwango cha gesi chafu inayotokana na shughuli za binadamu.
Madhumuni yake ni kutathmini namna mataifa yanavyowajali raia wao bila kuielemea dunia.
Nchi za ulaya katika kutatua changamoto ya ikolojia
Nchi za Sweden na Ujerumani kwa mfano, zina viwango sawa vya ustawi jumla na makadirio ya umri wa kuishi, lakini Sweden ilifanikiwa kuwa na kiwango hicho cha ubora wa maisha huku ikiwa na uzalishaji mdogo wa hewa chafu kuliko Ujerumani.
Costa Rica, ina kiwango kinachofanana na Ujerumani cha wastani wa umri wa kuishi na ustawi lakini ina nusu ya athari za mazingira ikilinganishwa na Ujerumani
Faharasa hiyo, inayochanganua pia viwango vya kipato ndani ya mataifa, ilibainisha kuwa, asilimia kumi ya watu wenye vipato vikubwa zaidi ndiyo wahusika wakuu wa karibu wa nusu ya uchafuzi wa mazingira lakini hawanufaiki chochote katika ustawi wala kiafya ikilinganishwa na nchi zinazochafua mazingira kwa kiasi kidogo.
Soma piaUjerumani na Ufaransa zakabiliwa na joto kali:
Mfano mzuri ni usafiri wa anga. Watu wanaosafiri sana kwa ndege wanachafua zaidi mazingira kuliko wasiotumia usafiri huo ingawa hawaoneshi kufaidika kiafya au kustawi ikilinganishwa na wanaotumia ndege kusafiri mara chache.