Wababe wa Simba na Yanga katikati ya mtego

AL Ahly ya Misri itabeba tena? Hilo ndilo swali  lililopo vichwani mwa mashabiki na wapenzi wa soka Afrika kwa sasa, wakati wakisubiri mechi mbili za fainali za michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mechi hizo zitakazopigwa kati ya Mei 18 na 25 mwaka huu itakutanisha watetezi hao wanaoshikilia taji la 11 dhidi ya mabingwa mara nne wa michuano hiyo, Esperance ya Tunisia.

Esperance ndio watakaokuwa wenyeji wa mechi ya mkondo wa kwanza itakayopigwa Mei 18 kwenye Uwanja wa Hammadi Agrebi, jijini Tunis, Tunisia na ile ya marudiano itachezwa Mei 25 Uwanja wa Kimataifa wa Cairo, Misri ambapo siku hiyo ndio na bingwa wa msimu wa 2023-2024 atafahamika.

Al Ahly iliyokuwa kundi moja na Yanga na kushinda mechi moja ya nyumbani na kulazimishwa sare ya 1-1 ugenini jijini Dar es Salaam kabla ya kutinga robo fainali na kuvaana na Simba iliyoifunga nje ndani kwa jumla ya mabao 3-0, hii itakuwa ni fainali ya 17 ya michuano hiyo tangu mwaka 1982.

Rekodi zinaonyesha katika fainali 16 ilizocheza tangu wakati huo, Al Ahly imebeba mataji 11, huku ikipoteza fainali tano, ilihali kwa Esperance hiyo ni fainali ya tisa ya Ligi ya Mabingwa, kwani tayari ilishacheza nane zikiwamo mbili dhidi ya Al Ahly mwaka 2012 na 2018 na kila moja kushinda moja.

Katika fainali za mwaka 2012, Al Ahly ndio iliyoibuka kidedea kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-2, baada ya sare ya 1-1 nyumbani na kwenda kushinda ugenini 2-1, kabla ya Esperance kujibu mapigo 2018 ikilala 3-1 ugenini na kushinda nyumbani 3-0 na kubeba taji kwa ushindi kwa jumla wa mabao 4-3.

Kitu cha kuvutia zaidi ni kwamba mbali na kukutana katika fainali hizo za 2012 na 2018, pia timu hizo zimeshavaana mechi 14 zikiwemo za nusu fainali za 2001, 2010, 2021 na 2023 pamoja na robo fainali ya 2017.

Pia zimeshakutana katika hatua ya makundi mara mbili tu mwaka 2007 na 2011 ya Ligi ya Mabingwa pamoja na ile ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2015.

Ukiangalia rekodi baina ya timu hiyo katika michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa tangu zilipoanza kukutana kuanzia mwaka 2001, namba zinaibeba zaidi Al Ahly, kwani imeshinda mara tisa kati ya 18, huku Esperance ikishinda mara nne tu na michezo mitano iliisha kwa sare tofauti.

Hiyo ni mbali na ushindi wa mechi mbili za makundi Kombe la Shirikisho, ambapo Al Ahly ilishinda 3-0 nyumbani kisha kwenda kutamba tena ugenini kwa bao 1-0.

Kwa namna timu hizo zilivyoianza safari ya fainali ya msimu huu, ni wazi bado kuna nafasi kubwa ya Al Ahly kutetea taji, iwapo itaendelea kucheza kama inavyofanya katika hatua ya mtoano ambapo soka lake huwa ni la kasi na kusaka zaidi ushindi bila kujali inacheza nyumbani au ugenini.

Katika mechi nne zilizopita za robo fainali dhidi ya Simba na za nusu fainali mbele ya TP Mazembe ya DR Congo, watetezi hao walikuwa tofauti kabisa na wale waliocheza makundi na kumaliza kama kinara wa Kundi D lililokuwa na Yanga, CR Belouizdad ya Algeria na Medeama ya Ghana.

Al Ahly ya hatua ya mtoano ilikuwa na kasi, inayoshambulia kwa akili na kujilinda vilivyo ndio maana haikuruhusu bao lolote katika mechi hizo nne, kwani iliifunga Simba 1-0 ugenini kisha kushinda 2-0 nyumbani, huku ikilazimisha suluhu ugenini jijini Lubumbashi na kushinda 3-0 nyumbani.

Hata katika hatua ya makundi, licha ya Al Ahly kutoonekana tishio, lakini iliruhusu bao moja tu siku ilipocheza na Yanga jijini Dar es Salaam na mechi kuisha kwa sare ya 1-1, ikitunguliwa na Pacome Zouzoua na ilimaliza na pointi 12 katika kundi hilo ikifunga mabao sita.

Mabao hayo yaliifanya Al Ahly kuwa na wastani wa kufunga bao moja katika mechi zote sita ilizocheza, ikifuatiwa na Yanga iliyokuwa ya pili na pointi nane sawa na za CR Belouizdad iliyokuwa ya tatu na Medeama ilimaliza mkiani ikiwa na pointi nne.

Ukiachana na aina ya soka inalocheza Al Ahly katika mechi za mtoano kulinganisha na hatua ya makundi, lakini ubabe wake mbele ya Esperance unaipa nafasi kubwa ya kuboresha rekodi ya kubeba taji kwa mara ya 12 na kuzidi kutengeneza pengo kubwa baina ya Zamalek ya Misri na Mazembe zinazoifuata kwa kutwaa mataji mengi, kwani zenyewe zimebeba mara tano kila mmoja.

Hata hivyo, bado itakuwa na kazi kubwa mbele ya Esperance, kwani wapinzani wao hao sio timu ya kubezwa kwa namna ilivyovuka kutoka makundi ikiwa Kundi B pamoja na Petro Atletico ya Angola na hata ilivyocheza mechi nne zilizopita za mtoano.

Watunisia waliomaliza nafasi ya pili katika kundi hilo ikiwa na pointi 11, ikifunga mabao sita na kufungwa matatu, huku katika mechi za robo fainali dhidi ya Asec Mimosas iliyokuwa vinara wa Kundi C lililokuwa pia na Simba, Jwaneng Galaxy na Wydad CA ya Morocco ilipenya kwa penalti.

Esperance ilivuka kwa penalti 4-2 baada ya kutoka suluhu nje ndani mbele ya mabingwa hao wa mwaka 1998, kisha katika nusu fainali ikakutana na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini iliyoing’oa Yanga pia kwa penalti baada ya suluhu ya nyumbani na ugenini kwa kuifunga jumla ya mabao 2-0.

Ilianza na ushindi wa bao 1-0 nyumbani kisha kurejea tena ushindi kama huo ugenini Afrika Kusini na kutinga hatua hiyo, lakini uzoefu wa kucheza fainali nane unaipa nafasi ya kuipa ugumu Al Ahly, hata kama rekodi zinawabeba Wamisri hao kwa sasa.

Kwa aina ya soka ililocheza mbele ya Asec na Mamelodi la kujilinda zaidi na kushambulia kwa kushtukiza inaweza kuipa ugumu Al Ahly, licha ya ya timu hizo kufahamiana kwa kukutana mara nyingi zaidi ktika michuano ya CAF.

Bila ya shaka kutakuwa na burudani tamu ya kutaka kushuhudia kama ni Esperance inabeba tena taji baada ya kufanya hivyo mwaka 2019 ilipoifunga Wydad CA ya Morocco, ili kuzifikia Zamalek ya Misri na TP Mazembe zilizobeba mara tano kila moja.

Pia mechi hizo mbili za fainali za michuano hiyo kwa msimu huu, licha ya vita ya mafahari hao wa Afrika Kaskazini, lakini zitakuwa na mchuano wa mastaa wa timu hizo hasa wanaowania tuzo ya Mfungaji Bora wa michuano hiyo kwa msimu huu.

Orodha ya sasa ya wafungaji wa michuano hiyo inaongozwa na Sankara Karamoko aliyekuwa na Asec Mimosas ya Ivory Coast kabla ya kuuzwa Ulaya kupitia dirisha dogo la Januari, akiwa na mabao manne ya kufunga na asisti moja.

Nyota huyo wa Ivory Coast anafuatiwa na Pacome Zouzoua wa Yanga mwenye mabao matatu na asisti moja, japo timu yake ilishatolewa pamoja, akiwa sambamba na Hussein El Shahat wa Al Ahly, Yas Sasse wa Esperance na Abdelraouf Benguit wa CR Belouizdad waliofunga pia mabao matatu kila mmoja. Kama ilivyo kwa Sankara na Pacome, pia Benguit naye timu yake ilishatolewa mapema michuanoni, hivyo kuacha vita ibaki kwa El Shahat na Sasse pekee kwani ndio wenye nafasi ya kumaliza ubishi wa tuzo hiyo itaenda wapi, kama watajituma na kufunga katika mechi hizo mbili za fainali.

Msimu uliopita wa Ligi ya Mabingwa, tuzo ya Mfungaji Bora ilienda kwa Mahmoud Kahraba wa Al Ahly na Peter Shalulile wa Mamelodi waliofunga mabao sita kila mmoja, huku Al Ahly ikibeba ubingwa kwa kuitungua Wydad kwa jumla ya mabao 3-2.

Bila ya shaka ni mtego kwa Al Ahly ya kutaka kutetea taji la michuano kwa ujumla ya Ligi ya Mabingwa, lakini kuona pia inatoa tena Mfungaji Bora kama ilivyokuwa msimu uliopita, huku wapinzani wao nao wakipania kuwatibulia kufuta unyonge mbele ya wababe hao kihistoria Afrika.

Ngoja tuone itakavyokuwa, lakini ni wazi fainali za mwaka huu zitakuwa ni kazi kazi kwelikweli.

Mechi zilizopita za timu hizo

Nusu fainali (CafCL) Nov 4, 2021

Al Ahly 0-0 Esperance Nov 17, 2001

Al Ahly 3-0 Esperance Ago 4, 2007

2010, Nusu fainali (CafCL)

Al Ahly 2-1 Esperance Okt 17, 2010

2011 Makundi (CafCL) July 30, 2011

Esperance 1-0 Al Ahly Sept 16, 2011

2012 Fainali (CafCL) Nov 4, 2012

Al Ahly 1-1 Esperance Nov 17, 2012

2015 Makundi (CafCC) Jun 28, 2015

Al Ahly 3-0 Esperance Ago 22, 2015

Robo fainali (CafCL) Sept 16, 2017

Al Ahly 2-2 Esperance Sept 23, 2017 Esperance 1-2 Al Ahly

Al Ahly 3-1 Esperance Nov 9, 2018

Nusu Fainali (CafCL) Jun 19, 2021

Esperance 0-1 Al Ahly Jun 26, 2021

Nusu Fainali (CafCL) Mei 12, 2023

Esperance 0-3 Al Ahly Mei 19, 2023

Related Posts