Watuhumiwa wengine sita wabainika ubadhirifu wa Sh1.3 bilioni

Mbeya. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mkoa wa Mbeya imebaini ongezeko la watuhumiwa sita wa ubadhirifu wa fedha kwa njia ya mtandao (POS) huku kiwango cha fedha kikipanda kutoka Sh382 milioni hadi Sh1.3 bilioni.

Agosti 28, 2023  zaidi ya watu 40 wakiwamo madiwani, watumishi, watalaamu wa Tehama na watendaji wa kata walishikiliwa na Takukuru kwa tuhuma za wizi wa kutumia mtandao kwenye makusanyo ya ushuru.

Akizungumza leo Alhamisi Mei 2, 2024, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mbeya, Maghela Ndimbo, amesema baada ya uchunguzi wamebaini watu wengine sita kuongezeka katika uhalifu huo.

Amesema awali watu 31 walikamatwa huku 11  kati yao walikutwa hawana hatia na kubaki 20 waliofunguliwa kesi ya uhujumu uchumi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya.

“Uchunguzi wa awali, watuhumiwa walikuwa 31 baadaye 11 wakabainika kutohusika na kuachiwa huru; baadaye 14 walifikishwa mahakamani kwa kesi ya uhujumu uchumi.

“Wengine sita walifunguliwa kesi katika Mahakama ya Wilaya ya Mbarali kati yao watano wako nje kwa dhamana na mmoja amerudishwa mahabusu kwa kukiuka masharti ya dhamana,” amesema Ndimbo.

Ndimbo ameongeza kuwa baada ya majalada kuwasilishwa makao makuu, mkurugenzi wa mashtaka alielekeza kufanyike uchunguzi zaidi ndipo Takukuru iliwabaini wengine sita kuhusika katika uhalifu huo na kufikia jumla ya watuhumiwa 26.

“Lakini kiasi cha fedha kimeongezeka na kufikia Sh 1.3 bilioni; fedha hizi hazijajumuisha hasara iliyopatikana kwenye kesi zilizofunguliwa,” amesema Ndimbo.

Wakati huohuo, kiongozi huyo wa Takukuru amesema katika kipindi cha mieizi mitatu (Januari – Machi), Takukuru imefanikiwa kurejesha nyumba ya mjane Emelda Omary, mkazi wa Mbarali.

“Huyu mjane nyumba yake ilitwaliwa kinguvu baada ya mwanaye Tamimu Halifa, kukopa Sh6 milioni kwa Baraka Mboya na kuiba hati aliyoiweka kama dhamana bila mama yake kujua.

“Baada ya kufuatilia tulibaini mkopaji hakufuata utaratibu na Takukuru kuamua nyumba irejeshwe kwa mjane huyo, huku mwanaye kuamriwa na Mahakama ya Mwanzo ya Chimala kurejesha fedha hizo au kutumikia kifungo cha miezi sita,” amesema.

Ndimbo amesema matarajio yao kwa miezi mitatu ijayo ni kuendelea kutekeleza programu ya Takukuru rafiki, kuzuia rushwa kupitia uchambuzi wa mifumo na kuwachukulia hatua watuhumiwa wa vitendo vya rushwa.

Related Posts